Monday, 17 October 2016

MASOMO YA MISA, Dominika ya 29 ya Mwaka.

Dominika 29 ya Mwaka

        SOMO LA 1
               Kut 17:8-13
         Wakati huo Waamaleki wakatokea, wakapigana na Israeli huko Refidimu.
Musa akamwambia Yoshua, Tuchagulie watu, ukatoke upigane na Waamaleki; kesho nitasimama juu ya kilele kile, na ile fimbo ya Mungu nitakuwa nayo mkononi mwangu. Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima. Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda.
Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa. Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga.

        WIMBO WA KATIKATI
             Zab 121
          Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.
                   (K) Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.
          Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye; Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.
                    (K) Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.
             Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume. Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku.
                   (K) Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.
              Bwana atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.
                  (K) Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.

        SOMO LA 2
              2Tim 3:14- 4:2
           Wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema. Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake; lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho.

         SHANGILIO
              Yn 17:17
           Aleluya, aleluya Neno lako ndiyo kweli, ee Bwana; Ututakase sisi kwa ile kweli Aleluya
 

         SOMO LA INJILI
        Lk 18:1-8
                  Yesu aliwaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.
Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?

No comments:

Post a Comment

"Asante sana kwa maoni yako"

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...