JUKWAA LA UJUZI

Karibu katika ukurasa huu tujifunze zaidi

JUKWAA LA UJUZI


HIJA
Utamaduni wa hija ni wa zama kama ulivyo ubinadamu wenyewe. Hija ni safari takatifu. Hija ni safari ya kiroho. Mazoea ya kawaida ni kuichukulia hija kuwa ni safari ya kutoka eneo moja kwenda eneo takatifu kutokana na historia yake. Jambo hilo ni sahihi kabisa. Lakini jambo la msingi na muhimu kabisa ni kuiona hija kuwa ni safari ya kiroho. Safari ya uongofu na utii kwa Mungu. Safari hii ya uongofu wa ndani ndiko kuabudu katika roho na kweli (Yn 2:21; 4:21-24). 

Katika Agano la Kale tunaona mifano mingi ya hija. Hata hiyo, mifano miwili inachukua nafasi ya muhimu katika historia ya wokovu wetu. Kwanza, ni mfano wa Ibrahimu, aliye baba yetu wa imani. Ibrahimu anafanya hija ya kutoka katika nchi yake na kwenda kule Mungu anakomwelekeza (Mwa 12:1-9). Huyu ni hujaji ambaye utayari wake wa kumtii Mungu ni kielelezo cha imani


Pili, katika kitabu cha Kutoka, Taifa la Israeli linafanya hija ya wokovu kutoka utumwani Misri kwenda Nchi ya Ahadi (Kut 15). Kwa hiyo, hija ni tendo binafsi (Ibrahimu) na ni tendo la jumuiya (Taifa la Israeli). Lengo lake ni kukuza uhusiano na Mungu na ni fursa ya mtu kumtolea Mungu sala na maombi yake.

Agano Jipya na mafundisho ya Mababa wa Kanisa yanayachukulia maisha kuwa ni hija; yaani, safari ya kiroho kuelekea Yerusalemu ya mbinguni. Kwa hiyo, maisha yote ya Mkristo ni hija, ni safari hii ya kukua katika uhusiano wa kina na Mungu.

Katika Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu Benedikto XVI amewahimiza waamini wakatoliki kuhiji katika vituo maalum vya hija vya kijimbo, kitaifa, na vya kiulimwengu, ili kuchota neema maalum. Pia, Baba Mtakatifu ametangaza pia kuwa waamini watakaotimiza masharti ya Rehema Kamili wapewe rehema.




REHEMA
Kanisa, kwa mamlaka na nafasi yake katika mpango wa ukombozi, linaweza kutoka rehema kwa waamini wake. Rehema iwe ya muda au kamili, "ni msamaha mbele ya Mungu wa adhabu ambazo kosa lao limekwishafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata kutoka katika 'hazina ya malipizi ya Kristo na ya watakatifu'" (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, n. 1471). Hii maana yake nini?

Mtu anapotenda dhambi anaharibu uhusiano wake na Mungu. Mtu anapotubu na kuungama dhambi zake, anajipatanisha na Mungu. Hapo anapewa malipizi ya kufanya. Kwa nini? Kwa sababu, dhambi inamtia mtu jeraha. Maungamo yanamponya jeraha, lakini kovu la dhambi linabaki na ndiyo maana mtu anapewa malipizi na anashauriwa kuendelea kutolea sadaka mbalimbali kama sehemu ya malipizi, ili kufuta makovu ya dhambi. Kipimo cha malipizi kamilifu hakuna anayekijua ila Mungu mwenyewe. Malipizi anayotoa padri ni kumwanzishia mwamini tendo la malipizi. 

Kanisa linafundisha kuwa wakatoliki wana mahali linapoweza kukimbilia. Ni kukimbilia kwenye  "hazina ya malipizi ya Kristo na ya watakatifu", ili kutoka humo watu watakaswe makovu ya dhambi zao. 

Hii ni kwa sababu hazina ya malipizi ya Kristo hayana mipaka na yapo kwa ajili yetu. Pia hazina ya malipizi ya watakatifu ambao kupitia "ushirika wa watakatifu" tulionao na watakatifu. 

Rehema inaweza kuwa ya muda au kamili. Rehema ya muda huondoa sehemu ya adhabu za dhambi na rehema kamili huondoa adhabu zote (rej. Katekisimu ya Kanisa Katoliki, n. 1472).

Mkristo anaweza kupata rehema kamili yeye binafsi au kwa ajili ya marehemu kama atatimiza yafuatayo:

1.Awe na nia ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa.

2.Apokee Sakramenti ya Upatanisho (Maungamo)

3.Apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo

4.Asali kwa nia za Baba Mtakatifu (Hizi ni nia mbalimbali ambazo Baba     Mtakatifu analialika Kanisa zima kuliombea ama Kanisa au ulimwengu)

5. Atembelee Kanisa au kituo maalum cha hija kilichotangazwa rasmi.


No comments:

Post a Comment

"Asante sana kwa maoni yako"

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...