MASWALI
YAHUSUYO IMANIkaribu sana kwa majibu mazuri ya maswali mengi yahusuyo imani yetu. Pia umaweza kuuliza swali lolote nasi tuta kutafutia majibu mazuri kutoka kwa Baba zetu wakiroho kalibusana.
<uliza swali hapa>
SWALI:
Tumsifu Yesu kristu. Asante kwa mafundisho mazuri mnayotupa. Swali langu ni moja tu nahitaji kupata majibu kibiblia ili niwe huru kuitetea imani yangu.
Swali ni hivi Padri anauwezo wa kutuondolea dhambi? Na je, imeandikwa wapi tuungame dhambi zetu kwa padre? Hili jambo uwalinanipa wakati mgumu kulijibu.
JIBU:
Kabla ya kulijibu swali lako kwa undani zaidi, tutafanya vyema kwanza tukiandika machache kidogo kuhusu Sakramenti hii takatifu ya Kitubio. Si Kanisa Katoliki peke yake linalofundisha na kuiishi Sakramenti hii. Makanisa yote ya Kitume ya Mashariki (Orthodox) nayo huwapatia waumini wake Sakramenti ya Kitubio.
Pia Makanisa mawili ya wenzetu Wakristu Waprotestanti (Waanglikana na Walutheri) waliogawanyika katika aina mbili yaani High church na Low church, wenzetu Waanglikana na Walutheri wa High church wao pia wanafundisha imani hii ya uondolewaji wa dhambi kwa njia ya Kitubio japo hawaiti imani hii Sakramenti. Nchini Tanzania Makanisa haya ni yale ya Low church ndio maana hatuoni kwa sana waumini wao wakienda kupata kitubio.
Sasa turudi kwenye maswali yako. Moja linauliza, Padri anauwezo wa kutuondolea dhambi? Swali hili linatukumbusha mshtuko wa Wafarisayo walioupata baada ya Yesu kusema amemsamehe dhambi yule aliyepooza aliyeletwa kwake. Walishtuka wakisema “…….Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake” (Marko 2:7). Yesu akijua mawazo yao anawaambia “…..nataka mjue kwamba Mwana wa Adam anayo mamlaka ya kuwasamehe watu dhambi duniani” (Marko 2:10). Neno la kuelewa hapa ni “mamlaka”. Kristo ndiye Mamlaka ya juu kabisa na ndiye mtoa mamlaka hayo kwa wengine hata sisi Binadamu. Wengi wanasahau kwamba ndiye Kristo huyu huyu aliyempa mamlaka hayo Yohana Mbatazaji kwa maana wakati Yohana anabatiza umati mkubwa ulimfuata kutoka “….Yerusalemu na Uyahudi wote na nchi zote za kandokando ya Yordani….(Luka 3:5). Watu walikua ni wengi sana na yeye akawabatiza “…..huku wakiziungama dhambi zao”(Luka 3:5). Mara nyingi wanaopinga kitubio hukwepa kuona ukweli huu. Watu walimfuata Yohana na kuungama dhambi zao ndipo akawabatiza. Ndio maana Paulo anasema ubatizo wake ulikua ni wa toba (Matendo 19:4). Lakini japo Yohana alikua ni nabii (Mathayo 11:9), pia kutokana na tamaduni za Kiyahudi, alikua pia ni Kuhani/Padri kwa kuwa alikua ni mtoto wa kiume wa kwanza wa Kuhani Zakaria (Luka 1:5). Lakini uwezo wake wa kufanya watu waungame dhambi mbele yake na kuwaondolea kwa njia ya ubatizo (Matendo 19:4) ulitokana na Mamlaka aliyopewa na Kristo kwa maana Yohana ndiye aliyemtangulia na kumwandalia njia (Luka 1:76) ili mioyo ya wengi ifanye toba kabla ya kuja kwake Kristo. Mungu ndiye anayeondoa dhambi za binadamu, Kuhani ama Padre anatumika kama chombo baada ya kupewa mamlaka hayo. Hii inajidhihirisha hata Agano la Kale ambapo watenda dhambi, ili kupata msamaha iliwapasa kuleta sadaka hekaluni na huko kama ilivyoandikwa “…..kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake… kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya; naye atasamehewa hiyo dhambi yake aliyoifanya” (Mambo ya Walawi 19:22). Hivyo toka Agano la Kale mpaka Jipya Kuhani ama Padre anatumika kama chombo cha upatanisho. Anapewa mamlaka lakini anayefanya kazi hiyo ni Kristo mwenyewe kupitia chombo hicho yaani Padre.
Mahala gani katika Agano Jipya Kristo anatoa mamlaka hayo?
Jibu la swali hili hapo juu ndilo pia linalojibu swali lako la pili, kwamba imeandikwa wapi tuungame dhambi zetu kwa Padre? Tayari tumeshaona hapo juu imani ya wenye dhambi kuwafuata Makuhani ili wapate ondoleo la dhambi. Kristo aliyesema kuwa “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati…”(Mathayo 5:17), alifahamu fikra tamaduni hiyo na ndio maana wakati alipotengeneza makuhani ama mapadre wapya, pia anawaambia “ WOWOTE MTAKAOWAONDOLEA DHAMBI, WAMEONDOLEWA, NA WOWOTE MTAKAOWAFUNGIA DHAMBI WAMEFUNGIWA (Yohana 20:23). Kabla ya haya aliwaambia “….kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi” (Yohana 20:21). Wote tunakiri kuwa Kristo alitumwa na Baba kuikomboa dunia na kuwaondolea watu dhambi. Hivyo katika hali ile ile, anawatuma wafuasi wake wafanye kama yeye lakini kwa kupitia yeye ambaye ndio njia. Mamlaka haya aliwapa wafuasi wake baada ya kukalimisha yote. Aliwaambia haya baada ya ufufuko wake.
Sasa swali lako la pili lajibiwa na swali jingine. Je, Kristo angeweza vipi kutoa mamlaka haya kwa Mitume wake bila kufahamu fikra kwamba itatupasa sisi wenye dhambi kwenda kwao kwa ajili ya kuondolewa dhambi? Watawezaje kutuondolea dhambi kama sisi wadhambi hatutawaeleza madhambi yetu kwa njia ya maungamo? Tutafakari
Ndio maana Mtume Paulo yeye alielewa fikra mamlaka aliyopewa na Kristo ndio maana anasema “…….kwa maana mimi nami, ikiwa nimemsamehe mtu neno lo lote, nimemsamehe kwa ajili yenu mbele za Kristo (2 Wakorinto 2:10).
Wakatoliki tuikimbilie Sakramenti hii ya kitubio. Tunazo dhambi nyingi sana tunazitenda kila saa (kwa mawazo, kwa maneno na kwa kutotimiza wajibu). Mababa Watakatifu 3 waliopita wanatufundisha vizuri. Papa Francis yeye huenda kupata kitubio kila baada ya wiki 2, Papa Mstaafu Benedikti XVI yeye huenda kila wiki na Papa Mt. Yohane Paulo wa pili yeye pia alienda kupata kitubio kila wiki. Kama wakuu hawa wa Kanisa waliobeba kazi kubwa hujiona wadhambi na kuhitaji Sakramenti hii, ni mara ngapi zaidi kwetu sisi wadogo tunaokumbwa na kazi za hapa na pale na kuzisahau neema za Kanisa? Tutafakari
Bwana akubariki mtumishi
ReplyDelete