Somo: 1Kor 15:35-37, 42-49
Zab/Kit: 56:10, 11-12, 13, 14
Injili: Lk 8:4-15
Nukuu
“Lakini labda mtu atasema, Wafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili gani?” 1Kor 15:35
“Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo,” 1Kor 15:36-37
“Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake; naye alipokuwa akizipanda, nyingine zilianguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila,” Lk 8:5
“Nyingine zikaanguka penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa moja kwa mia. Alipokuwa akinena hayo alipaza sauti akisema, Mwenye masikio ya kusikilia, na asikie,” Lk 8:8
“Na wale penye mwamba ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga,” Lk 8:13
“Na zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote,” Lk 8:14
“Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia,” Lk 8:15
TAFAKARI:
“Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia.”
Wapendwa wana wa Mungu,Leo Yesu anatupa mfano wa Mpanzi akitutaka kuujenga uhusiano mzuri na Mungu kupitia neno lake. Simulizi hili la Mpanzi linasimuliwa na wote watatu-‘fanana,’ (Mt 13:1-9, 18-23; Mk 4:1-20, Lk 8:4-15). Neno la Bwana ni uzima kwetu na neno hilo hututoa mautini na kuingia uzimani. “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani,” Yoh 5:24. Maadui wa neno la Mungu wa kwanza ni shetani na hila zake. Ila shetani wa mtu ni mtu mwenyewe.
Unaporuhusu hali ya ukavu ndani ya maisha yako ndivyo hivyo hivyo unavyo yapalilia makazi ya shetani ndani ya nafsi yako. Hawa ndio zile mbegu “zilizoanguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila,” Lk 8:5. Ni vyema kila siku ukawa hata na dakika 15 za kulisoma neno la Mungu na kulifanya lako. Usomapo neno hilo jiulize linasema nini juu ya maisha yako.
Adui wa pili kuhusu neno la Mungu ni dhiki na udhia katika maisha yetu. Katika dhiki za maisha na udhia Yesu anatuambia neno la uzima kwamba Yeye kesha ushinda ulimwengu hivyo tuwe na imani ndani yake. Naye Yesu anasema, “Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami. Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu,” Yoh 16:32-33.
Ndugu yangu bila kushikamana na Kristo aliyeushinda ulimwengu katika dhiki na udhia hutaweza kuushinda ulimwengu huu kwa nguvu zako mwenyewe. Kuzitumainia nguvu zako ni kuelekea kushindwa kabisa. Hawa ni zile mbegu “Nyingine zilizoanguka penye mwamba; zilipoanza kumea zikakauka kwa kukosa rutuba,” Lk 8:6
Adui wa tatu wa neno la Mungu ni shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine. Leo watu wengi lengo la maisha yao yote huongozwa na tamaa ya kupata vitu. Msukumo huu wa kutaka zaidi kila siku una misingi yake katika udanganyifu wa kuwa nikiwa na vingi nitakuwa na furaha zaidi, nitakuwa wa muhimu, na nitakuwa salama; lakini mawazo hayo yote matatu si ya kweli. Hawa ni kama mbegu zile “zilizoanguka kati ya miiba, na miiba ikamea pamoja nazo ikazisonga,” Lk 8:7. Mali huleta furaha ya "muda mfupi tu." Na sababu kubwa ndugu yangu, vitu havibadiliki, hivyo vinatuchosha na tunataka vipya, vikubwa, na bora zaidi.
Kuna imani pia kwamba nitapata mali nyingi nitakuwa wa muhimu. Umuhimu wako na mali ni vitu viwili tofauti. Thamani yako haitegemei mali zako, Mungu anasema kitu cha muhimu maishani mwako si vitu! Imani ya watu wengi kuhusu fedha ni kwamba kuwa nazo nyingi kutanipa usalama. Huwezi! Yesu anawaambia wale wafuasi wa Yohane Mbatizaji, “Mnatafuta nini?” Wanafunzi wale wakamjibu, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi?” Yoh 1:38. Anapokaa Yesu ndipo kwenye usalama kupita vitu vyote na hali zote tunazoweza kufikiria. Mt. Augustino anasema, “mioyo yetu haitulii mpaka itakapotulia kwako Ee Bwana.”
Ndugu yangu, utajiri unaweza kupotezwa mara moja kwa sababu zisizozuilika. Usalama halisi unaweza kupatikana katika kile ambacho huwezi kunyang'anywa yaani uhusiano wako na Mungu. Hawa ni mbegu zile “zilizoanguka penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa moja kwa mia,” Lk 8:8a. Mt. Augustino anatuwasa kutoka kwenye kanuni yake, "kuna furaha kubwa kuwa na vichache kuliko kuwa na vingi." Hata hivyo tatizo hapa ni kipimo cha huo uchache na huo wingi. Uzima wetu upo katika neno la uzima nalo ndilo ngao yetu katika ulimwengu huu kigeugeu.
Ili neno la Mungu liwe tumaini la kweli, na ushuhuda wa kweli ndani yetu, na kwa wale wanaotuzunguka, lazima neno hilo tulisikie, tulipokee, kulitafakari, kulishirikishe, na mwisho tuwe sehemu ya neno hilo kwa kuwa mashahidi wa neno hata ikibidi kufa kwa kweli hiyo. Kulipokea neno lazima uwe na utayari wa kulisikia neno. Usipokuwa na utayari huu ni sawa na mbegu zile “zilizoanguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila,” Lk 8:5. Na huu ndio ufafanuzi wa Yesu; kwamba, “Wale wa karibu na njia ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka,” Lk 8:12
Kulitafakari neno la Mungu kunakuhitaji kulisikia neno hilo na liguse maisha yako. Kutafakari neno ni kama kucheua kile ulichokula. Kama hili halikufanyika ni sawa na mbegu zile “zilizoanguka penye mwamba; zilipoanza kumea zikakauka kwa kukosa rutuba,” Lk 8:6. Na hapa Yesu anatuambia kwa kuifafanue lugha ile ya picha, kwamba, “wale penye mwamba ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga,” Lk 8:13. Kulipokea neno kwa furaha na kukosa mizizi ndani yake, ni kukosa tafakari ya kina juu ya kile ulichokisikia au kukisoma. Ni kutokulicheua neno, na hivyo neno hilo kutokuwa sehemu ya maisha yako, na kutokukupa uwezekano wa kulishirikisha kwa wengine. Huwezi kutoa usichokuwa nacho. Je, itawezekana kweli kushirikisha kwa wengine kile usichokuwa nacho?
Wapendwa wana wa Mungu, kuwa na uwezo wa kulishirikisha neno la Mungu kunategemea sana namna tunavyolicheua neno la Mungu, yaani, uwezo ule wa kulitafakari neno la Mungu na kuleta mabadiliko kwanza ndani yetu. Tunaposhindwa kufanya hivyo ni sawa na mbegu zile “zilizoanguka kati ya miiba, na miiba ikamea pamoja nazo ikazisonga,” Lk 8:7. Kumbe tunaweza kushirikishana neno la Mungu vizuri pale tunapokuwa na mazingira mazuri ya kulitafakari neno la Mungu kama lilivyo, na siyo tulivyo kwa kujionea huruma. Na hapa Yesu anafafanua lughu hii ya picha na kusema, mbegu zile “zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote,” Lk 8:14. Leo ni wangapi tu sehemu ya Jumuiya ndogo ndogo iliyopo kwenye eneno lako, ikiwa ni pamoja na kwenda kwenye jumuiya hiyo na kuwa sehemu ya familia hiyo, ukiumega mkate na kushirikishana neno la Mungu?
Leo jumuiya hizi sehemu nyingi zimekuwa kundi la watoto, akina mama, tena wajane, na wazee. Hakuna vijana, na wala hakuna akina Baba. Je, hayo malimwengu unayoyakubatia yana uzima ndani yake au umebaki kujifariji katika upumbavu?Tukifanikiwa katika hatua hii, yaani, kuliishi neno la Mungu, ni wazi tu mashahidi wazuri wa neno la Mungu ndani yetu na wale wote wanaotuzunguka.
Kuwa mashahidi na washuhuda wa neno ni sawa na mbegu zile zilizoanguka “zilizoanguka penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa moja kwa mia,” Lk 8:8a. Hiki ndicho atakacho Yesu kwako na kwangu, yaani, tuwe mashahidi wa kweli wa neno la Mungu. Na huu ndio ufafanuzi wa Yesu juu ya udongo mzuri; “ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia,” Lk 8:15. Kuzaa huku matunda kwa kuvumilia kunatokana na nguvu ya Roho ile isukumayo ufahamu wetu juu ya neno ambalo sasa siyo tu tumelisika, bali tumelipokea. Na siyo tu tumelipokea, bali tumelitafakari kwa kina na kulicheua. Na siyo tu tumelitafakari kwa kina na kulicheua, bali kwa sasa tumelishirikisha vyema kwa wengine (uinjilishaji upya).
Na mwisho siyo tu tumelishirikisha neno hilo kwa wengine bali tumekuwa sehemu ya neno hilo, kwa kuwa mashahidi na washuhuda wa kweli kwa sababu maisha yetu yanaakisi kweli hiyo. Kumbe haitoshi kufanya mambo mazuri katika ukamilifu wake, bali yakupasa kuwa mkamilifu katika maana halisi ya ukamifu kama anavyotuasa Yesu, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48.
Wapendwa wana wa Mungu, kwa tafakari hiyo ya kina kutoka somo la Injili ya leo, inatusaidia kulifahamu somo letu la kwanza kutoka waraka wa Mtume Paulo kwa Wakorintho kama tulivyokwisha kulisikia. Somo hili linaongelea juu ya maisha ya uzima wa milele na mwonekano wake. Jambo la maana na la msingi katika maisha yako hapa duniani leo na sasa ni kulenga katika ukamilifu ingawa udhaifu upo. Ni kulishika neno la Mungu na kuwa shahidi na shuhuda wa neno hilo.
Ni kujitahidi kila siku kufanya mambo yote katika ukamilifu na kuwa mkamilifu licha hapa na pale tunadongoka. Na pale tunapodongoka tusiiache Huruma na Neema ya Mungu kwa kupatanishwa naye. Swali labda mtu atafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili gani? 1Kor 15:35, halina maana sana kama hatutajianda vyema kwa muda huu mfupi tukiwa hapa duniani.
Aulizaye swali kama hili bila kufanya chochote, Mtume Paulo anamfananisha na mpumbavu. Na mpumbavu ni mtu yule ajifanyaye anajua kumbe hajui chochote. Naye Paulo Mtume anasema, “Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo,” 1Kor 15:36-37. Ni wazi kwamba miili yetu katika maisha ya umilele haitakuwa na mwonekano huu tulio nao. Miili baada ya ufufuko ni miili ile iliyotufukuzwa, na isiyo shikiliwa au zuiliwa na wakati na nafasi.
Kiyama, yaani, hukumu ya mwisho inategemea sana na haya unayoishi leo na sasa. Siku ya hukumu ya mwisho kitakachofanyika ni kuridhiwa-‘ratification’ kwa kile ulichokiishi. Kumbe kwa namna tunavyoishi ndivyo tunavyojiandalia palipo pema ama pabaya. Hivyo,“kadhalika na kiyama ya watu. Hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutokuharibika,” 1Kor 15:42. Katika ishi yako leo ambayo upingana na matamanio ya ulimwengu huu, kwa wengine ni aibu na udhaifu, ila kwa Mungu ni fahari na nguvu. Na siri ya maisha ya uzima wa milele ndiyo hii kwamba, “hupandwa katika aibu; hufufuliwa katika fahari; hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa katika nguvu,” 1Kor 15:43.
Tungali hapa duniani Mungu ametuita kama tulivyo, yaani, binadamu aliyeumbwa na sura na mfano wake. Na katika ubinadamu huo na udhaifu wake, tukiishi kwa uaminifu na kuushinda ubinadamu huo, hapo ndipo ulipo pia utakatifu wetu. Hivyo utakatifu huo, ukamilifu, huo, “hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko,” 1Kor 15:44. Ndugu yangu, usitamani kuwa kitu kingine ambacho sicho kusudi la Mungu ndani yake, yaani, hasa wale wenye matamanio ya kuyabadili maumbo yao na hata jinsia zao.
Wapendwa katika Kristo, wakutugeuza na kuwa kitu kingine na kwa namna nyingine ni yule yule lifanya hilo mwanza, yaani, Mungu aliyekuumba wewe na mimi na sura na mfano wake, Mwa 1:27. Ni katika mantiki hii, Mtume Paulo anafanya linganisho la mtu wa kwanza-Adamu, na Adamu wa mwisho-mwili ule uliotukufuzwa. Na “Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha,” 1Kor 15:45. Na kuupata mwili huu uliotukufuzwa-wa roho, yatupasa kuishi mwili huu wa asili katika ukamilifu wake licha ya udhaifu wake. Ni kwa maana hiyo, “hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho,” 1Kor 15:46. Hakuna utukufu pasipo Msalaba, na penye teso ndipo penye utukufu.
Baada ya maelezo hayo ya kina kuhusu ubinadamu wetu na asili yake hadi kutufukuzwa kwetu, Mtume Paulo anatupeleka hatua ya pili kwa kufanya linganisho la sisi kama wanadamu, na Neno aliyefanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Huyu ndiye Kristo Yesu. Na hii ndiyo maana ya maneno haya kwamba, “Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo (mwanadamu). Mtu wa pili atoka mbinguni (Neno aliyefanyika mwili na kukaa kwetu),” 1Kor 15:47. Ni katika maana hii tunaweza sasa kuongelea hali zetu katika ubinadamu wetu, na hali zao walioufikia ukamilifu kama Mungu alivyo mkamilifu, Mt 5:48. Na Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, alichukua asili mbili, yaani, Mwanadamu na Mungu.
Na kwa Ubinadamu wake na Umungu wake, Kristo Yesu aliikamilisha kazi ile ya kumkomboa mwanadamu katika ubinadamu wake kutoka utumwa wa dhambi na kumwinua katika hali ya umungu kwa Umungu wake Kristo Yesu. Ni kwa namna hiyo kwamba, “Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni,” 1Kor 15:48. Na huu ndio ukweli kwamba, ndani na katika Kristo Yesu, “kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni,” 1Kor 15:49. Hili liliwezekana tu ndani na katika Kristo Yesu, aliyekuwa na asili hizo mbili, yaani, Mungu na Mwanadamu angali hapa duniani.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo,” 1Kor 15:36-37
Tusali:-Ee Yesu Mwema, tufanye udongo mzuri. Amina
No comments:
Post a Comment
"Asante sana kwa maoni yako"