Thursday, 15 September 2016

"HURUMA YA MUNGU NIYA MILELE".
   
    KUMBUKUMBU YA BIKIRA    MARIA MAMA YETU WA           MATESO


Somo: 1Kor 15:1-11
Zab/Kit: 118:1-2, 16ab-17, 28
Injili: Yoh 19:25-27
Nukuu
Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu,” 1Kor 15:9 

Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami,” 1Kor 15:10 

Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene,” Yoh 19:25 

Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao,” Yoh 19:26

Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake,” Yoh 19:27

TAFAKARI: 
Mama, tazama, mwanao. Mwana tazama, mama yako.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya Bikira Mama Yetu wa Mateso. Wapendwa katika Kristo, ukiyatazama maisha yako na jinsi Mungu anavyoendelea kuwa upendo na huruma kwako, hakika yote ndani yetu ni kwa neema ya Mungu. Hakika, “Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?” Zab 130:3. Mungu huyu aliye Huruma na Neema anajidhihirisha wazi katika historia mbaya aliyokuwa nayo Sauli wa Tarso.

Leo kwa neema ya Mungu, Paulo anajulikana kama Mtume. Paulo anatoa ushuhuda wa maisha yake na kusema, Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu,” 1Kor 15:9. Hata pamoja na ukweli huo, huruma na neema ya Mungu ni kubwa zaidi ya uovu wako kama utajisalimisha kwake. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami,” 1Kor 15:10Mungu yupo tayari kuanza upya nawe endapo tu kama upo tayari. Hizi ni neema za Mungu zinazotuzunguka kila wakati. Na kwa namna ya pekee mwaka huu wa Kanisa wa huruma ya Mungu ni wakati wa kutumia fursa hiyo vizuri.

Wapendwa wana wa Mungu, leo tunapo mtafakari Mama Bikira Maria kama Mama wa wateso, tafakari hii inatupeleka moja kwa moja katika tukio lile kubwa la kukombolewa kwetu pale Golgota-fufu la kichwa, ambapo kadiri ya masimulizi, Bikira Maria na Mtume Yohana walikuwa chini ya Msalaba Yesu alipotundikwa juu yake. Katika tukio hili, Bikira Maria anashiriki moja kwa moja mateso ya Mwanaye Mpendwa akiwa na sitofahamu nyingi moyoni mwake. Bikira Maria kama Mama, bado anakumbukumbu dhahiri moyoni mwake ambazo leo inakuwa kinyume chake. Naomba nikurudishe nyuma ili uelewe mambo mazito yaliyokuwa ndani ya moyo wa Mama Maria ambayo leo katika tukio hili anakosa majibu yake.

Ndugu yangu tunaye safiri sote katika tafakari hii, katika tukio lile la kupashwa habari Mama Bikira Maria aliambiwa haya na Malaika Gabrieli;Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake,” Lk 1:31-32. Bikira Maria alijiuliza haya moyoni mwake akiwa chini ya Msalaba ule aliye tundikwa mwanaye, ‘haya ndiyo hayo makuu ya mwana wa aliye juu na Bwana Mungu ndiye ameamua kumpa kiti cha mtindo huu?’ Kama Mama, Bikira Maria alikuwa na uchungu mkubwa sana! Hili ni jaribu kuwa sana la Imani kwa Mama Bikira Maria.

Bikira Maria katika hali hii ya uchungu alitafakari pia aliyoambiwa na Malaika Gabrieli kwamba,Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho,” Lk 1:33. Matokeo yake leo anaona Mwanaye Mpendwa kusubishwa kati ya waovu, wezi wawili. Maswali yake ni haya; Mungu anawezaje kuruhusu hali hii? Na katika hali na mazingira haya ya fedheha awezaje basi Mtoto wangu kuwa na utawala usio na mwisho? Hata hivyo, Bikira Maria aliendelea kubaki chini ya Msalaba akiamini pasipo shaka neno hili la Mwanaye, “NITAFUFUKA!”

Bikira Maria kama Mwanamke na Mama, ni taswira hai ya Mungu Baba aliye ishi ufu wa mtoto wake. Mungu katika tukio hili kama Mama amemtaka sadaka kubwa sana. Tukio hili la Mama Bikira Maria linatufikirisha sadaka ile ya Ibarahimu aliyokuwa tayari kuitoa kwa Mungu kwa mwanaye Mpendwa Isaka, Mwa 22:1-14. Kutoka na tukio hili, Bikira Maria anaufunua ufahamu mkubwa na waajabu kuhusu Mungu, kutoka ndani ya moyo wake kama mama. Bikira Maria ni mtu pekee anayeshirikishwa mateso, uchungu, mahangaiko ya Mungu katika hali ya kibinadamu katika ushirikishwaji wa thamani ile ya kukombolewa.

Katika hali hii ya kushiriki mateso ya Mwanaye Yesu Kristo, Bikira Maria anapewa hadhi ya kuwa Mama wa wanadamu yote bila kujali leo itikadi zao kiimani. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao,” Yoh 19:26. Kwa tendo hili na kifo chake Bwana wetu Yesu Kristo, sadaka yake Kristo pale Msalabani ni kwa binadamu wote. Kama Mama katika ushiriki wa mateso haya, alichokitaka Mwanaye ni sawa na alichokitaka Mama yake kama waswahili wasemavyo, “uchungu wa mwana aujuaye mzazi wake.” Umama aliopenda Bikira Maria kama Mama ni hali hiyo aliyotupenda Yesu upeo hata kuyatoa maisha yake kwa ajili yako na yangu. Ni katika mantiki hii, Bikira Maria anashiriki kazi ya ukombozi wa mwanadamu, na kuzaliwa kwa ubinadamu mpya kwa imani na kwa umoja na Kristo.

Neno “Mama, tazama, mwanao,” Yoh 19:26, ni kweli yetu halisi kuhusu wito wetu. Yesu anaendelea kutuambia kwamba sisi ni wana wa kweli katika mwana. Yesu amekwisha fanywa ndugu yetu. Na katika kweli hii, sisi kama wafuasi wa Kristo, Mama Maria ndiye Mama Yetu. Ni wito wetu sasa kumchukua Mama Maria katika mioyo yetu kwa sababu uhakika huo tunao. Ni katika maana hiyo kwamba, “tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake,” Yoh 19:27. Mama Bikira Maria chini ya Msalaba aliishikilia tumaini ile ya ufufuko wa mwanaye Yesu Kristo pasipo shaka yoyote ile. Na katika uhimara huu wa imani, alisubiri ufufuko wa mwanaye.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake,” Yoh 19:27b


Tusali:- Ee Yesu Mwema, asante kwa uwepo wa Mama yako aliyeyashiriki Mateso yako. Nasi kwa kupitia Mama yako Mpenzi tushiriki Mateso yako.Amina

No comments:

Post a Comment

"Asante sana kwa maoni yako"

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...