Sunday, 11 September 2016

DINI NA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI DUNIANI!.

"HURUMA YA MUNGU NIYA MILELE".

Dini na mapambano dhidi ya Ukimwi duniani!


Viongozi wa kidini wanayo dhamana ya kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi duniani. - AFP
11/09/2016 10:44

   Wakristo pamoja na waamini wa dini mbali mbali duniani wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa kuwahudumia waathirika na wagonjwa wa Ukimwi sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kusaidia kuondokana na unyanyapaa na ubaguzi wanaofanyiwa wagonjwa wa Ukimwi duniani. Hii ni dhamana pia kwa watu wote wenye mapenzi mema, ili kusaidia kupambana na ugonjw wa Ukimwi pamoja na kuwapatia waathirika matumaini ya kuendelea kuishi.
Haya ndiyo yaliyopewa kipaumbele cha pekee wakati wa kongamano la kiekumene na majadiliano ya kidini, lililowakutanisha viongozi wa kidini na wadau mbali mbali wa mashirika ya kidini katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi duniani hivi karibuni huko Durban, Afrika ya Kusini. Kongamano hili la kimataifa liliongozwa na kauli mbiu “Imani iwe mstari wa mbele katika kuondokana na unyanyapaa na ubaguzi; kuongeza idadi ya wagonjwa wanaotibiwa pamoja na kulinda haki zao msingi”.
Kongamano hili lilihudhuriwa na wajumbe zaidi ya mia tano kutoka katika mashirika ya kidini na wadau mbali mbali ambao wako mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi. Kwa mara nyingine tena, mashirika ya kidini yameonesha umuhimu wa kushikamana kwa pamoja katika kuwahudumia waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi duniani katika ngazi mbali mbali pamoja na kusimama kidete kupinga unyanyapaa na ubaguzi wanaofanyiwa waathirika wa Ukimwi hasa zaidi kutoka katika Nchi zinazoendelea duniani.
Huu umekuwa ni wakati wa kushirikishana uzoefu na mang’amuzi mbali mbali kuhusu huduma kwa waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi; kwa kusimamia utu, heshima na haki zao msingi. Hii ndiyo njia muafaka ya kuweza kuwahudumia waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanapata tiba muafaka ya kuweza kurefusha maisha. Wajumbe walipata nafasi ya kusikiliza shuhuda mbali mbali zilizotolewa na watu waliobobea katika huduma kwa waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi.
Bi Faghmeda Miller kutoka Afrika ya Kusini, alitangaza hadharani kuwa ni muathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi na kushuhudia jinsi ambavyo alipambana sana hadi kukubali kwamba, alikuwa ameathirika. Sasa yuko mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, watu wengi wanapima afya zao, ili kuanza kupata tiba ya magonjwa nyemelezi pamoja na dawa za kurefusha maisha. Anawahimiza wagonjwa wote wa Ukimwi waliokwisha anza kutumia dawa za kurefusha maisha, kuendelea kuzitumia ili kuishi kwa matumaini.
Bi Laichhuanzulai Ralte kutoka India, alipokea tuzo ya Mary Robinson kutokana na ujasiri wake wa kusimama kidete kutetea utu na haki msingi za wanawake walioathirika kwa Ugonjwa wa Ukimwi nchini India. Ameelezea jinsi ambavyo tiba ya Ugonjwa wa Ukimwi kwa sasa imechukua mwelekeo mpya katika jamii kwani hii ni sehemu ya haki jamii, ushuhuda ambao umetolewa na waamini wa dini mbali mbali nchini India: kwa kuwapokea, kuwakarimu na kuwahudumia waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, kama kielelezo cha mshikamano wa huduma makini kwa waathirika na daraja la majadiliano ya kidini na kiekumene.
Wajumbe wa Kongamano la Ukimwi Duniani huko Durban, Afrika ya Kusini, walisikitishwa sana na ongezeko la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi miongoni mwa vijana wa kizazi kipya na kwamba, wengi wao bado hawajitambui kwamba, wameambukizwa na virusi vya Ukimwi, ili kuanza kupata tiba ya kurefusha maisha. Wajumbe wamejadili pia changamoto zinazoendelea kujitokeza katika mapambano dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi kutokana na ukata hali ambayo inapelekea wagonjwa wengi kushindwa kupata dawa za kurefusha maisha.
Mashirika ya kidini yanaendelea kuimarisha kampeni miongoni mwa vijana ili kupima afya zao, tayari kuanza kupata tiba kwa wale watakaogundulika kwamba, wameambukizwa virusi vya Ukimwi. Inasikitisha kuona kwamba, wasichana wengi waliobakwa ndio walioambukizwa pia virusi vya Ukimwi kadiri ya utafiti uliowasilishwa wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Ukwimi Duniani huko Durban, Afrika ya Kusini.
Kampeni za mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi haina budi kuwa na mwelekeo mpana zaidi kuliko mwelekeo wa sasa wa kujikita katika masuala ya afya peke yake. Sasa waamini na watu wote wenye mapenzi mema wasimame kidete kupinga nyanyaso na ubaguzi dhidi ya waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi kwani hili ni donda ndugu la kijamii, linalohitaji ushirikiano na mshikamano kutoka kwa wadau mbali mbali ili kujenga utamaduni wa ukarimu, huduma na upendo; mambo msingi yanayosaidia mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki na upendo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

No comments:

Post a Comment

"Asante sana kwa maoni yako"

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...