Wednesday, 14 September 2016

TAFAKARI YA MASOMO YA MISA, 14/9/2016 Sikukuu ya kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu.

"HURUMA YA MUNGU NIYA MILELE".

SHEREHE YA KUTUKUKA KWA MSALABA MTAKATIFU WA YESU KRISTO
Somo I: Hes 21:4b-9                                    
Zab: 78:1-2, 34-35, 36-37, 38
Somo II: Flp 2:6-11
Injili: Yoh 3:13-17
Nukuu:
Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi,” Hes 21:8

tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:8 

Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;  ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye,” Yoh 3:14-15

Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye,” Yoh 3:17

TAFAKARI: 
“Penye Msalaba pana uzima na uponyaji.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni kweli usiyotia shaka kwamba penye msalaba pana uzima na uponyaji. Tumekombolewa kupitia Msalaba: mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa mantiki hii tunajichukulia misalaba yetu kwa upendo  na bila shuruti tukiwa na Kristo aliyeushinda msalaba kwa utii na uvumilivu wote, tunauhakika wa uzima wa milele na uponyaji kadiri ya muda na wakati inavyompendeza Mungu.

Kivuli cha msalaba halisi wa Kristo kinaonekana kwa Waisraeli kwa njia ya nyoka aliyeinuliwa na Musa baada ya kutubu na kuiacha njia yao mbaya. Kupitia ishara hii, wana wa Israeli wanaponywa na kuishi. Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi,” Hes 21:8. Nyoka huyu wa shaba ni kivuli halisi cha msalaba halisi wa Kristo. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;  ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye,” Yoh 3:14-15. Mpango wa Mungu katika historia ya wokovu wetu hauwezi kusitishwa wala kupingwa kwa nguvu yeyote ile.

Leo tunapofanya sherehe ya kutukuka kwa msalaba Mtakatifu wa Yesu, tunatambua kwa kina kabisa kuinuliwa kwa fumbo zima la msalaba kama kielelezo cha wokovu, tukijua fika ni mti ambao wokovu wetu umetundikwa juu yake. Ukweli huu ndio unaotufanya sisi sote twende na kuabudu Msalaba Mtakatifu.

Ndugu yangu Msalaba kutukuka ni kielelezo cha unyenyekevu wetu kama wafuasi wa Kristo aliyeushinda msalaba kwa kujinyenyekeza hadi mwisho. Mtume Paulo anasema hivi;tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:8. Unyenyekevu ni msingi imara wa Imani yetu kote kwa matendo na kinadharia.

Ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo haukuwa na lengo la kutoa hukumu, bali tuwe na imani ya kweli na kuishi maisha ya umilele ikiwa ndiyo mpango mzima wa historia ya wokovu wetu.Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye,” Yoh 3:17

Wapendwa wana wa Mungu, hukumu ya Mungu itamfika kila mmoja wetu kwa kadiri ya kazi na wito wake. Basi yanipasa kuwa makini na mwaminifu katika kazi na wito wangu.
Tumsifu Yesu Kristo!

Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye,” Yoh 3:17


Tusali:-Ee Yesu, Msalaba wako unikumbushe wajibu wangu hapa duniani daima. Amina

Copy right© by Fr.Edgar Tanga ngowi,OSA
Published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG.
website:
ernestliapanga.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

"Asante sana kwa maoni yako"

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...