Tuesday, 27 September 2016

TAFAKARI: Jumanne wiki ya 26 ya Mwaka


JUMANNE WIKI YA 26 YA MWAKA-C

   Somo: 
   Ayu 3:1-3, 11-17, 20-23
    Zab/Kit: 88:2-3, 4-5, 6, 7-8
           Injili: Lk 9:51-56

      Nukuu: 
       “Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu,” Lk 9:53
       “Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?” Lk 9:54
            “Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]” Lk 9:55
             “Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa,” Lk 9:56a
              “Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake,” Ayu 3:1

         
            TAFAKARI:
             “Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.”
             Wapendwa wana wa Mungu, sehemu hii ya Injili n asomo letu la leo juu ya habari ile ya Ayubu, inafua ‘kweli ya Mungu’ ambayo hubaki kuwa ‘siri’ katika maisha yetu ya kila siku. Ni kweli kabisa katika hali na mazingira ambayo twateseka tu bila sababu ya teso hilo, maisha upoteza maana yake. Hii ndiyo hali aliyokuwa nayo Ayubu baada ya kupatwa na janga lile la majaribu na kuanza kulaani, Ayu 3:1.

         Kulaani kwa kile usichokijua vizuri hakutakufanya kuelewa fumbo la kile usichokijua vizuri. Kuzama katika fumbo usilolielewa ili upate maana yake ni kujiuliza swali hili; Je, katika jambo hili, Mungu wataka kunifundisha nini? Hakuna jaribu lisilo kuwa na mlango wa kutokea, 1Kor 10:13.
          Kuupata mlango wa kutokea ni kuachana na laana na laumu. Yesu Kristo aliye Mungu na Mwanadamu anaelekea Yerusalemu kwa kile kinachosimuliwa na Mwinjili Luka kama “siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia.” Je, kupaa bila kupitia mateso, kifo, na ufufuko? Mwinjili Luka halisemi jambo hili kwa kukosea. La! Hasha. Kupaa kwa Yesu ni hitimisho linalo elezea Wokovu ikiwa ndiyo lengo lengwa katika historia nzima ya mwanadamu (Yoh 1:14, Gal 4:4-5).
       
           Wokovu huo unathibishwa kwa Ufufuko wake Kristo Yesu. Ufukuko huo ni alama ya wazi ya ushinda dhidi ya kifo kilichokuwa adui yetu mkubwa. Na Kifo hicho cha Kristo Yesu ni alama wazi ya upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu kutuweka huru kutoka utumwa wa dhambi. Kwa maana nyingine, kupaa kwa Kristo kusingekuwa na maana kama kusingesema chochote kuhusu wokovu, ufufuko, na kifo. Na kuelekea Yerusalema katika maana ya “kukaza uso wake kwenda Yerusalemu,” kulimaanisha, mateso, kifo, wokovu, ufufuko, na kupaa. Hata pamoja na mpango huu mahususi uliobeba kilele cha historia mzima ya wokovu wa mwanadamu, jambo hili kwa ajabu kubwa na mshangao halimgusi mwanadamu. Hii ndiyo kweli ya Mungu inayobaki kuwa siri katika maisha ya mwanadamu. Na hii ndiyo maana ya maneno haya; “Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu,” Lk 9:53.
           
            Mwenye kufikiriwa kuhusu kesho na hatma yake itakuaje hana habari kabisa na kile anachofanyiwa. Kwa bahati nzuri au mbaya siri hii haikufichwa kabisa kwa baadhi ya wateule wa Mungu. Mwanga wa siri hii unafunuliwa kwa wanafunzi wake Yesu, kama asemavyo mwenyewe kwamba, “Ninyi mmepewa kuzijua siri za ufalme wa Mungu; bali wengine kwa mifano, ili wakiona wasione, na wakisikia wasielewe,” Lk 8:10.
           Kufunuliwa kwa siri hii kuna kuwa bahati mbaya kwa namna wanafunzi wake Yesu wanavyotafuta suluhu ya mambo hasa katika safari hii ya kuelekea Yerusalemu alipoyakazia macho yake Yesu. Na mambo yalikuwa hivi; “Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?” Lk 9:54. Yesu hakuja kufanya mwendelezo wa sheria ile ya jino kwa jino, bali kuitakatifuza na kuifanya kamili, Mt 5:17. Na lengo na uwepo wake Yesu siyo kuukumu ulimwengu bali ulimwengu uukolewe na yeye, Yoh 3:17. Ni wazi kabisa kwa kile walichoshupalia wanafunzi wake Yesu, Yakobo na Yohana cha onyesha kile kilicho ndani ya mioyo yao na ubinadamu wao. Na hapa ndipo Yesu “Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]” Lk 9:55. Yesu anawakanya wao na sisi leo kama Wakristo na Wafuasi wake kwamba mtindo wa jino kwa jino siyo staha na maadili yetu kama Wakristo. Kufanya hivyo ni kutokujua fumbo zima la wokovu wetu. Ukweli ni kwamba, “Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa,” Lk 9:56a.
         
          Tumsifu Yesu Kristo!
          “Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa,” Lk 9:56a Tusali:-Ee Yesu, tuondolee ile roho ya kukata tamaa na kuwa watu wa visasi. Amina

Copyright © 2016 by Fr Edgar Tanga Ngowi.OSA  and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
      see: imani-katoliki.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

"Asante sana kwa maoni yako"

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...