TAFAKARI
Alhamisi, Septemba 8, 2016.
Juma la 23 la Mwaka
Sikukuu ya Kuzaliwa Bikira Maria Mtakatifu
Mik 5: 1-4 au Rum 8: 28-30; Zab 12: 6; Mt 1: 1-16, 18-23
MUNGU ANA MPANGO NASI!
Bikira Maria Mama yetu, alichukuliwa mimba kitakatifu, alizaliwa na kuishi bila dhambi, na sasa anatuombea ili hata mmoja wetu asipotee. Sisi, wanawe tunafurahi kusheherekea sikukuu yake ya kuzaliwa. Kuhusu sikukuu ya leo Mt. Andrea wa Crete anasema,"viumbe vyote vilivyo umbwa viimbe sifa na kucheza na kwa pamoja viungane kuadhimisha utukufu wa siku hii...kwani leo hekalu limejengwa kwa ajili ya Muumba wa ulimwengu". Maria alizaliwa kama hekalu la Muumba, na kwa njia ya utii wake akatimiza lengo lake ambalo alizaliwa kwa ajili yalo. Kama Mungu alivyokuwa na mpango kwa Maria, kuzaliwa kwetu sio kwa bahati mbaya au makosa. Mungu ana mpango nasi. Kama Maria alivyotimiza lengo lake duniani, tunapaswa kutambua lengo letu katika maisha na kuwa waaminifu kwa lengo hilo. Tunapaswa kuheshimu maisha ya wengine pia, kwani Mungu naye ana mpango nao pia! Tuwaombee kwa namna ya pekee “ watoto wa kike” ambao siku hii pia ni maalumu kwa ajili yao pia Sala: Bwana, kwa maombezi ya Bikira Maria Mama yetu, tufundishe kuheshimu kila mtu. Amina
No comments:
Post a Comment
"Asante sana kwa maoni yako"