Friday, 30 September 2016

TAFAKARI: 30/9/2016 Ijumaa ya 26 ya Mwaka-C. " “Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4 "


IJUMAA WIKI YA 26 YA MWAKA-C
        Somo:
             Ayu 38:1, 12-21, 40:3-5
        Zab/Kit: 139:1-3, 7-8, 9-10, 13-14ab
        Injili: Lk 10:13-16

          Nukuu:
         “Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake?” Ayu 38:12
         
           “Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4
            “Ole wako Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu,” Lk 10:13
     
             “Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu,” Lk 10:15
          “Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma,” Lk 10:16

         TAFAKARI:
         “Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma."
 
              Wapendwa wana wa Mungu, katika maisha yapo “mambo fulani” na hata wakati mwingine hutokea “mambo fulani,” ambayo kwayo kwa ufahamu wa ubinadamu wetu hukoswa na majibu. Huu “ufulani wa mambo” tusioujua katika maisha, huyafanya maisha hayo kuwa fumbo.
           Fumbo siyo tatizo na lingekuwa tatizo basi lingekuwa na jibu au suluhu yake. Fumbo halina suluhu zaidi ya kulizungumzia katika maana ya kulihusisha na kile tukifahamucho ili tuzame katika undani wa fumbo hilo.
          Lengo ni kupata mwanga katika fumbo hilo. Ili kumfanya Ayubu azame ndani ya yale yaliyompata, Mungu kupitia upepo ule wa kisulisuli anamuuliza, “Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake?” Ayu 38:12.
        Msingi wa swali hili ni kumtaka Ayubu afahamu kuwa yapo mambo mengine ambayo kwayo kwa mazoea yetu twayaona ya kawaida, ila yamebeba fumbo zito kwa Yule anayeyaratibisha, yaani, Mungu mwenyewe. Katika mwendelezo huo wa maswali ya kina, Ayu 38:13-20, yanamfanya Ayubu kufunguka na kuzama zaidi katika fumbo lile la maisha yake na yote yaliyompata.
           Yote tuyapatayo katika maisha yana kusudi la umilele kwa sababu tumeumbwa tuishi milele, na hili ndilo kusudi la Mungu kwako na kwangu. “Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo, Na hesabu ya siku zako ni kubwa!” Ayu 38:21.
           ‘Ukubwa wa hesabu za siku zako’ ni umilele wa maisha yako. Baada ya kuzamishwa katika tafakari hii, na kupata mwanga wa fumbo la maisha yake, “ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4. ‘Mimi si kitu kabisa, naweka mkono wangu kinywani pangu,’ ni hali ya kujisalimisha kabisa bila kujibakiza kwa Mungu Mweza wa vyote.
          Kujisalimisha huku si kwa kijinga, bali ni kujisalimisha katika ‘ufahamu na umaana’-“rationality and significativity.” Akimaanisha ufahamu na umaana, Ayubu anasema, “nimenena mara moja, nami sitajibu; Naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi,” Ayu 40:5. Hii ni hatua kubwa na ya ukomavu katika maisha ya kiroho.
            Je, kuna uhusiano gani kati ya Imani na miujiza? Imani siyo miujiza! Ila miujiza usaidia imani changa kukua na kukomaa. Mkristo anayebaki katika hatua ya miujiza tu, huyo bado hajakomaa katika imani. Wapenda miujiza bila kukua katika imani, na wenye kuhama kutoka nyumba moja ya sala na kwenda nyumba nyingine ya sala, huku wakivutwa na ‘nani zaidi’, ni sawa na watoto wa ‘shule ya awali imani’ katika miaka yao yote. Na hili ndilo analolikemea Yesu katika Injili ya leo na kusema, “Ole wako Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu,” Lk 10:13. Miujiza ni mwito wa mabadiliko katika Imani kuelekea ukomavu, na siyo kigoto cha imani.
 
        “Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1 Watu waishio katika miji hiyo iliyotajwa na Yesu tungeweza kusema ni “watoto wazee,” katika imani. Na linganisho la ‘utoto uzee’ kiimani ni wakazi wa Tiro na Sidoni. Hawa wana hofu ya Mungu. Naye Yesu anasema, “Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi,” Lk 10:14.
          Wakazi wa mji wa Kapernaumu ni sawa na mbegu zile zilizoanguka kwenye mwamba. Hawa ni “wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga,” Lk 8:13. Katika hali hii kiimani, Yesu anasema, “Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu,” Lk 10:15.
          Kukuzwa hata mbinguni ni furaha kulipokea neno, ila wakati wa majaribu hukosa nguvu na kushuka hadi kuzimu. Pamoja na hali na mazingira haya kiunjilishaji, Yesu anakuasa wewe na mimi tusivunjike moyo katika kuitangaza habari njema ya wokovu wetu. Hapa na pale tutahuzunishwa na hata kukatishwa tamaa, ila tusife moyo kwa sababu, “awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma,” Lk 10:16. Utume si lelemama. Utume ni kuvumilia ndani na katika Kristo Yesu.

        Tumsifu Yesu Kristo!
      “Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4 

           Tusali:-
Ee Yesu, tujalie Roho ya Kimisionari tukiazia pale tulipo. Amina


Copyright © 2016 by Fr Edgar Tanga Ngowi, OSA  and published by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
        See: imani-katoliki.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

"Asante sana kwa maoni yako"

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...