Monday, 19 September 2016

TAFAKARI: Jumatatu ya 25 ya Mwaka-C.




JUMATATU WIKI YA 25 YA MWAKA-C

Somo: Mit 3:27-34
Zab/Kit: 15:2-3ab, 3cd-4ab, 5
Injili: Lk 8:16-18
             Nukuu “Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, Ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda,” Mit 3:27 “Usimwambie jirani yako, Nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa; Nawe unacho kitu kile karibu nawe,” Mit 3:28 “Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka mvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake,” Lk 8:16 “Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang'anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho,” Lk 8:18

TAFAKARI:
“Mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang'anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.”

           Wapendwa wana wa Mungu, ufahamu wa kawaida waonyesha wazi kwamba aliye tayari kushirikisha alivyo navyo kwa wengine, ikiwa ni pamoja na vipaji vyake, kwa njia hiyo uvikuza vipaja vyake na kugundua mambo mengine zaidi na yenye uhusiano na kipaji kile. Hakuna apotezaye muda wake kwa kumsaidia mwingine kufahamu jambo fulani ambalo yeye ana ufahamu nalo. Ni kadiri ufanyavyo jambo hilo mara kwa mara ndivyo unavyo lifahamu vizuri na kugundua vingine zaidi. Hivyo, karama au vipaji tulivyojaliwa na Mungu hukua na kufikia ‘ukamilifu’ wake pale tunapovitumia, na kuvishirikisha kwa wengine. Kwa maana hiyo, “Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka mvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake,” Lk 8:16. Kama kilivyo kioo waweza kuiona sura yako, ndivyo hivyo hivyo mtu mwingine ukuwezesha kujiona vizuri pale unaposhirikisha vipaji vyako na kuwa wazi kwa kile ulicho. Ni katika uelewa huu, neno hili la Yesu ubeba maana yake, yaani, “Mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang'anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho,” Lk 8:18. Na kile ulicho ni sawa na ‘kikohozi’ kiasi kwamba huwezi kukizuia ikiwa wakiishi na kukishirikisha kwa upendo. “Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kutokea wazi,” Lk 8:17. Katika kweli hii, Kristo Yesu ndiye kielelezo chetu na upendo ule wa Mungu ambao kwa wakati wake alipenda kutushirikisha, Gal 4:4-5. Upendo huo wa Mungu umewekwa wazi kwa Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Na hivi ndivyo ilivyompendeza Mungu kwamba, “jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16 Kinyume chake, yaani, “yule asiye na kitu atanyang'anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho,” Lk 8:18b, ni pale tunapoongozwa na choyo na ile roho ya ‘kwa nini.’ Kutoshirikisha vipaji na karama zako kwa wengine na kubaki nazo kwa kujiinua, huzidumaza karama na vipaji hivyo. Ni sawa na kuwa na shilingi 1000 na kuihifadhi kwenye kopo zuri la dhahabu na kuifungua kabatini. Fedha hii itabaki katika upya wake, ila kila kukichwa upungua thamani yake, na hasa pale penye mdororo wa kiuchumi. Kumbe kila mmoja wetu ni vyema akavijua vipaji na karama zake. Na karama na vijaji hivyo ujionyesha kwa huduma tuzitowazo kutokana na wito na nafasi tulizokuwa nazo katika jamii. Hivyo, “usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, Ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda,” Mit 3:27. Kufanya hivyo, yaani, kuwanyima watu mema yaliyo haki yao, hakuna tija yoyote katika ufanyizi wako na nafasi uliyo nayo, na wala hakuna tija kwa wale unaowahudumia. Kile uwezacho kufanya kwa wengine leo na sasa kadiri ya uwezo na nafasi, kisisubiri kesho. Kwa maana hiyo “usimwambie jirani yako, Nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa; Nawe unacho kitu kile karibu nawe,” Mit 3:28. Kwa kutokufanya hivi unakoswa fadhila nyingi kutoka kwa Mungu. Ni kweli kabisa pale ulipo wapo wengi wenye imani nawe, na kwa upande mwingine wanakuchukulia kama mfano wa kuigwa. Ikiwa hali ndivyo ilivyo, basi elewa huo ndio mwito sahihi wa kuishi na kila mtu bila mwelekeo wa kubaguana. Ni mwito pia wa kuchukuliana kwa upendo na upya kila siku. Si wakati wa kuhama au kutembea na kumbukumbu mbaya za watu. Hivyo “usiwaze mabaya juu ya jirani yako, Ambaye anakaa karibu nawe na kujiona salama,” Mit 3:29. Kila mmoja anaye hitaji uwepo wako mpe nafasi kadiri ya nafasi uliyonayo. Hatari katika maisha ya ‘ujirani mwema’ ni pale tunapopenda kuishi maisha linganishi na shindanishi pasipo kujua kwa nini nafanya kama ninavyofanya. Si mbaya wala vibaya kuwa na wivu wa maendeleo katika maana ya kufanya vizuri zaidi kila siku kwa kuona mfano mzuri kutoka kwa mwengine. Ila wivu huu usinipeleka katika uharibufu, yaani, kuharibu kile cha mwenzangu ili changu kionekane. Ndugu yangu, “usishindane na mtu bila sababu, Ikiwa hakukudhuru kwa lo lote,” Mit 3:30. Mara zote nijiuze hivi kabla ya kutenda lolote; Je, na fanya hivi kwa sababu gani, na ili iwe nini? Kushindana na watu pasipo lengo chanya ni sawa na kuotesha upepo na mwisho wa siku utavuna kimbunga. Hivyo “usimhusudu mtu mwenye jeuri, Wala usiichague mojawapo ya njia zake,” Mit 3:31. Ikiwa twaishi ulimwenguni hapa kama jukumu la muda mfupi, basi hatuna sababu ya kupoteza muda kwa yale yasiyotujenga mwili na roho. Je, una sababu ya kushindana na mtu jeuri na kaidi? Hapana! “Maana mtu mkaidi ni chukizo kwa Bwana, Bali siri yake ni pamoja na wanyofu,” Mit 3:32. Katika mazingira na hali hii, ni mwito kwetu pia kuishi maisha ya unyofu kwa sababu hatutopungukiwa kitu. Ikiwa amani ile tuipendayo ndani yetu na kwa wenzetu ni muhimu pale tunapoishi zaidi ya mmoja, basi tuelewe amani hiyo ni tunda la haki. Hivyo tutende haki kwa kila mtu ili tupate matunda yake, yaani, amani. Kwani “Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki,” Mit 3:33. Na maskani ya kwenye haki ujengwa na unyenyekevu. Unyenyekevu ni kukubali pia yapo mambo mengine yaliyo juu ya uwezo wangu, na kuyafahamu hayo yanipasa kujinyenyekeza. Katika lugha ya picha na yenye kueleweka vizuri kati yetu ni kwamba, Mungu “huwadharau wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema,” Mit 3:34. Ndugu yangu, kuijua siri ya Mungu na maarifa yake, yanipasa kujinyenyekeza mbele yake. 

Tumsifu Yesu Kristo! 
       “Usishindane na mtu bila sababu, Ikiwa hakukudhuru kwa lo lote,” Mit 3:30 
            Tusali:-Ee Yesu Mwema, nijalie moyo wa kujitoa bila kujibakiza kadiri ya karama na vipaji ulivyonijalia. Amina

Copy right© by Fr Edgar Tanga Ngowi, OSA.  and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
     website:
imani-katoliki.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

"Asante sana kwa maoni yako"

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...