Tuesday, 13 September 2016

TAFAKARI YA MASOMO YA MISA, 13/9/2016 Jumanne ya 24 ya Mwaka.

"HURUMA YA MUNGU NIYA MILELE".

JUMANNE WIKI YA 24 YA MWAKA-C

Somo: 1Kor 12:12-14, 27-31a

Zab/Kit: 100:1-2, 3, 4, 5

Injili: Lk 7:11-17

Nukuu

“Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo,” 1Kor 12:12

“Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja,” 1Kor 12:13

 “Takeni sana karama zilizo kuu,” 1Kor 12:31a

“Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye,” Lk 7:12

“Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie,” Lk 7:13

“Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka,” Lk 7:14

“Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake,” Lk 7:15

TAFAKARI:
“Takeni sana karama zilizo kuu.”

   Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na sheria ya Bwana, yaani Torati, leo kielelezo chetu kuufikia uzima wa milele ni Kristo Yesu kwa wote walio na ufahamu juu yake (dhamira safi na hofu ya Mungu), na kwa namna ya pekee wabatizwa wote. “Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja,” 1Kor 12:13. Ni katika kweli hii kwamba wapo wengine kwa dhamiri zao safi na hofu yao juu ya Mungu watapata wokovu.

Wapendwa katika Kristo, Mungu wetu ni Mungu wa wanadamu wote licha ya tofauti zetu za kiimani. Hakuna anayeishi katika ulimwengu huu kwa sababu yake mwenyewe, Rum 14:7. Kila mmoja wetu anayo chapa ya Mungu ndani yake, Mwa 1:27. Ulimwengu huu ukiwemo na vyote vilivyomo ni Mali yake Mungu, Zab 24:1. “Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia; kama kwa kweli Mungu ni mmoja, atakayewahesabia haki wale waliotahiriwa katika imani, nao wale wasiotahiriwa atawahesabia haki kwa njia ya imani iyo hiyo,” Rum 3:29-30. Ukweli ni kwamba kila anayeongozwa na mwenye dhamiri hai na safi ataokolewa siku ya mwisho.

Mafundisho ya Kanisa hasa tunaposoma Katekisimu ya Kanisa Katoliki, namba 847, inafundisha juu ya dhamiri hai na safi ambapo hata wale wasiomjua Kristo ndiyo ponya yao. Ukweli huu pia umefafanuliwa vizuri katika mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano, Konstitusio ya Kichungaji juu ya Kanisa katika Ulimwengu wa leo, “Gaudium Et Spesteaches,” “Furaha na Matumaini,” inaelezea ukweli huu kama ifuatavyo; “Kwa kweli ni katika fumbo la Neno aliyefanyika mwili tu kwamba fumbo la binadamu linaangazwa. Maana Adamu, mtu wa kwanza, alikuwa mfano wa yule atakayekuja, yaani Kristo Bwana. Naye Kristo, aliye Adamu mpya, akilifunua fumbo la [Mungu] Baba na la upendo wake, hudhihirisha kikamilifu kwa binadamu, binadamu alivyo, na kumjulisha wito wake mkuu. Jambo hilo haliwahusu wakristo tu bali pia wanadamu wote wenye mapenzi mema, ambao neema ya Mungu hufanya kazi mioyoni mwao, kwa namna isiyoonekana. Maana Kristo alikufa kwa ajili ya watu wote na wito halisi wa binadamu ndio mmoja, ule wa kimungu. Kwa hiyo lazima tuwe na wazo kwamba Roho Mtakatifu anawajalia watu wote uwezekano wa kushiriki fumbo la kipasaka, kwa jinsi anayoijua Mungu,” (no. 22)

 Somo letu la leo Mtume Paulo anaongelea vizuri sana kuhusu Kristo kama Kanisa nasi tukiwa viungo vyake. Ni kwa Sakramenti ya ubatizo tunafanywa wana wa Mungu na warithi wa ufalme wake. Lakini tunaishi na kupata uhai tukiunganika na Kristo kama viungo vya huo mwili yaani Kanisa. “Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo,” 1Kor 12:12. Kanisa kwa mtazamo huu, ni mwili wa Kristo, yaani wabatizwa wote, na Sakramenti ya wokovu wetu. Basi tukiwa viungo vya Kristo vyenye kujenga mwili wa Kristo ambao ni Kanisa, kila kiungo kina kazi yake na kwa kutimiza kazi yake ndiyo afya ya mwili mzima.“Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi,” 1Kor 12:14.

Hivyo kila mmoja wetu, yaani mbatizwa ana umuhimu wake wa pekee kuujenga mwili huu, yaani Kanisa, na kufanya vizuri. “Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake,” 1Kor 12:27. Umoja katika utofauti wetu ndio uzuri wa mwili huu wa Kristo yaani Kanisa. Karama zetu mbalimbali ni kwa ajili ya Kanisa na kufaidiana. Hivyo, “Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha,” 1Kor 12:28. Utofauti huo katika huduma na karama ni kwa ajili ya Kanisa zima la wana wa Mungu. Sote kwa pamoja twaufanya mwili huu, yaani Kanisa kuwa hai.

Wapendwa katika Kristo, ni vyema ukajua karama zako na huduma yako katika Kanisa. Si vizuri kupoteza muda wako kwa kuishi maisha linganishi, yaani, maisha ya mfanano na mwingine, bila kuvitambua vipaji vyako ambavyo ndiyo njia bora ya kutumika katika mwili huu, yaani Kanisa. Na kuvijua vipaji na karama zako ni kutokukata tamaa pale unaposhindwa kufikia lengo lako kusudiwa maisha au huduma unayoitoa. Wote hatuwezi fanana. “Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?” 1Kor 12:29-30. HAPANA! Kila mmoja wetu anakarama yake ambayo Mungu anapenda uitumie hiyo kuudhihirisha Utukufu wake na Furaha yake.

Wapendwa wana wa Mungu, ukweli ni kwamba kila jambo lina kusudi lake, hivyo litazame jambo hilo kwa jicho la imani, na wala usiruhusu manung’uniko na kujihukumu pale mambo yanapokwenda ndivyo sivyo. Tazama mara zote tumaini lile lililopo mbele yako. Mfano wa mtu  aliyetazama tumaini lililopo mbele ya maisha yake ni Mama yule wa mji wa Naini kadiri ya Injili ya leo, na aliyefiwa na mwanaye wa pekee, Lk 7:11-12. Mama huyu na tukio lake hili kiimani linatufundisha kuishi kwa tumaini pale tunapokumbana na sintofahamu katika maisha.

Injili ya leo inatupa simulizi hili kwa namna ya pekee. Yesu Kristo katika safari zake za kuihubiri habari njema ya wokovu akiwa na wanafunzi wake, wanakutana na msafara uliobeba maiti ya mwana pekee wa mama mjane. “Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye,” Lk 7:12. Bila shaka msafara ule wa maiti ile na hali za watu kama zilivyokuwa kwa kusikitika juu ya msiba ule, na hasa mama huyu ambaye anaonekama kuwa mwema kwa jirani zake, unamsikitikisha Yesu pia.“Bwana alipomwona (mama mfiwa) alimwonea huruma, akamwambia, Usilie,” Lk 7:13.

Neno ‘usilie’ katika mazingira haya limebeba ujumbe, ‘ondoa hofu na uwe na matumaini.’ Tumaini lenyewe hapa na katika uhasilia wake ni Kristo Yesu mwenyewe. Kwa upendo wa ajabu na huruma ya Kimungu, ambaye kwa sasa ni Mungu na mwanadamu, Yesu “Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka,” Lk 7:14. Baada ya tukio hili la pekee kabisa na ajabu,“Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake,” Lk 7:15. Bila shaka mimi na wewe tungekuwa katika msafara huo tungetimua mbia kwa hofu!

Pamoja na hofu waliokuwa nayo watu wale katika msafara ule, walibaki na tumaini kubwa mbele yao. “Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake,” Lk 7:16. Hili ni fundisho kwetu pia. Twapaswa daima kumshukuru Mungu na kuliweka tumaini kwake tu aliyetutendea mambo ya ajabu, badala ya kujitafutia utukufu binafsi, na hata kutaka kuabudiwa. Pili, tuwe vyombo vya kusambaza habari njema kwa wengine, badala ya chuki. “Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando,” Lk 7:17. Je, ndugu yangu, hapo ulipo watumika kama chombo cha habari njema ya wokovu, au ndiyo upande wa pili, yaani, mzalisha chuki?

Tumsifu Yesu Kristo!
🙏🏿 🙏🏿
“Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie,” Lk 7:13

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie Neema na Baraka ili tudumu katika tumaini lako. Amina

No comments:

Post a Comment

"Asante sana kwa maoni yako"

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...