Friday, 23 September 2016
TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 25 YA MWAKA-C, “Kwa kila jambo kuna majira yake.”
IJUMAA WIKI YA 25 YA MWAKA-C
Somo:
Mhu 3:1-11
Zab/Kit: 144:1a, 2abc, 3.4
Injili: Lk 9:18-22
Nukuu:
“Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu,” Mhu 3:1
“Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo?” Mhu 3:9
“Nimeiona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake,” Mhu 3:10
“Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho," Mhu 3:11
“Akawaambia, Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu,” Lk 9:20
TAFAKARI:
“Kwa kila jambo kuna majira yake.”
Wapendwa wana wa Mungu, ikiwa kitabia na kimakuzi ni tokeo la historia yako na jamii iliyomzunguka, basi kile tulicho leo, yaani, kimwili na kiroho kimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na historia yako na jamii hiyo iliyokuzunguka. Leo katika taifa letu tunapambana na rushwa na ufisadi uliotukuka. Hali na mazingira haya yanataka kuibadilisha ovu hilo kuwa sifa. Ni jambo la kushangaza sana unapoona jamii kutokushtushwa na ubadirifu mkubwa wa mali ya umma. Badala yake tukio kubwa liwe ni rushwa au ufisadi linaongelewa kiushabiki ilhali tendo hilo linaangamiza taifa wakiwemo na hao ‘malimbukeni’ katika ubora wao wa kiushabiki. Ni wazi kabisa tunapoona idadi kubwa ya wale waliopewa dhamana na umma kuwa viongozi na kwa idadi yao ndio wala rushwa na mafisadi wakubwa, ni wazi jamii tunayoishi imeoza. Viongozi hao, au wala rushwa hawa na mafisadi ni tunda la jumuiya husika. Na tunapokwenda kwenye jumuiya au jamii husika tunagundua kwamba jamii hiyo imejengwa katika misingi ya kifamilia. Hivyo familia kama shule ya kwanza katika makuzi na malezi ya kila mmoja wetu kimwili na kiroho, nayo imeoza. Baadhi ya familia hujeuka na kuwa kichaka cha mafisadi na wala rushwa. Hivi unawezaje kwa mfano kuhafikiana na hali ambayo mzazi anakuwa mpiganaji namba moja kupita njia za panya ili mtoto wake afanikiwe? Je, huyu ambaye amepita njia za panya hadi kufikia nafasi hiyo ya juu katika jamii aweza kuwa mtu wa haki na kweli? Leo yale yote tunayotaabika nayo wakati fulani watu fulani na jamii fulani haikuenenda katika haki na kweli. Kwani “kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu,” Mhu 3:1. Hakika kwa yale yasiyo haki na kweli ni kinyume na makusudi ya kuumbwa kweli, na mwisho wa siku hatuta faidika na chochote. Jambo lolote lile lisilo akisi umilele wake ni sawa na kupanda upepo na mwisho wa siku jiandae kuvuna kimbunga. “Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo?” Mhu 3:9. Na mbaya zaidi kama hayo anayojishughulisha nayo hayana chembe ya umilele. Ndugu yangu, ingawa tupo hapa duniani kwa muda mfupi sana, kila jambo lina wakati wake, Mhu 3:2-8. Pamoja na ukweli huo, Je! watumiaje muda huu mfupi hapa duniani? Au umeamua kuishi kama inzi ambaye umri wake ni siku saba tu, na hupenda kutua kila mahali bila kujali kwamba anahatarisha maisha yake? Hakika Mungu husikitishwa sana pale anapoona unaishi nje ya makusudi yake, yaani, amekuumba ili uishi milele. Naye Mhubiri katika hili anasema, “nimeiona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake,” Mhu 3:10. Na taabu hii si kitu kingine zaidi ya uhuru ule Mungu aliotupatia. Ni katika uhuru huu tunaweza kumwazi Mungu au kujisalimisha kwake katika toba ya kweli na majuto. Katika mpango wake Mungu tangu kuumbwa ulimwengu, “kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho,” Mhu 3:11. Ni katika kweli hii tunaona kwamba uumbaji wa ulimwengu huu kwa kiasi kikubwa umemlenga mwanadamu na wokovu wake. Je, tunadhamisha kweli hii kwa kuulinda ulimwengu huu ili kuwa sehemu salama zaidi ya kuishi? Leo tunaona ni kwa namna gani binadamu huu alivyo kuwa “Mr. Kipepe,” anavyo kata tawi lile alilokalia. Hata hivyo mimi na wewe leo yanipasa kumjua huyu Yesu ni nani kwangu. Kwa upande wake Yesu, kama kiongozi na mwenye kujali na kuwajibika, alitaka kujua kutoka kwa watu na hata kwa wanafunzi wake wa karibu kabisa wanamtazamo gani juu yake. Mtume Petro anatoa jibu sahihi kuhusu Yesu, na lile lililo mpasa Kristo katika ulimwengu huu. “Akawaambia, Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu,” Lk 9:20. Mpendwa unayesafiri nami katika tafakari hii nikuulize swali la msingi; pamoja na majibu ya wengine, na hasa jibu alilolitoa Petro kuhusu swali alilouliza Yesu, wewe binafsi Yesu kwako ni nani? Jibu la Petro kwa tafasiri, Kristo, yaani ‘Masiha wa Mungu,’ ndiye yeye tu aliyewekwa katika mpango mzima wa ukombozi wa mwanadamu. Hivyo tutaiona mbingu na kuufurahia uhuru wa kweli endapo tu tutakuwa tayari kushikamana na mwana huyu wa Mungu. “Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina lingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:11-12. Hivyo kufikia hatua hii la kuokolewa kwetu kupitia jina hili hatunabudi kushiriki njia ile aliyopitia Bwana wetu Yesu Kristo kama anavyowanong’onozea wanafunzi wake siri hii na kusema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka,” Lk 9:22. Ndugu yangu hakuna PASAKA PASIPO IJUMAA KUU. Ndivyo hivyo kwetu kama wafuasi wake Kristo tulio hai kwamba hakuna UTUKUFU PASIPO MSALABA. Leo wapo watu kati yetu wamejawa hofu na hawapendi kukosolewa hata kuzungumziwa, ili hali Yesu aliye Mungu na Mwanadamu aliruhusu watu wasema kile waonacho kuhusu Yeye. Uhuru huu wa kukosolewa ni uthibitisho wa kiongozi asiyekuwa na mawaa wala makandokando. Tumsifu Yesu Kristo! “Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu,” Lk 9:20 Tusali:-Ee Yesu, kwa maisha yako hapa duniani, yatakase pia maisha yetu ili tuifuate njia yako kikamilifu. Amina
Copyright © by Fr Edgar Tanga Ngowi,OSA. and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
website:
imani-katoliki.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.
Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita ...
-
Katika kuhakikisha kwamba uinjili shaji unakua tumekuletea nata zanyimbo za kikatoliki hizihapa Bofya hapa ...
-
Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita ...
-
Dominika ya 28 ya Mwaka SOMO LA 1 2 Fal 5:14-17 Naamani alishuka, akajichovya mara saba katika Y...
-
Dominika ya 30 ya Mwaka SOMO LA 1 Ybs 35:12-14,16-19 Kwa kuwa Bwana ndiye mhukumu wala hakijali cheo cha mtu. Hatamkubali ye yote juu...
-
Dominika 29 ya Mwaka SOMO LA 1 Kut 17:8-13 Wakati huo Waamaleki wakatokea, wakapigana na Israeli huko Ref...
No comments:
Post a Comment
"Asante sana kwa maoni yako"