Friday, 30 September 2016

TAFAKARI: 30/9/2016 Ijumaa ya 26 ya Mwaka-C. " “Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4 "


IJUMAA WIKI YA 26 YA MWAKA-C
        Somo:
             Ayu 38:1, 12-21, 40:3-5
        Zab/Kit: 139:1-3, 7-8, 9-10, 13-14ab
        Injili: Lk 10:13-16

          Nukuu:
         “Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake?” Ayu 38:12
         
           “Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4
            “Ole wako Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu,” Lk 10:13
     
             “Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu,” Lk 10:15
          “Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma,” Lk 10:16

         TAFAKARI:
         “Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma."
 
              Wapendwa wana wa Mungu, katika maisha yapo “mambo fulani” na hata wakati mwingine hutokea “mambo fulani,” ambayo kwayo kwa ufahamu wa ubinadamu wetu hukoswa na majibu. Huu “ufulani wa mambo” tusioujua katika maisha, huyafanya maisha hayo kuwa fumbo.
           Fumbo siyo tatizo na lingekuwa tatizo basi lingekuwa na jibu au suluhu yake. Fumbo halina suluhu zaidi ya kulizungumzia katika maana ya kulihusisha na kile tukifahamucho ili tuzame katika undani wa fumbo hilo.
          Lengo ni kupata mwanga katika fumbo hilo. Ili kumfanya Ayubu azame ndani ya yale yaliyompata, Mungu kupitia upepo ule wa kisulisuli anamuuliza, “Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake?” Ayu 38:12.
        Msingi wa swali hili ni kumtaka Ayubu afahamu kuwa yapo mambo mengine ambayo kwayo kwa mazoea yetu twayaona ya kawaida, ila yamebeba fumbo zito kwa Yule anayeyaratibisha, yaani, Mungu mwenyewe. Katika mwendelezo huo wa maswali ya kina, Ayu 38:13-20, yanamfanya Ayubu kufunguka na kuzama zaidi katika fumbo lile la maisha yake na yote yaliyompata.
           Yote tuyapatayo katika maisha yana kusudi la umilele kwa sababu tumeumbwa tuishi milele, na hili ndilo kusudi la Mungu kwako na kwangu. “Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo, Na hesabu ya siku zako ni kubwa!” Ayu 38:21.
           ‘Ukubwa wa hesabu za siku zako’ ni umilele wa maisha yako. Baada ya kuzamishwa katika tafakari hii, na kupata mwanga wa fumbo la maisha yake, “ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4. ‘Mimi si kitu kabisa, naweka mkono wangu kinywani pangu,’ ni hali ya kujisalimisha kabisa bila kujibakiza kwa Mungu Mweza wa vyote.
          Kujisalimisha huku si kwa kijinga, bali ni kujisalimisha katika ‘ufahamu na umaana’-“rationality and significativity.” Akimaanisha ufahamu na umaana, Ayubu anasema, “nimenena mara moja, nami sitajibu; Naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi,” Ayu 40:5. Hii ni hatua kubwa na ya ukomavu katika maisha ya kiroho.
            Je, kuna uhusiano gani kati ya Imani na miujiza? Imani siyo miujiza! Ila miujiza usaidia imani changa kukua na kukomaa. Mkristo anayebaki katika hatua ya miujiza tu, huyo bado hajakomaa katika imani. Wapenda miujiza bila kukua katika imani, na wenye kuhama kutoka nyumba moja ya sala na kwenda nyumba nyingine ya sala, huku wakivutwa na ‘nani zaidi’, ni sawa na watoto wa ‘shule ya awali imani’ katika miaka yao yote. Na hili ndilo analolikemea Yesu katika Injili ya leo na kusema, “Ole wako Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu,” Lk 10:13. Miujiza ni mwito wa mabadiliko katika Imani kuelekea ukomavu, na siyo kigoto cha imani.
 
        “Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1 Watu waishio katika miji hiyo iliyotajwa na Yesu tungeweza kusema ni “watoto wazee,” katika imani. Na linganisho la ‘utoto uzee’ kiimani ni wakazi wa Tiro na Sidoni. Hawa wana hofu ya Mungu. Naye Yesu anasema, “Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi,” Lk 10:14.
          Wakazi wa mji wa Kapernaumu ni sawa na mbegu zile zilizoanguka kwenye mwamba. Hawa ni “wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga,” Lk 8:13. Katika hali hii kiimani, Yesu anasema, “Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu,” Lk 10:15.
          Kukuzwa hata mbinguni ni furaha kulipokea neno, ila wakati wa majaribu hukosa nguvu na kushuka hadi kuzimu. Pamoja na hali na mazingira haya kiunjilishaji, Yesu anakuasa wewe na mimi tusivunjike moyo katika kuitangaza habari njema ya wokovu wetu. Hapa na pale tutahuzunishwa na hata kukatishwa tamaa, ila tusife moyo kwa sababu, “awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma,” Lk 10:16. Utume si lelemama. Utume ni kuvumilia ndani na katika Kristo Yesu.

        Tumsifu Yesu Kristo!
      “Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4 

           Tusali:-
Ee Yesu, tujalie Roho ya Kimisionari tukiazia pale tulipo. Amina


Copyright © 2016 by Fr Edgar Tanga Ngowi, OSA  and published by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
        See: imani-katoliki.blogspot.com

MASOMO YA MISA, 30/9/2016 Ijumaa ya 26 ya Mwaka. "      ( Yn. 14:5) Bwana anasema: mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi."


SOMO LA 1
   Ayu. 38:1, 12 – 21, 40:3 – 5

       Ndipo Bwana alimjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake? Yapate kuishika miisho ya nchi, waovu wakung’utwe wakawe mbali nayo? Hubadilika mfano wa udongo chini ya muhuri, vitu vyote vinatokea kama mavazi. Na waovu nuru yao huzuiliwa isiwafikie, na mkono ulioinuka huvunjika. Je! Umeziingia chemchemi za bahari, au umetembea mahali pa siri pa vilindi? Je! Umeziingia chemchemi za bahari, au umetembea mahali pa siri pa vilindi? Umeyafahamu mapana ya dunia? Haya! Sema, ikiwa unayajua hayo yote. Iko wapo njia ya kuyafikia mako ya nuru? Na giza pia, mahali pake ni wapi? Upate kuipeleka hata mpaka wake, upate kuelewa na mapito ya kuiendea nyumba yake? Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo, na hesabu ya siku za ni kubwa! Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu. Nimenena mara moja, nami sitajibu; naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi.

      WIMBO WA KATIKATI
   Zab. 139:1 – 3, 7 – 10, 13 – 14

        (1).   Ee Bwana umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu: Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote.
                 (K) Uniongoze Bwana, katika njia ya milele.
       (2).  Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.
                 (K) Uniongoze Bwana, katika njia ya milele.
      (3).  Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika.
                (K) Uniongoze Bwana, katika njia ya milele.
      (4).    Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu. Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.
              (K) Uniongoze Bwana, katika njia ya milele.

           SHANGILIO
      Yn. 14:5

                     Aleluya, aleluya, Bwana anasema: mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Aleluya.

        SOMO LA INJILI
            Lk. 10:13 – 16

             Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu. Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu. Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.


Copyright © 2016 by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
      see: imani-katoliki.blogspot.com

Thursday, 29 September 2016

TAFAKARI: 29/9/2016 Juma la 26 la Mwaka-C " JESHI LA MBINGUNI! "



TAFAKARI

      Alhamisi, Septemba 29, 2016. Juma la 26 la Mwaka

       Sikukuu ya Watakatifu Malaika Wakuu, MIKAEL, GABRIELI NA RAFAELI 

    
          Dan 7: 9-10, 13-14 au
        Ufu 12: 7-12
   Zab 137: 1-5
               Yn 1: 47-51

          JESHI LA MBINGUNI!
           Leo tuna adhimisha sikukuu ya Malaika wakuu watatu ambao majina yao yanatajwa katika maandiko: Mikaeli, Gabriel na Rafaeli. Hawa malaika wanaitwa “Malaika Wakuu” maana yake ni wakuu kwasababu wana utume maalumu waliopewa na Mungu. Sikukuu hii ya malaika inatukumbusha kwamba vitu vinavyo onekana na kushikika ni sehemu ndogo sana ya ukweli halisi na hatuwezi kujifanya kujua kila kitu. Siku hizi tunaweza tusitembelewe na malaika kama alivyomtembelea Bikira Maria wakati wakutangazwa kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo au kipindi cha kutangaza ufufuko wa Yesu, lakini Mungu anaendelea kuwasiliana nasi kwa namna ya pekee. Swali ni kwamba, mimi nipo wazi kiasi ghani Mungu anapotaka kuongea nami?
   
       Sala: Baba wa Mbinguni, umetupa malaika wakuu ili kutusaidia sisi wahujaji hapa duniani. Mtakatifu Malaika Mikaeli ni kinga yetu, namuomba aje kunisaidia, awapiganie wapendwa wangu wote, na atukinge na hatari. Mtakatifu Malaika Gabrieli ni mjumbe wa habari njema, namuomba anisaidie kusikia sauti yako na anifundishe ukweli. Mtakatifu Malaika Rafaeli ni malaika anaye ponya, ninamuomba anipe uponyaji wa yale yote ninayohitaji kuponywa na ya kila mmoja ninaye mfahamu, nyanyua juu katika kiti chako cha neema na utupe tena zawadi yako ya kupona na kuwa huru. Tusaidie Bwana tuweze kutambua kwa ukamilifu kabisa, ukweli wa Malaika Wakuu na hamu yao yakutaka kututumikia. Malaika Watakatifu, Mtuombee. Amina.

Copyright © 2016 by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG

MASOMO YA MISA, 29/9/2016 " Zab. 105:3 Aleluya, aleluya, Mhimidini Bwana, enyi majeshi yake yote, ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake. Aleluya."


SIKUKUU YA WATAKATIFU MIKAELI, GABRIELI NA RAFAELI, MALAIKA WAKUU  

      SOMO LA 1
      Dan. 7:9-10,13-14

                Nilitazama viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake, maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa. Nikaona katika njozi za usiku, na tazama mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.

       WIMBO WA KATIKATI
         Zab. 138:1-5

         (1).  Nitakushukuru kwa moyo wangu wote, Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi. Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu.
                 (K) Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
         (2).    Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako, Kwa maana umeikuza ahadi yako, Kuliko jina lako lote. Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.
                  (K) Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
         (3).   Ee Bwana, wafalme wote wa dunia watakushukuru, Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako. Naam, wataziimba njia za Bwana, Kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu
                  (K) Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.

         SHANGILIO
     Zab. 105:3

                     Aleluya, aleluya, Mhimidini Bwana, enyi majeshi yake yote, ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake. Aleluya.

           SOMO LA INJILI
          Yn. 1:47-51
        
     Yesu alipomwona Nathanaeli anakuja kwake akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwa chini ya mtini nilikuona. Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli. Yesu akajibu, akamwambia, kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya. Akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.

Copyright 2016 by shajara and published by  MAMBO YAHUSUYO  IMANI BLOG 

Wednesday, 28 September 2016

TAFAKARI: Jumatano ya 26 ya Mwaka-C. " GHARAMA YA KUWA MFUASI WA KWELI WA KRISTO! "



Jumatano, Septemba 28, 2016.
Juma la 26 la Mwaka

         Ayu 9: 1-12, 14-16
Zab 87: 10-15
Lk 9: 57-62

         GHARAMA YA KUWA MFUASI WA KWELI WA KRISTO!
         Tunaishi katika ulimwengu ambao gharama za maisha zinapanda kadiri ya mahitaji yanavyopanda. Na wakati mwingine kadiri gharama inavyopanda ndivyo tunavyo hitaji zaidi. Kuna gharama ya kumfuata Kristo pia! Katika Injili, watu watatu wanakuja kwa Yesu na wanataka kumfuata. Lakini Yesu alivyo ongea kuhusu gharama ya kumfuata hawakuwa tayari kuilipa.
   Walitaka kuwa na Yesu lakini katika hali yao wenyewe. Hawakuwa tayari kuachia mambo yao, tamaa zao, mipango yao n.k, kwa ajili ya Kristo. Haishangazi kwamba Yesu alisema njia ya kwenda kwenye uzima wa milele ni nyembamba na ni wachache watakao ipata.
      Ayubu ni mtu ambaye anajulikana kwetu kama mtumishi mwaminifu wa Mungu. Alikuwa mzuri kwa wengine na alibarikiwa na mengi, alikuwa na familia, afya njema, na kwa wakati, utajiri mwingi. Alikuwa na mitizamo na ndoto za maisha. Lakini yote yalibadilika na Ayubu akapoteza kila kitu. Somo la kwanza la leo, linamuonesha Ayubu baada ya kuteseka kwa mateso ya kupoteza yote, na pia mtazamo wa Ayubu juu ya Mungu unabadilika vile vile. Mwanzoni alionekana kuwa na uchungu. Lakini mwishoni Ayubu alichagua kujitegemeza kwa Bwana. Kwa kuangalia mfano huu, tunaweza kuona ni kwanini tunaambiwa tutoke katika njia zetu ili Bwana aingie afanye kazi yake. Kufanya yote haya yanahitaji kujikabidhi kweli kwa Mungu, dunia inaweza isikuelewe na hata marafiki wanaweza wasikuelewe na hata kukutenga, kwasababu wakati mwingine inakupasa kufanya kinyume na mtazamo wa dunia inavyodhani. Je, upo tayari kulipa gharama ili uwe mfuasi wa kweli wa Kristo?
      Sala: Chukua Ee Bwana, na pokea uhuru wangu wote, kumbukumbu zangu, uelewa wangu, na mapenzi yangu.
  Vyote jinsi nilivyo na yote niliyonayo umenipa. Nipe tu upendo na neema yako-kwa haya nitakuwa tajiri kabisa na sitatamani kingine zaidi. Amina.
      (Sala ya Mt. Inyasi wa Loyola)

Copyright © 2016 by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG 

MASOMO YA MISA, 28/9/2016 Jumatano ya 26 ya Mwaka. " Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. "


       MASOMO YA MISA JUMATANO,
SEPTEMBA 28, 2016 JUMA LA 26 LA MWAKA

     SOMO 1
      Ayu. 9:1 – 12, 14 – 16
            Ndipo Ayubu akajibu
, na kusema, kweli najua kuwa ndiyvo hivyo; lakini mtu huwaje mwenye haki mbele za Mungu? Kama akipenda kushindana naye, hawezi kumjibu neno moja katika elfu. Yeye ni mwenye hekima moyoni, na mwenye uwezo katika nguvu; ni nani aliyejifanya kuwa mgumu juu yanke, naye akafanikiwa? Aiondoaye dunia itoke mahali pake,na nguzo zake kutetema. Aliamuruye jua, nalo halichomozi; nazo nyota huzipiga muhuri. Ambaye peke yake ni mwenye kuzitandika mbingu. Na kuyakanyaga mawimbi ya bahari. Yeye afanyaye hizo nyota za Dubu, na Orioni, na hivyo kilima, na makundi ya nyota ya kusini. Atendaye mambo makuu yasiyotafutikana; naam, mambo ya ajabu yasiyohesabika. Tazama, yuaenenda karibu nami, nisimwone; tena yuapita kwenda mbele, nisitambue. Tazama, yuakamata, ni nani awezaye kumzuia? Ni nani awezaye kumwuliza, Wafanya nini? Je! Siuze mimi nitamjibuje, na kuyachagua maneno yangu kuhojiana naye? Ambaye, nijapokuwa mimi ni mwenye haki, nisingemjibu; nisingemsihi-sihi mtesi wangu. Kama ningemwita, naye akaniitikia hata hivyo nisingeamini kuwa ameisikia sauti yangu.
       Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

       WIMBO WA KATIKATI
    Zab. 88:9 – 14 (K) 2

                  (K) Maombi yangu yafike mbele zako, Ee Bwana.
         (1).   Bwana, nimekuita kila siku, Nimekunyoshea Wewe mikono yangu. Wafu je! Utawafanyia miujiza? Au waliofariki watasimama na kukuhimidi? (K)
          (2).    Fadhili zako zitasimuliwa kaburini? Au uaminifu wako katika uharibufu? Miujiza yako itajulikana gizani? Au haki yako katika nchi ya usahaulifu? (K)
          (3).      Lakini mimi nimekulilia Wewe, Bwana, Na asubuhi maombi yangu yatakuwasilia. Bwana, kwa nini kuitupa nafsi yangu, Na kunificha uso wako? (K)

       SHANGILIO
        Mt. 4:4

      Aleluya, aleluya, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Aleluya.

        INJILI
       Lk. 9:57-62

           Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda njiani, mtu mmoja alimwambia, Nitakufuata kokote utakakokwenda. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake. Akamwambia mwingine, Nifuate. Akasema, Bwana, nipe ruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu. Akamwambia, Waache wafu wawazike wafu; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu. Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusu kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.
         Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo

Copyright © 2016 by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG 

Tuesday, 27 September 2016

TAFAKARI: Jumanne wiki ya 26 ya Mwaka


JUMANNE WIKI YA 26 YA MWAKA-C

   Somo: 
   Ayu 3:1-3, 11-17, 20-23
    Zab/Kit: 88:2-3, 4-5, 6, 7-8
           Injili: Lk 9:51-56

      Nukuu: 
       “Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu,” Lk 9:53
       “Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?” Lk 9:54
            “Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]” Lk 9:55
             “Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa,” Lk 9:56a
              “Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake,” Ayu 3:1

         
            TAFAKARI:
             “Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.”
             Wapendwa wana wa Mungu, sehemu hii ya Injili n asomo letu la leo juu ya habari ile ya Ayubu, inafua ‘kweli ya Mungu’ ambayo hubaki kuwa ‘siri’ katika maisha yetu ya kila siku. Ni kweli kabisa katika hali na mazingira ambayo twateseka tu bila sababu ya teso hilo, maisha upoteza maana yake. Hii ndiyo hali aliyokuwa nayo Ayubu baada ya kupatwa na janga lile la majaribu na kuanza kulaani, Ayu 3:1.

         Kulaani kwa kile usichokijua vizuri hakutakufanya kuelewa fumbo la kile usichokijua vizuri. Kuzama katika fumbo usilolielewa ili upate maana yake ni kujiuliza swali hili; Je, katika jambo hili, Mungu wataka kunifundisha nini? Hakuna jaribu lisilo kuwa na mlango wa kutokea, 1Kor 10:13.
          Kuupata mlango wa kutokea ni kuachana na laana na laumu. Yesu Kristo aliye Mungu na Mwanadamu anaelekea Yerusalemu kwa kile kinachosimuliwa na Mwinjili Luka kama “siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia.” Je, kupaa bila kupitia mateso, kifo, na ufufuko? Mwinjili Luka halisemi jambo hili kwa kukosea. La! Hasha. Kupaa kwa Yesu ni hitimisho linalo elezea Wokovu ikiwa ndiyo lengo lengwa katika historia nzima ya mwanadamu (Yoh 1:14, Gal 4:4-5).
       
           Wokovu huo unathibishwa kwa Ufufuko wake Kristo Yesu. Ufukuko huo ni alama ya wazi ya ushinda dhidi ya kifo kilichokuwa adui yetu mkubwa. Na Kifo hicho cha Kristo Yesu ni alama wazi ya upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu kutuweka huru kutoka utumwa wa dhambi. Kwa maana nyingine, kupaa kwa Kristo kusingekuwa na maana kama kusingesema chochote kuhusu wokovu, ufufuko, na kifo. Na kuelekea Yerusalema katika maana ya “kukaza uso wake kwenda Yerusalemu,” kulimaanisha, mateso, kifo, wokovu, ufufuko, na kupaa. Hata pamoja na mpango huu mahususi uliobeba kilele cha historia mzima ya wokovu wa mwanadamu, jambo hili kwa ajabu kubwa na mshangao halimgusi mwanadamu. Hii ndiyo kweli ya Mungu inayobaki kuwa siri katika maisha ya mwanadamu. Na hii ndiyo maana ya maneno haya; “Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu,” Lk 9:53.
           
            Mwenye kufikiriwa kuhusu kesho na hatma yake itakuaje hana habari kabisa na kile anachofanyiwa. Kwa bahati nzuri au mbaya siri hii haikufichwa kabisa kwa baadhi ya wateule wa Mungu. Mwanga wa siri hii unafunuliwa kwa wanafunzi wake Yesu, kama asemavyo mwenyewe kwamba, “Ninyi mmepewa kuzijua siri za ufalme wa Mungu; bali wengine kwa mifano, ili wakiona wasione, na wakisikia wasielewe,” Lk 8:10.
           Kufunuliwa kwa siri hii kuna kuwa bahati mbaya kwa namna wanafunzi wake Yesu wanavyotafuta suluhu ya mambo hasa katika safari hii ya kuelekea Yerusalemu alipoyakazia macho yake Yesu. Na mambo yalikuwa hivi; “Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?” Lk 9:54. Yesu hakuja kufanya mwendelezo wa sheria ile ya jino kwa jino, bali kuitakatifuza na kuifanya kamili, Mt 5:17. Na lengo na uwepo wake Yesu siyo kuukumu ulimwengu bali ulimwengu uukolewe na yeye, Yoh 3:17. Ni wazi kabisa kwa kile walichoshupalia wanafunzi wake Yesu, Yakobo na Yohana cha onyesha kile kilicho ndani ya mioyo yao na ubinadamu wao. Na hapa ndipo Yesu “Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]” Lk 9:55. Yesu anawakanya wao na sisi leo kama Wakristo na Wafuasi wake kwamba mtindo wa jino kwa jino siyo staha na maadili yetu kama Wakristo. Kufanya hivyo ni kutokujua fumbo zima la wokovu wetu. Ukweli ni kwamba, “Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa,” Lk 9:56a.
         
          Tumsifu Yesu Kristo!
          “Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa,” Lk 9:56a Tusali:-Ee Yesu, tuondolee ile roho ya kukata tamaa na kuwa watu wa visasi. Amina

Copyright © 2016 by Fr Edgar Tanga Ngowi.OSA  and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
      see: imani-katoliki.blogspot.com

MASOMO YA MISA, 27/9/2016 Jumanne ya 26 ya Mwaka. "Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. "


Jumanne ya 26 ya Mwaka 

SOMO LA 1
Ayu 3:1-3, 11-17, 20-23

              Ayubu alifunua kinywa chake, na kuilaani siku yake. Ayubu akajibu, na kusema; Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba. Mbona si kufa mimi tokea mimbani? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni? Mbona hayo magoti kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya? Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika; Pamoja na wafalme na washauri wa dunia, Hao waliojijengea maganjoni; Au pamoja na wakuu wenye dhahabu, Waliozijaza fedha nyumba zao; Au, kama kuzikwa mimba iliyoharibika, nisingekuwako; Kama wachanga wasiouona mwanga kabisa. Huko waovu huacha kusumbua; Huko nako hao waliochoka wapumzika Mbona yeye aliye mashakani kupewa mwanga, Na hao wenye uchungu rohoni kupewa uhai; Ambao wangojea mauti, lakini hawayapati; Na kuyachimbulia zaidi ya kutafuta hazina iliyostirika; Ambao wafurahi mno, Na kushangilia watakapoliona kaburi? Kwa nini mtu aliyezibiwa njia kupewa mwanga, Ambaye Mungu amemzingira kwa ukingo?

     WIMBO WA KATIKATI
      Zab 88:1-7

       (1).    Ee Bwana, Mungu wa wokovu wangu Mchana na usiku nimelia mbele zako. Maombi yangu yafike mbele zako, Uutegee ukelele wangu sikio lako.
                 (K) Maombi yangu yafike mbele zako, Ee Bwana.
       (2).  Maana nafsi yangu imeshiba taabu, Na uhai wangu umekaribia kuzimu. Nimehesabiwa pamoja nao washukao shimoni; Nimekuwa kama mtu asiye na msaada.
                  (K) Maombi yangu yafike mbele zako, Ee Bwana.
        (3).    Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono wako.
                  (K) Maombi yangu yafike mbele zako, Ee Bwana.
        (4).    Mimi umenilaza katika shimo la chini, Katika mahali penye giza vilindini. Ghadhabu yako imenilemea, Umenitesa kwa mawimbi yako yote.
                   (K) Maombi yangu yafike mbele zako, Ee Bwana.

        SHANGILIO
       Mk 10:45

                    Aleluya, aleluya Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi. Aleluya

       SOMO LA INJILI
        Lk 9:51-56
           
Ilikuwa , siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu; akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali. Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu. Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]? Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.] Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine.

Copyright © 2016 by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG 

Monday, 26 September 2016

TAFAKARI: Jumatatu, Septemba 26, 2016. Juma la 26 la Mwaka. " KUJITEGEMEZA KWA MUNGU BABA YETU! "


TAFAKARI
Jumatatu, Septemba 26, 2016.
Juma la 26 la Mwaka

       Ayu 1:6-22
Zab 17:1-3.6-7
Lk 9: 46-50

       KUJITEGEMEZA KWA MUNGU BABA YETU!
             Leo Injili inaanza na majadiliano kati ya wanafunzi wa Yesu juu ya nani aliye mkubwa. Yesu alikuwa amemaliza kuwaambia wanafunzi atakapo ingia Yerusalemu, atatiwa mikononi mwa wakuu na watawala na kwamba atauwawa. Ana wafumbulia kwamba bado kidogo atayapoteza maisha yake na wao madai yao wanajiuliza ni nani wa kwanza kati yao! Yesu anajibu jambo lao kwakumchukua mtoto mdogo na kumweka karibu yake. “Anaye mpokea mtoto mdogo kama huyu kwa jina langu amenipokea mimi…kwasababu aliye mdogo kati yenu ndiye aliye mkubwa”. Katika utamaduni wa kipindi cha Yesu, mtoto aliwakilisha “mdogo kabisa” kwasababu hawakuwa na chochote cha kumpa mtu. Utu wao ulikuwa ni kwasababu wapo tu, na sio kwasababu walikuwa na nguvu fulani au umaarufu fulani. Wakati tunapokuwa kuelekea utu uzima, mara nyingi, ni rahisi kudhani tunakuwa tunapunguza kuwa tegemezi na kuwa tayari zaidi kujitegemeza wenyewe. Yesu anatukumbusha kwamba, sivyo, ambapo ni vigumu kwa mtu kama sisi ambao tunafikiri sisi tunaji tosheleza na tunaweza kujijali na kupambana na mambo sisi wenyewe. Walio wakubwa ni wale wanao tambua wanahitahi wengine, wanao jiruhusu kuhusiana na wengine, kwasababu ni watu hao wanaotenda yaliyo katika asili ya Mungu na wanatambua asili yao wenyewe inategemezwa na Mungu. Tunapo jinyenyekesha na kukubali utegemezi wetu kwa Mungu na wengine, na kukubali udhaifu wetu na kuto kukamilika kwetu, ni vigumu kuwatenga wengine na kuwa hukumu wale ambao ni tofauti na sisi na wale wasio ishi kadiri ya sisi tunavyotaka. Tukianza kutembea katika njia hii, tutatambua kuwa tumenza kuwa wakubwa mbele ya macho ya Mungu. Tumtegee Mungu daima kama Ayubu kama tutakavyosikia kutoka katika somo la kwanza. Ayubu alitambua kuwa Mungu ndiye tegemezi kwake licha ya mabaya tena makubwa na majaribu mengi yaliompata. Yeye alisimama imara na alijua nguvu zake zina tegemezwa na Mungu. Sala: Bwana, tusaidie tuweze kutambua kwamba WEWE ni kielelezo, na kwamba ni wewe tunakutegemea kila wakati. Bwana naomba nisiwe tegemezi-binafsi bali niwe Yesu-ananitegemeza. Amina

Copyright ©2016 by shajara  and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG

MASOMO YA MISA, 26/9/2016 Jumatatu ya 26 ya Mwaka. " Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu. "


Jumatatu ya 26 ya MWaka

SOMO LA 1
Ayu 1:6-22

             Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako. Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana. Ilitukia siku moja hao wanawe na binti zake walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, mjumbe akamfikilia Ayubu na kumwambia, Hao ng'ombe walikuwa wakilima, na punda walikuwa wakilisha karibu nao; mara Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam, wamewaua hao watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wakaldayo walifanya vikosi vitatu, wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watumishi kwa makali ya upanga; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wanao na binti zako walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa; mara, tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba pembe zake nne, nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe. Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.

    WIMBO WA KATIKATI
    Zab 17:1-3, 6-7

       (1).   Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila.
          (K) Utege sikio lako ulisikie neno langu.
       (2).    Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili. Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, Umenihakikisha usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose,
              (K) Utege sikio lako ulisikie neno langu.
       (3).    Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu. Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kuume Uwaokoe nao wanaowaondokea.
              (K) Utege sikio lako ulisikie neno langu.

      SHANGILIO
    Mk 10:45

             Aleluya, aleluya Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi. Aleluya 
      
SOMO LA INJILI
        Lk 9:46-50

        Wanafunzi waliaanza kuhojiana, ni nani atakayekuwa mkubwa miongoni mwao. Naye Yesu alipotambua mawazo ya mioyo yao, alitwaa mtoto mdogo akamweka karibu naye, akawaambia, Ye yote atakayempokea mtoto huyu kwa jina langu anipokea mimi; na ye yote atakayenipokea mimi ampokea yeye aliyenituma. Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa. Yohana akajibu akamwambia; Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kwa jina lako; tukamkataza, kwa sababu hafuatani na sisi. Yesu akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu.

Copyright © 2016 by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG

Sunday, 25 September 2016

TAFAKARI: Jumapili, Septemba 25, 2016. “KISA CHA LAZARO NA TAJIRI”.


TAFAKARI
     Jumapili, Septemba 25, 2016.
  
  Dominika ya 26 ya Mwaka
    Amo 6: 1, 4-7
  Zab 146: 7-10 1
      Tim 6:11-16
      Lk 16: 19-31

         MATOKEO YA YESU!
         Leo katika Injili ya Luka tunakutana na mfano wa tajiri na Lazaro. Mfano huu una sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni maisha ya hapa duniani na sehemu ya pili ni maisha yajayo baada ya maisha ya duniani. Kuna mgongano wa tofauti kati ya sehemu hizi mbili zinapo linganishwa. Katika sehemu ya kwanza tajiri ana chakula kizuri na Lazaro ana njaa, na sehemu ya pili Lazaro yupo na Abraham na tajiri anateseka na kupata kiu. Inaogopesha na kutisha kusikia matokeo ya huyu tajiri katika maisha yajayo. Huyu tajiri hakufanya chochote kibaya, hakudanganya, au hakuiba chochote cha Lazaro. Sasa kwa nini apate adhabu kubwa namna hio? Kujibu hili swali, ni lazima na kwanza kabisa kujua kuna aina mbili za kutenda dhambi-ya kwanza, kutenda au kuamuru ili itendeke na pili kutokutimiza wajibu. Sisi tunajua dhambi za kutenda, kwa mfano kuiba, kusema uongo, kuiba nk. Kwa upande mwingine tunatenda dhambi kwa kutotimiza wajibu, na mfano mzuri wa dhambi ya kutotimiza wajibu ni mfano wa leo kutoka katika Injili. Huyu tajiri haku adhibiwa kwasababu alitenda kitu fulani, bali hakutimiza wajibu aliopaswa kutenda. Maskini Lazaro alikuwa katika mlango wake akiteseka na njaa na kuugua. Kwa hakika lazima huyu tajiri alikuwa akimuona kila wakati alipo ingia nyumbani mwake lakini hakuna hata siku moja alifikiria kumsaidia au angalao kumpa kitu cha kula hata angalao angempa mabaki ya chakula, hii ni kwasababu maskini Lazaro alikuwa tayari kula hata mabaki yaliyo dondoka katika meza yake. Tajiri huyu alishindwa kushirikisha utajiri wake hapa duaniani na hivyo anakosa kushirikishwa utajiri wa maisha yajayo. Hali hiyo hiyo inaonekana katika somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Amosi. Bwana anatoa ujumbe mdogo unao onesha kukuwa kwa tofauti kati ya matajiri na masikini. Hali ya uchumi ya Israeli kipindi cha Amosi ilikuwa imekuwa na kusitawi kama katika hali ya yule tajiri katika mfano wa Injili na maskini walikuwa maskini kweli kweli, katika hali ya kutisha kabisa. Mungu anawaka hasira yake kusema ‘Ole wao wanaostarehe’ wakati maskini na wahitaji wanateseka kwa njaa, wakati matajiri wana karamu zao za kondoo walio nona, divai, ninyi mnaolala juu ya vitanda vya pembe. Mungu hakasiriki kwasababu wanafurahia ni kwasababu wamesahau kuwajali masikini na kuwa shirikisha wahitaji wanao teseka kwa umaskini na njaa. Ndugu zangu kuwa tajiri sio kitu kiovu bali uovu nikuwa mchoyo, mbinafsi na usiyejali. Kanisa katika maandiko yake kuhusu mtizamo wa jamii inaongelea kuhusu lengo la rasili mali ya duniani. Kwa kufafanua kwa urahisi zaidi ni kwamba, wakati mtu akiwa na kitu/vitu vingi mno hata asivyo hitaji anakuwa amechukua sehemu ya mwingine anaye hitaji. Ukiukwaji wa mtizamo huu wa Kanisa, unakuwa unapinga wema ambao unapaswa kutendwa na hapo dhambi nyingi za kutotimiza wajibu huwa nyingi. Hali hii tunaiita “KISA CHA LAZARO NA TAJIRI”. Katika hali ya sasa, tunakutana na “KISA CHA LAZARO NA TAJIRI”. Kila mahali katika ulimwengu; tuna nchi kubwa zilizo endelea walio hifadhi chakula ambacho hata hawajui watatumia lini tofauti na Nchi maskini ambapo watu wake wana hangaika kila siku kupata mlo wa siku. Kuna majengo makubwa tena marefu katika miji yetu ya nchi zetu ambapo watu huishi maisha ya kifahari tofauti na watu wanaoshi katika hali ngumu tena bila kuwa na uhakika wakupata chakula au mlo wa siku. Kuna tofauti nyingi ambazo tunaweza kuoanisha katika maisha na leo Yesu anatuita tuweze kuondoa tofauti hizi katika maisha yetu na tuishi kwa upendo, kujaliana na usawa. Mt. Teresa wa Kalkata alisema “Kwa kidogo zaidi tulicho nacho ndivyo tunavyozidi kutoa zaidi, inaonekana kama ujinga lakini ndio mantiki ya upendo”. Aliguswa na MATOKEO YA YESU, kutafuta Amani, furaha na upendo kwa kuwa na kidogo na kwakutumia hicho kidogo kuwashirikisha wengine. Je, tunaweza kuchukua mfano wake kwa kuguswa na ujumbe wa Injili, kwa MATOKEO YA YESU na kuleta ufalme wa Mungu kati yetu. Matokeo ya Yesu maana yake, Yesu akigusa maisha yako na ukabaki mwaminifu kadiri ya mafundisho yake, matokeo yake ni kufurahi naye katika Maisha yajayo.
             Sala: Bwana Yesu, fungua macho yetu tuweze kuona mateso ya ndugu zetu wanao tuzunguka na utupe nguvu ya kushirikishana nao yale ulio tujalia, ili nawao waweze kuhisi upendo wako kwa kupitia sisi. Amina

Copyright © 2016 by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
       see: 

MASOMO YA MISA, 25/9/2016 Dominika ya 26 ya Mwaka. " Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu."


Dominika ya 26 ya Mwaka

SOMO LA 1 
Amo 6:1, 4-7
              Ole wao wanaostarehe katika Sayuni, na hao wanaokaa salama katika mlima wa Samaria, watu mashuhuri wa taifa lililo la kwanza, ambao nyumba ya Israeli huwaendea: ninyi mnaolala juu ya vitanda vya pembe, na kujinyosha juu ya masemadari yenu; ninyi mnaokula wana-kondoo wa kundi, na ndama waliomo zizini; ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi; ninyi mnaokunywa divai katika mabakuli, na kujipaka marhamu iliyo nzuri; lakini hawahuzuniki kwa sababu ya mateso ya Yusufu. Basi kwa ajili ya hayo sasa watakwenda utumwani pamoja na wa kwanza watakaokwenda utumwani, na kelele za machezo za hao waliojinyosha zitakoma.

    WIMBO WA KATIKATI
     Zab 146:6-10
        (1).    Bwana huwafumbua macho waliopofuka; Bwana huwainua walioinama; Bwana huwapenda wenye haki; Bwana huwahifadhi wageni;
             (K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
        (2).   Huwategemeza yatima na mjane; Bali njia ya wasio haki huipotosha. Bwana atamiliki milele, Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. Haleluya.
               (K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.

SOMO LA 2
      1 Tim 6:11-16

           Wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole. Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi. Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato, kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo;ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana; ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina.

     SHANGILIO
  Yn 17:17

            Aleluya, aleluya Neno lako ndiyo kweli, ee Bwana; Ututakase sisi kwa ile kweli. Aleluya

      SOMO LA INJILI
       Lk 16:19-31

                Yesu aliwaambia Mafarisayo, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu. Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu. Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu.

Copyright © by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI 
         website:

Saturday, 24 September 2016

TAFAKARI: 24/9/2016 Juma la 25 la Mwaka. " Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili, Mhubiri asema!” (Muh 12: 8)."


Jumamosi, Septemba 24, 2016.
Juma la 25 la Mwaka

      Mhu 11: 9 - 12: 8
   Zab 89: 3-6, 14, 17
      Lk 9: 43-45

     UBATILI: MAISHA BILA MUNGU! “Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili, Mhubiri asema!” (Muh 12: 8).

         Kitu ambacho Mwandishi anakiita ubatili ni maisha bila hofu ya Mungu. Maisha ya kufurahia maisha na zawadi zote tulizo pewa bila kujali nafasi ya mwenzangu (jirani) ambapo mtu anakuwa kipofu kuhusu mahitaji ya wengine. Lakini maisha anayoishi mtu kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya watu wake, yanakubalika sana na yana matunda mengi. Yesu leo katika somo la Injili anaongelea kuhusu kifo chake. Lakini mitume hawakuelewa fumbo hili kuu. Yesu alimpenda Baba yake sana kiasi kwamba alikuwa akijiandaa kutimiza mapenzi yake. Nasi ndicho tunachopaswa kufanya, tunapaswa tujitahidi kuyajua mapenzi ya Mungu kwetu na kujaribu kuyatimiza katika maisha yetu. Na hapo maisha yetu hayatakuwa maisha ya ubatili. Sala: Bwana mpendwa, tubariki wote na tuongoze ili tuweze kutambua mapenzi yako kwetu ili tuweze kuongozwa na maisha ya fadhila. Amina

Copyright © by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG

MASOMO YA MISA, 24/9/2016 Jumamosi ya 25 ya Mwaka " Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu."


Jumamosi ya 25 ya Mwaka 

       SOMO LA 1
     Mh 11:9 - 12:8
          Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni. Kwa hiyo ondoa majonzi moyoni mwako, nawe uuondoe ubaya mwilini mwako; kwa maana ujana ni ubatili, na utu uzima pia.Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo. Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua; Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema; Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; Na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba; Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza; Na milango kufungwa katika njia kuu; Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; Na mtu kusituka kwa sauti ya ndege; Nao binti za kuimba watapunguzwa; Naam, wataogopa kilichoinuka Na vitisho vitakuwapo njiani; Na mlozi utachanua maua; Na panzi atakuwa ni mzigo mzito; Na pilipili hoho itapasuka; Maana mtu aiendea nyumba yake ya milele, Nao waombolezao wazunguka njiani. Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani; Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa. Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!

         WIMBO WA KATIKATI
        Zab 90:3-6, 12-14, 17
         (1).    Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo, Rudini, enyi wanadamu. Maana miaka elfu machoni pako Ni kama siku ya jana ikiisha kupita, Na kama kesha la usiku.
            (K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi.
         (2).     Wawagharikisha, huwa kama usingizi, Asubuhi huwa kama majani yameayo. Asubuhi yachipuka na kumea, Jioni yakatika na kukauka.
            (K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi.
          (3).     Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima. Ee Bwana urudi, hata lini? Uwahurumie watumishi wako.
               (K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi.
          (4).     Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote. Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu, Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti, Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe.
                 (K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi. 

         SHANGILIO
         2 Tim 1:10
        Aleluya, aleluya Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili; Aleluya

    SOMO LA INJILI
      Lk 9:43-45
          Makutano walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu. Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.

Copyright © by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG

Friday, 23 September 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 25 YA MWAKA-C, “Kwa kila jambo kuna majira yake.”


IJUMAA WIKI YA 25 YA MWAKA-C 

Somo: 
Mhu 3:1-11 
Zab/Kit: 144:1a, 2abc, 3.4
Injili: Lk 9:18-22

 Nukuu: 
      “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu,” Mhu 3:1
       “Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo?”  Mhu 3:9
     “Nimeiona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake,” Mhu 3:10
     “Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho,"  Mhu 3:11
       “Akawaambia, Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu,” Lk 9:20

 TAFAKARI:
           “Kwa kila jambo kuna majira yake.” 
            Wapendwa wana wa Mungu, ikiwa kitabia na kimakuzi ni tokeo la historia yako na jamii iliyomzunguka, basi kile tulicho leo, yaani, kimwili na kiroho kimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na historia yako na jamii hiyo iliyokuzunguka. Leo katika taifa letu tunapambana na rushwa na ufisadi uliotukuka. Hali na mazingira haya yanataka kuibadilisha ovu hilo kuwa sifa. Ni jambo la kushangaza sana unapoona jamii kutokushtushwa na ubadirifu mkubwa wa mali ya umma. Badala yake tukio kubwa liwe ni rushwa au ufisadi linaongelewa kiushabiki ilhali tendo hilo linaangamiza taifa wakiwemo na hao ‘malimbukeni’ katika ubora wao wa kiushabiki. Ni wazi kabisa tunapoona idadi kubwa ya wale waliopewa dhamana na umma kuwa viongozi na kwa idadi yao ndio wala rushwa na mafisadi wakubwa, ni wazi jamii tunayoishi imeoza. Viongozi hao, au wala rushwa hawa na mafisadi ni tunda la jumuiya husika. Na tunapokwenda kwenye jumuiya au jamii husika tunagundua kwamba jamii hiyo imejengwa katika misingi ya kifamilia. Hivyo familia kama shule ya kwanza katika makuzi na malezi ya kila mmoja wetu kimwili na kiroho, nayo imeoza. Baadhi ya familia hujeuka na kuwa kichaka cha mafisadi na wala rushwa. Hivi unawezaje kwa mfano kuhafikiana na hali ambayo mzazi anakuwa mpiganaji namba moja kupita njia za panya ili mtoto wake afanikiwe? Je, huyu ambaye amepita njia za panya hadi kufikia nafasi hiyo ya juu katika jamii aweza kuwa mtu wa haki na kweli? Leo yale yote tunayotaabika nayo wakati fulani watu fulani na jamii fulani haikuenenda katika haki na kweli. Kwani “kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu,” Mhu 3:1. Hakika kwa yale yasiyo haki na kweli ni kinyume na makusudi ya kuumbwa kweli, na mwisho wa siku hatuta faidika na chochote. Jambo lolote lile lisilo akisi umilele wake ni sawa na kupanda upepo na mwisho wa siku jiandae kuvuna kimbunga. “Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo?” Mhu 3:9. Na mbaya zaidi kama hayo anayojishughulisha nayo hayana chembe ya umilele. Ndugu yangu, ingawa tupo hapa duniani kwa muda mfupi sana, kila jambo lina wakati wake, Mhu 3:2-8. Pamoja na ukweli huo, Je! watumiaje muda huu mfupi hapa duniani? Au umeamua kuishi kama inzi ambaye umri wake ni siku saba tu, na hupenda kutua kila mahali bila kujali kwamba anahatarisha maisha yake? Hakika Mungu husikitishwa sana pale anapoona unaishi nje ya makusudi yake, yaani, amekuumba ili uishi milele. Naye Mhubiri katika hili anasema, “nimeiona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake,” Mhu 3:10. Na taabu hii si kitu kingine zaidi ya uhuru ule Mungu aliotupatia. Ni katika uhuru huu tunaweza kumwazi Mungu au kujisalimisha kwake katika toba ya kweli na majuto. Katika mpango wake Mungu tangu kuumbwa ulimwengu, “kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho,” Mhu 3:11. Ni katika kweli hii tunaona kwamba uumbaji wa ulimwengu huu kwa kiasi kikubwa umemlenga mwanadamu na wokovu wake. Je, tunadhamisha kweli hii kwa kuulinda ulimwengu huu ili kuwa sehemu salama zaidi ya kuishi? Leo tunaona ni kwa namna gani binadamu huu alivyo kuwa “Mr. Kipepe,” anavyo kata tawi lile alilokalia. Hata hivyo mimi na wewe leo yanipasa kumjua huyu Yesu ni nani kwangu. Kwa upande wake Yesu, kama kiongozi na mwenye kujali na kuwajibika, alitaka kujua kutoka kwa watu na hata kwa wanafunzi wake wa karibu kabisa wanamtazamo gani juu yake. Mtume Petro anatoa jibu sahihi kuhusu Yesu, na lile lililo mpasa Kristo katika ulimwengu huu. “Akawaambia, Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu,” Lk 9:20. Mpendwa unayesafiri nami katika tafakari hii nikuulize swali la msingi; pamoja na majibu ya wengine, na hasa jibu alilolitoa Petro kuhusu swali alilouliza Yesu, wewe binafsi Yesu kwako ni nani? Jibu la Petro kwa tafasiri, Kristo, yaani ‘Masiha wa Mungu,’ ndiye yeye tu aliyewekwa katika mpango mzima wa ukombozi wa mwanadamu. Hivyo tutaiona mbingu na kuufurahia uhuru wa kweli endapo tu tutakuwa tayari kushikamana na mwana huyu wa Mungu. “Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina lingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:11-12. Hivyo kufikia hatua hii la kuokolewa kwetu kupitia jina hili hatunabudi kushiriki njia ile aliyopitia Bwana wetu Yesu Kristo kama anavyowanong’onozea wanafunzi wake siri hii na kusema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka,” Lk 9:22. Ndugu yangu hakuna PASAKA PASIPO IJUMAA KUU. Ndivyo hivyo kwetu kama wafuasi wake Kristo tulio hai kwamba hakuna UTUKUFU PASIPO MSALABA. Leo wapo watu kati yetu wamejawa hofu na hawapendi kukosolewa hata kuzungumziwa, ili hali Yesu aliye Mungu na Mwanadamu aliruhusu watu wasema kile waonacho kuhusu Yeye. Uhuru huu wa kukosolewa ni uthibitisho wa kiongozi asiyekuwa na mawaa wala makandokando. Tumsifu Yesu Kristo! “Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu,” Lk 9:20 Tusali:-Ee Yesu, kwa maisha yako hapa duniani, yatakase pia maisha yetu ili tuifuate njia yako kikamilifu. Amina

Copyright © by Fr Edgar Tanga Ngowi,OSA.  and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG 
     website: 
imani-katoliki.blogspot.com

MASOMO YA MISA,23/9/2016 Juma la 25 la Mwaka. " Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu."


MASOMO YA MISA IJUMAA,
SEPTEMBA 23, 2016
JUMA LA 25 LA MWAKA

KUMBUKUMBU YA MT. PADRE PIO WA PIETRELCINA, MKAPUCHINI.

      SOMO 1
Mhu. 3:1 – 11
          Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa; wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa; wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena; wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; wakati wa vita, na wakati wa amani. Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo? Nimeiona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake. Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.
      Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

     WIMBO WA KATIKATI
   Zab. 144:1 – 4 (K) 1
             (K) Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu.
        (1).   Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu, Mhisani wangu na boma langu, Ngome yangu na mwokozi wangu, Ngao yangu niliyemkimbilia. (K)
        (2).   Ee Bwana, mtu ni kitu gani hata umjue? Na binadamu hata umwangalie? Binadamu amefanana na ubatili, Siku zake ni kama kivuli kipitacho. (K)

SHANGILIO
     Zab. 119:135
       Aleluya, aleluya, Umwangazie mtumishi wako uso wako, na kunifundisha amri zako. Aleluya.

INJILI
    Lk. 9:18 – 22
            Yesu alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwapo pamoja naye, akawauliza, Je! Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani? Wakamjibu wakisema, Yohane Mbatizaji; lakini wengine, Eliya; na wengine kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. Akawaambia, Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani?
Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu. Akawaonya, akawakataza wasimwambie mtu neno hilo. Akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka.
       Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo

Copyright © by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
      website:

Thursday, 22 September 2016

TAFAKARI YA MASOMO YAMISA,22/9/2016 "Kutumikia mungu na jirani".


TAFAKARI
Alhamisi, Septemba 22, 2016.
       Juma la 25 la Mwaka

         Mhu 1: 2-11
Zab 89: 3-6, 12-14, 17
Lk 9: 7-9

   KUTUMIKIA MUNGU NA JIRANI!
            Katika somo la Injili ya leo, tunasikia Herode, akifadhaika baada ya kupata habari kuhusu Yesu. Alama iliyo baki katika dhamiri yake bado inaendelea kumkumbusha kuhusu damu aliyo mwaga ya mtu asiye na hatia ya Yohane Mbatizaji. Sehemu ya pili ya Injili pia inatueleza nini kinacho leta furaha –kumtumikia Bwana, na pia kuwafikia wengine. Maisha ya Herodi hayakukosa chochote cha anasa na maisha ya kujiburudisha. Lakini, watu hawakuwa wanaongea kuhusu yeye. Wote walikuwa wakiongelea kuhusu Kristo. Baba Mtakatifu mstaafu Benedict wa XVI alisema “Kanisa linalo tafuta kuwa kivutio na maarufu kuliko yote tayari lipo katika njia isio sahihi, kwasababu Kanisa halifanyi kazi kwa ajili yake binafsi, halifanyi kazi ili kuongeza idadi ya watu na nguvu zake. Kanisa lipo kwa ajili ya kuwatumikia watu. Halijitumikii, halitumikii ili kuwa lenye nguvu, bali, linatumikia ili kumtangaza Yesu Kristo: ukweli mkuu, nguvu kuu ya upendo na msahama unao jionesha kwake na ambao unatokea kila wakati kwa uwepo wa Yesu Kristo
   Sala: Bwana, niongezee tamaa yangu ya kufanya mapenzi yako na kuwatumikia wengine kwa mapendo. Amina.

Copyright © by shajara  and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
website:
imani-katoliki.blogspot.com

MASOMO YA MISA,22/9/2016 Alhamis ya 25 ya Mwaka.


Alhamis ya 25 ya Mwaka
SOMO LA 1
Mhu 1:2-11
           Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili. Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua? Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima. Jua lachomoza, na jua lashuka, na kufanya haraka kwenda mahali pa maawio yake. Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake. Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena. Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia. Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua. Je! Kuna jambo lo lote ambalo watu husema juu yake, Tazama, ni jambo jipya? Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi. Hakuna kumbukumbu lo lote la vizazi vilivyotangulia; wala hakutakuwa na kumbukumbu lo lote la vizazi vitakavyokuja, miongoni mwao wale watakaofuata baadaye.

                 WIMBO WA KATIKATI
          Zab 90:3-6, 12-14, 17
        (1).    Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo, Rudini, enyi wanadamu. Maana miaka elfu machoni pako Ni kama siku ya jana ikiisha kupita, Na kama kesha la usiku. 
            (K)Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi                 (2).    Wawagharikisha, huwa kama usingizi, Asubuhi huwa kama majani yameayo. Asubuhi yachipuka na kumea, Jioni yakatika na kukauka.
                 (K)Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi
        (3).     Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima. Ee Bwana urudi, hata lini? Uwahurumie watumishi wako.
              (K)Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi
        (4).    Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote. Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti, Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe.
              (K)Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi

       SHANGILIO
     Zab. 27:11
              Aleluya, aleluya, Ee Bwana, unifundihse njia yako, na kuniongoza katika njia iliyonyoka. Aleluya.

          SOMO LA INJILI
        Lk 9:7-9
           Herode mfalme akasikia habari za yote yaliyotendeka, akafadhaika kwa sababu watu wengine walisema ya kwamba Yohana amefufuka katika wafu, na wengine ya kwamba Eliya ametokea, na wengine ya kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. Lakini Herode akasema, Yohana nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona.

Copyright © by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
        website:

imani-katoliki.blogspot.com

Wednesday, 21 September 2016

TAFAKARI YA MASOMO YA MISA,21/9/2016. Jumatano ya 25 ya Mwaka.


Jumatano, Septemba 21, 2016. 
Juma la 25 la Mwaka


Sikukuu ya Mt. Mathayo, Mtume na Mwinjili 


Efe 4:1-7, 11-13
Zab 19:1-4
Mt 9: 9-13

MUNGU HAWAITI WAKAMILIFU, ANAWAPA UKAMILIFU WALE ALIO WAITA 

         Leo tuna sheherekea sikukuu ya Mtakatifu Matayo, mmoja wapo wa mitume kumi na mbili wa Bwana wetu Yesu Kristo. Alikuwa mtoza ushuru, alijulikana kama Lawi. Hapa anaitwa Matayo, maana yake “zawadi ya Mungu au aliyetolewa na Mungu”. Kama wale wakwanza wanne walio itwa na Yesu kwanza,  Matayo, mtoza ushuru, aliacha kila kitu alichokuwa nacho na akamfuata Yesu. Wakati wa Yesu watu maarufu na watoza ushuru walikataliwa kama wadhambi kwa Wayahudi kadhalika na kwa Wayunani. Walikuwa na picha mbaya kiasa kwamba hata waombaji (omba omba) wenyewe walikataa kuomba chochote kutoka kwao. Ni katika utamaduni huu, Yesu alimuita Matayo/Lawi. Hii ni hali mpya ya kimapinduzi anayo fanya Yesu ili kujenga familia mpya ya Mungu. 

Kuna vitu viwili tunaweza kujifunza kutoka kwa Matayo. Cha kwanza, alikubali mwenyewe wito wa Yesu. Wakati Mungu anapo ongea mmoja anaweza kupata kishawishi cha kusema ‘kesho; bado sijawa tayari’. Lakini Matayo mara moja aliitika wito wa Yesu. La pili, Matayo anaitwa akiwa katika mazingira ya hali yake ya maisha ya kawaida, wakati akijishughulisha na kazi yake. Yesu pia aliwaita mitume wa kwanza, Petro na Adrea, Yakobo na Yohane wakati wakiwa wakivua samaki. Leo tutambue kwamba sisi ni wadhambi lakini bado Mungu anatupenda, tumuombe nguvu zake na neema zake ili tuwe na maisha yenye kustahili wito wake.

Sala: Bwana Yesu, tusaidie tuweze kuitika wito wako na tutangaze ujumbe wa Amani na upendo. Amina

Copy right © by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG 
         website:
imani-katoliki.blogspot.com

MASOMO YA MISA,21/9/2016. Jumatano ya 25 ya Mwaka-C


MASOMO YA MISA 
JUMATANO, SEPTEMBA 21, 2016
JUMA LA 25 LA MWAKA


Sikukuu ya Mt. Mathayo, Mtume na Mwinjili



SOMO 1
Efe. 4:1 – 7, 11 – 13

Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani, mwili mmoja, na Roho mmoja, Imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. Lakini kila mmoja wenu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Naye alitoa wengine kuwa mitume; na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti; na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa Imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 19:1 – 4 (K) 4

(K) Sauti yao imeenea duniani mwote.

Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa. (K)

Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. (K)


SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Ee Mungu, tunakusifu, 
tunakukiri kuwa Bwana. 
Jamii tukufu ya Mitume inakusifu.
Aleluya.


INJILI
Mt. 9:9 – 13

Yesu alipokuwa akipita aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata. Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo


Copy right© by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
       website:

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...