Sunday, 13 October 2019

TAFAKARI YA MASOMO YA MISA, DOMINIKA YA 28 YA MWAKA "C" WA KANISA



Somo I: 2Fal 5:14-17
Zab/Kit: 98:1-2, 3ab, 3cd-4
Somo II: 2Tim 2:8-13
Injili: Lk 17:11-19
Nukuu
“Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi,” 2Fal 5:14
“Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa iwako,” 2Fal 5:15
 “Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!” Lk 17:12-13
“Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika,” Lk 17:14
 “Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?” Lk 17:17
 “Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu,” 2Tim 2:8
“Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi,” 2Tim 2:9

TAFAKARI:
      “Kujishusha na kujinyenyekesha mbele ya Mungu ndio ufunguo wa maarifa na siri ile ihusuyo uzima ule wa milele.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 28 ya mwaka “C” wa Kanisa. Na kwa namna ya pekee, Mama Kanisa leo anatutaka kwa pamoja tutafakari, “unyenyekevu ukiwa ndio msingi wa Fadhila zote, ndio ufunguo wa maarifa na siri ile ihusuyo uzima wa milele.” Na tufanyavyo hivyo na kuishi, Mungu atatenda. Masomo yote matatu ya leo yanatuwasa kutafakari sana tendo hili la unyenyekevu na kujinyenyekesha. Bila shaka wote twafahamu vizuri habari za Jemadari Naamani, na uponyaji wake kupitia Nabii Elisha. Safari ya uponyaji wake haikuwa rahisi, kutokana na njia, na namna ya uponyaji ule ulivyokuwa uwe kwa namna Mungu alivyopenda.
Hata hivyo mara nyingi hatuyapati yale tuombayo, na hata uponyaji wa yale yatusumbuayo kutokana na mitazamo yetu kimaisha, na namna tutakavyo Mungu kufanya huruma na upendo wake kwetu. Mtume Yakobo anasema hivi, “hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,” Yak 4:3. Kumbe niwapo mbele ya Mungu, ni jambo la msingi na muhimu sana kujishusha na kujinyekesha huku nikitambua ubinadamu wangu, na kwa huo ubinadamu sote ni wahitaji na waja wa Mungu.
Mungu utukweza tu pale tunapojishusha na kujinyenyekesha kwake na kuukubali ubinadamu wetu. Mungu daima anabaki kuwa Mungu. “Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, na ajidhiliye atakwezwa,” Lk 14:11. Mtoza ushuru katika sala yake hekaluni, kinyume na Mfarisayo, sala yake (Mtoza ushuru) ilisikika mbele ya Mungu kwa sababu alijishusha na kusema kwa unyenyekevu na kwa uchache wa maneno kabisa, “Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi,” Lk 18:13. Kwa tendo hili la unyenyekevu la mtoza ushuru, Yesu anasema, “Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; (Mfarisayo) kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa,” Lk 18:14

Jemadari Naamani anapata uponyaji wa ukoma wake baada tu ya kujishusha na kufanya kadiri ya mapenzi ya Mungu. “Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi,” 2Fal 5:14. Ndugu yangu, Mungu ana njia nyingi na mbalimbali za kufikishia ujumbe wake kwetu kadiri ya hitaji letu, na kwa kupitia jambo hilo au uponyaji huo iwe au liwe somo la maisha.
Mwanzoni tunaona Naamani anashindwa kupokea njia ya uponyaji ule, yaani, kujichovya mara saba katika mto Jordani, kwa kujitazama historia yake, na ufahamu wake. Mpendwa, “Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mipaka,” Zab 147:5. Hatuwezi kumpangia Mungu namna ya kufanya hata kama tukiwa na nia njema afanye yale tumwombayo na tunayotamani.
Ndugu yangu, hata Yesu mwenyewe, alimwachia Baba yake-Mungu atende kadiri ya mapenzi yake. “Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe,” Mt 26:39. Kama huyu, yaani, Mwana wa Mungu na Mwenye Uweza wote anajinyenyekeza na kujiachia mikoni mwa Baba yake, mimi na wewe tuna nini cha kujikweza hata kama historia yetu inaonyesha hatujawahi kushindwa?
Naamani Jemadari, anapojishusha, jinyenyekeza, na kumwachia Mungu atende kadiri ya neno lake kupitia Mtumishi wa Mungu Nabii Elisha, Mungu anatenda mara moja. “Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi,” 2Fal 5:14. Kujinyenyekesha na kujishusha ni kukiri Ukuu wa Mungu kabla na baada atendapo mema yake kwako. Uponyaji wa Naamani Jemadari, unaibua hisia za uchaji na utambuzi wa Mungu huyu wa Ajabu, na kusema, "Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli,” 2Fal 5:15.

Ndugu yangu, tunachojifunza katika maisha yetu ya sala na unyenyekevu ni kwamba tunapokuwa mbele ya Mungu yatupasa kujua kwamba sisi ni viumbe tu, na wahitaji na waja wake Mungu. Mungu haitaji kujua mazuri yetu kwa sababu hayatampunguzia Wema, Upendo, Uzuri, na Ukuu wake. Mungu pia haitaji historia ya yale tuyafanyayo kama alivyofanya Mfarisayo, bali tusiache kutenda mema kwani Yeye aliye Mwema katika yote na uzuri wote ataonekana katika matendo hayo mema, na hasa tunapoyatenda kwa wale aliowaumba kwa sura na mfano wake.
Naamani baada ya kutendewa tendo hili kuu na Mungu kupitia Nabii wake Elisha, anataka kumtolea Elisha kitu kama tendo la shukrani. Elisha anakataa tendo lile kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kujifananisha na Mungu. Elisha kwa unyenyekevu anatambua nafasi yake kama mtumishi tu, tena asiye na faida. Katika tendo hili la Nabii Elisha, tunajifunza pia kile anachotufundisha Kristo Yesu kuhusu utumishi. Naye  Yesu anasema, “vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10. Hakika yatupasa kutumika na siyo kutumikiwa.
Kutokana na msimamo wake Elisha, tendo lile la kukataa kutolewa kitu linagusa mtima wa Naamani, naye anaweka ahadi yake kwa Mungu aliye hai. Naye anasem, “Kama sivyo (kutokupokea kitu), lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa Bwana,” 2Fal 5:17. Tumwache Mungu aitwe Mungu, na ndivyo alivyo.

Ni kwa upendo wake Mungu katuumba kama tulivyo, yaani, kwa sura na mfano wake, na ndivyo tulivyo wanadamu. Na kuishi ubinadamu wetu kwa uaminifu na hofu ya Mungu kwa lengo lile alilotuumba, yaani, tumjue, tumpende, tumtumikie, na mwisho turudi kwake mbinguni, ndipo lilipo taji letu, yaani, utakatifu wako. Ni utakatifu huo ambao ndio cheo chako ndio wezesho la wewe kuuona uso wa Mungu. Bila utakatifu huwezi kumwana Mungu, kwa sababu Yeye ni Mtakatifu.
Hivyo ni mwaliko kwako na mwangu leo na kila kutenda kama wa watoto wachanga. Watoto wachanga ndiyo hufunuliwa mambo ya Mungu kutokana na kujiaminisha pasipo shaka kwa wazazi wao. Katika hili Yesu anasema, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga,” Mt 11:25. Utendaji huu kama watoto ndio utupao fursa ya kuurithi  ufalme wa Mungu.  “Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 19:14.

Mwisho wa siku ndugu yangu, “tutahukumiwa au kutathminiwa kwa upendo wetu,” kama asemavyo Mtakatifu Yohana wa Msalaba. Kwa hiyo, yale yote tufanyayo na tujihesabie tu kuwa tumefanya yale yampendezayo Mungu. Hatuna chochote za kujivunia mbele ya Mungu zaidi ya kujishusha na kujinyeyekesha. Mafanikio yetu ni moja ya uzuri wake Mungu. Mapungufu yetu ni sababu ya ubinadamu wetu, na katika kujishusha na kujinyenyekeza mbele zake Mungu hatachoka kuzifungua neema na huruma yake kwetu. Mtume Paulo anasema, “Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Kumbe mimi kama Mkristo kujivuna kwangu iwe Msalaba wake Kristo kwani hakuna Utukufu pasipo Msalaba.

Katika jambo hili ndugu yangu, yatupasa kujua kwa uhakika kwamba Yesu Kristo ndiye kielelezo cha UNYENYEKEVU. Kifo cha Msalaba na cha Aibu ni kwa sababu yangu na wewe. Basi, tujivunie tu Msalaba kwani kwayo kuna Utukufu. Vingine vyote ni vya kupita tu. Mtume Paulo anatuambia makusudi ya Yesu kufanya hayo yote ni kwamba, “ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu, tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:6-8. Je, ndugu yangu, una cho chote cha kujivunia na na kukufanya kutokushuka na kujinyenyekesha kwa Mungu?
Katika Injili ya leo tunaona ‘fanya zaidi’ ya waleo wakoma kumi walivyo yakazi macho yao kwa Kristo Yesu, na kwa ummoja wao, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!” Lk 17:13. Ndugu yangu, lazima ufahamu msaada wako unatoka wapi hasa pale unapoona giza tupu katika maisha yako. Uponyaji wa wakoma hawa ni tofauti kabisa na ponyaji nyingine alizokwisha kuzifanya Yesu. Yesu anawataka ‘kufanya zaidi’ na kuwaambia, “Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika,” Lk 17:14. Wakoma hawa wanatakasika wakiwa njiani. Kumbe wakati mwingine kupona kwako kwaweza chukua hatua kwa lengo la kukuimarisha kiimani, na kukupatia utakaso kamili. Kumbe yote ni neema na heri, na kamwe nisilitoe tumaini langu kwa yule anipaye uzima huo, yaani, Mungu muumba wangu.
Katika tendo hili la uponyaji lililo la baraka na neema, unyenyekevu unajidhihirisha kwa tendo la shukrani. Ni mambo mangapi tunakutana nayo njiani ya neema na baraka ila hatuoni sababu ya kushukuru? Ni mmoja tu kati ya wale kumi aliyekuja kwa Yesu naakaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria,” Lk 17:16. Tendo hili linamshangaza sana Yesu, naye akamjibu, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?,” Lk 17:17. 
Ona jinsi tunavyomshangaza Mungu tunavyokoswa moyo wa shukrani kwa yale anayotutendea. Ndugu yangu tuliyesafiri pamoja katika tafakari hii, bado tu hauna cha kumshukuru Mungu?
Jambo lingine la pekee katika tukio hili la uponyaji ni kile mtu apatacho mwisho wa uponyaji huo. Wale tisa ambao hawakuja kutoa shukrani walipokea uponyaji wa mwili, na kuwa huru kutoka mateso yale ya ukoma. Ni huyu mmoja tu, tena Msamaria aliyepata vyote, yaani, uponyaji wa mwili na wokovu. Katika kweli hii Yesu anamwambia, “Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa,” Lk 17:19. Hakika moyo usio na shukrani ukausha mema yote! Tunapoutazama kwa ukaribu uhusisano kati ya Wayahudi na Wasamaria, katika uponyaji huu unaweka wazi maneno haya ya Yesu, kwamba, “vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho,” Mt 20:16. Mungu wetu hana upendeleo, Mdo 10:34-35, hasa pale tunapomwelekea kwa hofu na uchaji wa kweli.
Wapendwa wana wa Mungu, mwanadamu kwa kuumbwa kwake, Mwa 1:27, na uwepo wake hapa duniani, mara zote hutafuta maana ya maisha yake. Hufanya hivyo si kwa bahati mbaya, au udadisi fulani usio na mwalekeo, bali kama alivyo, mwanadamu usukumwa kufanya hivyo kama tokeo la historia  yake kijamii na jamii anayoishi leo na sasa. Hivyo, mwanadamu huyu hapo alipo kadiri ya imani na maadili yake, hakosi kuifikiria kesho ambayo bado kuiishi akiwa na matumaini kuwa ipo na yaja.
Na kama ni Mkristo achoki kuyafikiria maisha yale ya umilele na hukumu yake ya mwisho, kwa sababu anatambua wazi maisha ya hapa duniani ni jukumu la muda mfupi tu.Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya,” 2Kor 5:10. Kwa hali hii, mazingira haya, na mtazamo huo, mwanadamu hakosi kutafuta maana ya maisha yake. Utafutaji wa maana juu ya maisha yake humpa pia maana ya mahangaiko na mateso yake.
Katika hali hii Mtume Paulo anasema, Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi,” 2Tim 2:9. Neno la Mungu ni hai, na pia ni uhai. Tulisadiki neno kama alivyofanya Diwani yule wa Kana ya Galilaya, Yoh 4:46, mwanaye aliyekuwa hajiwezi, naye akapata uponyaji. Yesu akamwambia, Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia,” Yoh 4:50 
Maisha yakikosa maana, binadamu hujikabidhi katika ‘ovu’ lolote lile bila kujali chochote kwa sababu maisha yake kesha yahesabu kuwa si chochote. Huku ni kutaka tamaa pale tunapokosa tumaini la kweli. Matendo ya uovu tunayoyashuhudia kila siku katika jamii yetu ni ishara ya watu kukata tamaa na kupoteza tumaini la kweli katika maisha yao. Ni vyema kama jamii tukajiuliza ni wapi tulipoupoteza ufunguo huo wa tumaini la kweli. Utoaji wa matamko kila siku na kwa kila tukio bila ukomo kamwe hatuta upata ufunguo huo wa tumaini la kweli. Kumbe yatupasa kila mmoja na kwa nafasi aliyokuwa nayo katika jamii, ikiwa ni pamoja na wale wenye weledi wa mambo haya ya kijamii kufanya tathmini ya kina kuhusu mwenendo mzima wa jamii yetu leo. Swali ni hili: Kwa nini tunafanya kama tunavyofanya?
Tunapo mtazama Mtume Paulo tunagundua kuna kitu tofauti. Yesu Kristo ndiye nahodha wa maisha yake, na kwake, yaani kwa Kristo, maisha yake (Paulo Mtume) yamepata maana halisi. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. 
Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe,” 2Tim 2:10-13. Huyu ndiye Kristo ambaye kwake kama wafuasi wake, kuna tumaini la kweli.
Hata pamoja na ukweli huo, Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli,” 2Tim 2:15. Ndani na katika Yesu Kristo hakuna sababu ya kuishi kwa hofu. Na kujishusha na kujinyenyekesha mbele ya Mungu ndio ufunguo wa maarifa na siri ile ihusuyo uzima ule wa milele.
Basi nikuache na mfano huu: ‘kwa wale ambao ni madereza, na hata sisi ambao ni wasafiri tu, bila shaka tumewahi kukutana na kitu kinachoitwa “shokamzoba.” Shokamzoba ni aina ya chuma fulani imara na chenye umbo la kujisokota katika mtindo wa duara na kufanya mnaso fulani.

Pamoja na kazi kubwa ya shakamzoba kuzuia uharibufu au uvunjikaji wa vitu vilivyo kwenye mwendo, shokamzoba utujengea hisi fulani tofauti ya pale tulipo na kile kinachoendelea nje ya mazingira yale tuliyopo. Mara nyingi katika kweli hii wengi hatuguswi kwa sababu utulivu tulionao wakati huo upoteza kweli hii. Katika hali hii ya utulivu ilhali tupo kwenye mwendo kasi, shokamzoba huwa mwimili wa kila kitu.

Hivyo vyote vibebwavyo juu yake hubaki salama tu iwapo shokamzoba hizi zitabaki katika hali yake ya usalama. Katika maisha ya mwanadamu, shokamzoba ndiyo fadhila kuu ya unyenyekevu. Bila unyenyekevu, yote tuyajengayo juu yake, yaani, fadhila nyingine zote, hukosa msingi imara. 
Kuijenga jamii mpya na yenye mwelekeo chanya, mimi na wewe lazima yatupasa pasipo shuruti kuwa shokamzoba.’

Tumsifu Yesu Kristo!
“Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi,” 2Tim 2:9

Tusali:- Ee Yesu Mwema, nijalie fadhila ya Unyenyekevu. Amina

Copyright © 2016 by Fr Edgar Tanga Ngowi, OSA  and. Published  by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG 

MASOMO YA MISA, DOMINIKA YA 28 YA MWAKA "C" WA KANISA


Dominika ya 28 ya Mwaka

     SOMO LA 1
               2 Fal 5:14-17
            Naamani alishuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi. Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako. Lakini akasema, Kama Bwana aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa. Naamani akasema; Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa Bwana.

Neno la Mungu..... Tumshukuru Mungu

          WIMBO WA KATIKATI
         Zab 98:1-4

        (1).   Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake wenyewe, Mkono wake mtakatifu umetenda wokovu
                   (K) Bwana ameufunua Soloviev wake machoni pa mataifa
        (2).     Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake
                   (K) Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa
       (3).  Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu, Mshangilieni Bwana, nchi yote. Inueni sauti, imbeni kwa furaha
                    (K) Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa

           SOMO LA 2
              2 Tim 2:8-13

           Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi.
Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa.
Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa.
Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.

Neno la Mungu...... Tumshukuru Mungu.

       SHANGILIO
           Yn 10:27

             Aleluya, aleluya Kondoo wangu waisikia sauti yangu, asema Bwana: Nami nawajua nao wanifuata. Aleluya

      SOMO LA INJILI
        Lk 17:11-19

                 Yesu alipokwenda njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya.
Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani.
Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.
Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.

Neno la Mungu...... Sifa kwako Ee Mungu.

Copyright © 2016 by shajara  and published   by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
    see: imani-katoliki.blogspot.com

Sunday, 22 September 2019

WIMBO WA KATIKATI DOMINIKA YA 26 MWAKA "C"



✝🎢🎢🎡🎡🎢🎡🎡✝

MTUNZI: CAROL STEPHEN

Maneno ya wimbo
KIITIKIO:
           Ee nafsi yangu Umsifu Bwana, Ee nafsi yangu Umsifu Bwana×2.
       MASHAIRI:

  1. Bwana, huishika kweli kweli milele, huwafanyia hukumu walio onewa.
  2. Bwana, huwafumbua macho walio pofuka, huwainua walio walio inama.
  3. Bwana, huwategemeza yatima na mjane, Bali njia ya wasio haki huipotosha.

PAKUA NOTA ZA WIMBO HAPA CHINI:
http://www.swahilimusicnotes.com/wimbo/nafsi-yangu-umsifu-bwana/16780

Monday, 15 July 2019

JUMATATU YA 15 YA MWAKA "C" WA KANISA.

Masomo ya Misa 15/07/2019

Somo la Kwanza
Kut 1:8-14,22
            Aliinuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi, tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, kukitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii, Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli. Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali. Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake, akisema, Kila mtoto mwanamume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtahifadhi hai

Neno La Mungu........   Tumshukuru Mungu.

Wimbo wa katikati
Zab 124
Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Israeli na aseme sasa,
Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi
wanadamu walipotushambulia.
Papo hapo wangalitumeza hai,
Hasira yao ilipowaka juu yetu.
(K) Msaade wetu u katika jina la Bwana.

Papo hapo maji yangalitugharikisha,
Mto ungalipita juu ya roho zetu.
Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu
Maji yafurikayo.
(K) Msaade wetu u katika jina la Bwana.

Na ahimidiwe Bwana:
Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno hayo.
Nafsi yetu imeokoka kama ndege
Katika mtego wa wawindaji,
Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.
(K) Msaade wetu u katika jina la Bwana.

Shangilio
1 Sam. 3:9 Yn. 6:68
Aleluya, aleluya,
Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia: wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.

Somo la Injili
Mt. 10:34 - 11:l
         Yesu aliwafundisha mitume wake: Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! sikuja kuleta amani, bali upanga. Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu; na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake. Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona. Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipomimi, ampokea yeye aliyenituma. Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki. Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake. Ikawa Yesu alipokwisha kuwaagiza wanafunzi wake kumi na wawili, alitoka huko kwenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.

Neno La Mungu....... Sifa Kwako Ee Kristo.

Copyright © 2019: Shajara and Published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG

Tuesday, 9 July 2019

MASOMO YA MISA

MASOMO YA MISA, 
JUMANNE, JULAI 9, 2019
JUMA LA 14 LA MWAKA


SOMO 1
Mwa. 32:23-33

          Yakobo aliondoka usiku ule akawatwaa wakeze wawili, na vijakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja, akavuka kivuko cha Yaboki. Akawatwaa, akawavusha mto, akavusha na vyote alivyokuwa navyo.

Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri. Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusu panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye. Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki. Akamwuliza, Jina lako n’nani? Akasema, Yakobo. Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda. Yakobo akamwuliza, akasema, Niambie, tafadhali, jina lako? Akasema, Kwa nini waniuliza jina langu? Akambariki huko.

Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema, Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi vangu imeokoka. Jua likamzukia akivuka Penueli, akachechemea kwa sababu ya paja la mguu wake. Kwa hiyo wana wa Israeli hawali ule mshipa ulio katika uvungu wa paja hata leo; maana alimgusa Yakobo panapo uvungu wa paja katika mshipa wa kiuno.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 17 :1-3, 6-8, 15 (K) 15

(K) Nikutazame uso wako katika haki..

Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiyotoka katika midomo ya hila. (K) 

Hukumu yangu na itoke kwako,
Macho yako na yatazame mambo ya adili.
Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, 
Umenihakikisha usione neno;
Nimenuia kinywa changu kisikose. (K)

Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika,
Utege sikio lako ulisikie neno langu.
Dhihirisha fadhili zako za ajabu,
Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia;
Kwa mkono wako wa kuume 
Uwaokoe nao wanaowaondokea. (K )

Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako; 
mimi nikutazame uso wako katika haki,
Niamkapo nishibishwe kwa sura yako. (K)


SHANGILIO 
Yn. 10 : 27

Aleluya, aleluya, 
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, 
nami nawajua, nao wanifuata. 
Aleluya.


INJILI
Mt. 9: 32-39
      Walimletea Yesu mtu bubu mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wa kastaajabu, wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wo wote. Lakini Mafarisayo wakisema, Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo.

Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.

Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.

Neno la Bwana........Sifa kwako Ee Kristo

Copyright © 2019, Shajara and Published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG

Monday, 8 July 2019

NENO LA MUNGU 8/07/2019, JUMATATU YA 14 YA MWAKA 'C' WA KANISA.

Masomo ya Misa 08/07/2019


Somo la Kwanza
Mwa. 28:10-22
           Yakobo alitoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulanl akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamisha juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama. malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, Bwana amesimama juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli, Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni. Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake. Akaita jina la mahali pale Betheli; lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu. Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu. Na jiwe hili nililosimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.

Neno la Mungu;..... Tumshukuru Mungu.

Wimbo wa katikati
Zab 91:1-4, 14-15
Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu
Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu,
Mungu wangu nitakayemtumaini.
(K) Mungu wangu nitakayemtumaini. 

Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji,
Na katika tauni iharibuyo.
Kwa manyoya yake atakufunika,
Chini ya mbawa zake utapata kimbilio;
Uaminifu wake ni ngao na kigao.
(K) Mungu wangu nitakayemtumaini.

Kwa kuwa amekaza kunipenda
Nitamwokoa; na kumweka palipo juu,
Kwa kuwa amenijua jina langu.
Ataniita nami nilamwitikia;
NitaKuwa pamoja naye taabuni,
Nitamwokoa na kumtukuza.
(K) Mungu wangu nitakayemtumaini.

Shangilio
Lk.8:15
          Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao,  hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya.

Somo la Injili
Mt 9:18-26
            Yesu alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi. Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu, imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote.

Neno la Mungu;...... Sifa kwako Ee Kristo.

Copyright ©2019, Shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG,
See: imani-katoliki.blogspot.com

Saturday, 6 July 2019

NENO LA MUNGU 06/07/2019,. JUMAMOSI YA 13 MWAKA 'C' WA KANISA

Masomo ya Misa 06/07/2019

Somo la Kwanza
Mwa 27:1-5, 15-29
        Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia, Mwanangu. Nave akamwitikia, Mimi hapa. Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu. Basi, nakuomba, chukua mata yako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo; ukanifanyie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa. Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda nyikani awinde mawindo, ayalete. Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo yake. Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu na mkate alioufanya. Akaja kwa baba yake, akasema, Babangu. Akasema, Mimi hapa, U nani wewe, mwanangu? Yakobo akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama ulivyoniambia. Ondo- ka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako inibariki. Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii, mwanangu? Akasema, Kwa sababu Bwana, Mungu wako, amenifanikisha. Isaka akamwambia Yakobo, Karibu, tafadhali, ili nikupapase, mwanangu, nione kwamba wewe ndiwe mwanangu Esau, ama siyo. Basi Yakobo akamkaribia Isaka, babaye, naye akampapasa, akasema, Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau. Wala hakumtambua, kwa maana mikono yake ilikuwa kama mikono ya Esau, ndugu yake, yenye malaika; basi akambariki. Akamwuliza, Wewe ndiwe kweli mwanangu Esau? Akasema, Ndimi. Akasema, Niletee karibu nami nipate kula mawindo  ya mwanangu, ili roho yangu ikubariki. Akamsogeza karibu, naye akala; kisha akamletea mvinyo, akanywa. Isaka, baba yak, akamwambia, Njoo karibu sasa, ukanibusu, mwanangu. Akamkaribia akambusu. Naye akasikia harufu ya mavazi yake, akambariki akasema, Tazama, harufu ya mwanangu Ni kama harufu ya shamba alilolibariki Bwana. Mungu na akupe ya umande wa mbingu, Na ya manono ya nchi, Na wingi wa nafaka na mvinyo, Mataifa na wakutumikie Na makabila wakusujudie, Uwe bwana wa ndugu zako, na wana wa mama yako na wakusujudie, atakayekulaani alaaniwe, Na atakayekubariki abarikiwe.

Wimbo wa katikati
Zab 135:1-6
Aleluya.
Lisifuni jina la Bwana,
Enyi watumishi wa Bwana, sifuni.
Ninyi msimamao nyumbani mwa Bwana,
Nyuani mwa nyumba ya Mungu wetu.
(K) Msifuni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Msifuni Bwana kwa kuwa Bwana ni mwema.
Liimbieni jina lake kwa maana lapendeza.
Kwa sababu Bwana amejichagulia Yakobo,
Na Israeli, wawe watu wake hasa.
(K) Msifuni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Maana najua ya kuwa Bwana ni mkuu.
Na Bwana wetu yu juu ya miungu yote.
Bwana amefanya kila lililompendeza,
Katika mbingu na katika nchi,
Katika bahari na katika vilindi vyote.
(K) Msifuni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Shangilio
Mt 4:4
Aleluya, aleluya,
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Aleluya.

Somo la Injili
Mt 9:14-17
Wanafunzi wake Yohane walimwendea Yesu wakusema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda Bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga. Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huonndoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote.


MIITO SHARTI IHUBIRIWE

MIITO SHARTI IHUBIRIWE

Na Padri Innocent Bahati Mushi OFMCap.

Ni wazi kwamba familia, jumuiya na jamii nzima, inahusika sana kuipokea zawadi ya miito kwa kujijengea mazingira bora yanayovutia kwa wale walioitwa, kuitikia wito mtakatifu.

Mwitiko wa wito wa ndoa, upadre na maisha ya wakfu huzaa matunda pale ambapo mazingira yameandaliwa, kwenye udongo uliorutubishwa na Neno la Mungu, madhimisho ya kiliturujia, imani kwa Yesu Kristo, maadili mema na uadilifu, uchaji Mungu, moyo wa sadaka na majitoleo ya kila siku.

Kumbukeni kwamba maji hufuata mkondo au mfereji, tena udongo uliokulia huathiri sana namna yetu ya kuitikia wito au kuukata wito mtakatifu.

Kuandaa mazingira mazuri na malezi bora ni hatua za mwanzo katika kuitikia wito wowote. Maandalizi maridhawa ni pamoja na sala, mahubiri yanayobainisha umaana wa wito mtakatifu, faida na changamoto zake.

Mahali pengi ambapo miito ya ndoa, upadre na maisha ya wakfu imepungua, kuna uwezekano mkubwa kwamba kuna ukimya mkubwa kuhusu sala juu ya miito, na mafundisho juu ya miito yaliyoshehenishwa ushuhuda na uzuri wa maisha ya Jumuiya kwa wale waliokwishaingi katika maisha hayo.

Huenda sauti ya unabii imeshafifia mno na wanaoyaishi maisha yale hawatoi mwaliko wa furaha na matumaini kwa wale ambao wanawahudumia, katika hilo, jitihada inahitajika sana kufufua tena roho ya maisha ya kikristo.

Wanaohusika huenda wamekaa kimya au hawajali hali iliyopo kana kwamba kuna mambo mengine ya muhimu zaidi.

Miito iwe ni ya ndoa, utawa au upadre ni lazima ihubiriwe, isakwe na kuhamasishwa usiku na mchana, wakati ufaao na wakati usiofaa.

Hii ni changamoto kwa wale ambao wamepewa dhamana ya kuisakanya na kulea miito. Ni jukumu la wale wanaolea vyama vya kitume ambamo humo ni chimbuko la miito mingi.

Hatuwezi kusubiri kusema kwamba watakuja. Mtume Paulo anasema watakujaje wasipohubiriwa na kuhamasishwa?

Fr. Innocent Bahati Mushi OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208

Tuesday, 9 April 2019

UJUMBE WA KWARESMA 2019. Ter, 09/04/2019


TAFAKARI JUU YA UJUMBE WA KWARESMA 2019 TOKA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA

1.Utangulizi&Sura ya I
          Katika ujumbe wa mwaka huu Mababa Maaskofu wametoa mwaka huu kuwa ni mwaka wa familia. Ujumbe ukijikita katika 'FAMILIA NI KANISA LA NYUMBANI NA NI SHULE YA MAADILI'. Wanasisitiza juu ya kujifunza sala,  kuhimiza kupokea Sakramenti,  na kujifunza liturujia ni kazi ya wanafamilia kufunzana,  hasa wazazi wawafunze watoto. Lkn sio tu wazazi hata watoto kuwakumbusha wazazi kusali pamoja na hata kuwafunza sala kama wamesahau. Watoto wanatakiwa kuwaombea na wapige kelele juu ya wazazi wasiosali wala kujishughulisha na mambo ya kanisa.
        Maaskofu wanasisitiza juu ya utakatifu wa ndoa na maisha ya familia. Wazazi waheshimu ndoa zao na kurekebisha pale palipopotoka. Ili kulinda utakatifu wa ndoa wazazi waache kuendekeza michepuko,  mitara,  uzinzi ni vitu ambavyo vinaharibu utakatifu wa ndoa.
          Watoto wajisikie amani wakiwa nyumbani kama vile wanavyojisikia amani wawapo kanisani kwani hapo nyumbani ni kanisani pia. Akinamama  wapendeni waume zenu msiwafanye wakawa walevi kisa kukimbia manyanyaso ya familia na hata kuanzisha michepuko. Wanaume wajibikeni ktk familia zenu na sio kuwaachia majukumu ya familia akinamama.
        Tunapoendelea kutafakari juu ya ujumbe huu wa Kwaresma wa mwaka huu juu ya familia, siku hizi familia zetu zimegeuka kuwa makambi ya mateso,  jehanamu,  na hata jela ndogo inayotokana na ukosefu wa upendo na ukatili uliopitiliza.
         Katika Mwaka huu 2019 kunamatukio makuu manne kama ifuatavyo.
  1.1 Ni miaka 25 toka Sinodi ya kwanza ya Afrika iliyojikita katika kutafakari juu ya familia. Wanasisitiza kuwa kujenga familia imara ni kujenga jamii imara na kanisa imara. Tunawajibika kufundisha wanandoa juu ya majukumu yao ya malezi katika ngazi ya familia. Mfano akina baba wamewatulia majukumu ya malezi ya watoto akinamama na akinamama nao wamewatulia majukumu yao mahouse girls.
  1•2 Mwaka huu ni wa 25 toka UMOJA WA MATAIFA ulipotangaza kuwa mwaka 1994 kuwa ni mwaka wa familia. Ulisisitiza kuwa familia inaunda kitengo cha msingi cha jamii,  hivyo inatakiwa kuhakikishiwa ulinzi. Ni jukumu la viongozi wa serikali kuzihakikishia ulinzi familia. Viongozi wa serikali hasa watendaji katika tarafa,  miji,  vijijini na mitaa wanajukumu la kuibua matukio ya unyanyasaji ktk ngazi ya familia ambayo hufanyika kwa siri. Mfano kumeripotiwa watoto kufungiwa ndani kwa muda mrefu,  watoto kunyimwa chakula,  kubakwa,  kulawitiwa,  wazazi kuzaa na mabinti zao, akinamama kuwalaghai kimapenzi mahouse boys hali kadhalika akinababa na watoto wakiume kuwanyanyasa kingono mahousegirls,  ukeketaji..n.k Vitendo hivi vipo ni kazi ya wanahabari za uchunguzi kuibua kadhia hizi ktk familia zetu ambapo ni vitu vinavyoondoa utakatifu wa familia na maana ya kanisa na shule ya maadili.
 1.3 Mwaka huu pia ni jubilei ya miaka 50 tangu HALMASHAURI YA BARAZA LA WALEI kuanzishwa mwaka 1969. Ni ukweli usiopingika kwamba viongozi walei wa kanisa ktk maparokia mengi wamekuwa wakijitoa sana ktk kulihudumia kanisa. Viongozi hawa wapo tayari kutoa muda wao kuwahudumia mapadre,  kuwatafutia usafiri,  kuanzisha miradi ya parokia na kusimamia kanisa. Wapo wachache ambao kutokana na ufurufuru wa imaani wamekuwa miiba kwa maparoko na kanisa,  wamekuwa wapinga maendeleo ya kanisa,  wezi na wavurugaji wa imani, mwaka huu ukiwa wa uchaguzi,  viongozi kama hawa wawekwe pembeni wajifunze dini kwanza. Ni wajibu wa Maparoko kuwafanyia kitu fulani cha pekee ktk mwaka wao huu wa jubilei ikiwa ni kuwapongeza,  kuwafanyia sherehe, na mengine mengi kama kutambua kazi yao muhimu.
  1.4 Mwaka huu ni jubilei ya dhahabu ya miaka 50 tangu TYCS\YCS ianzishwe. Hawa ni vijana ambao bado wanakuwa chini ya wazazi au walezi. Inatakiwa kuwaandaa vizuri ili waje kuwa waumini wazuri baadae. Tukiwafundisha vzr vijana hawa tutaondoa tatizo la kuingia ktk ndoa bila sakramenti,  ubaridi wa kuchangamkia mambo ya kanisa,  kusali,  ambapo kwa sasa vijana wengi ni kama mtindo wao wa maisha. Mapadre hatuna budi kufanya makongamano ya kutosha kwa ajili yao kama vile Kongamano la Pasaka. Tuwalee vzr kwa kuwafundisha dini kwa usahihi. Kuwaongoza kumwelekea Yesu.
   ******Itaendelea*****
By; Fr. Kawonga
Holy Family Parish-Mkongo

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...