Na Padri Innocent Bahati Mushi OFMCap.
Ni wazi kwamba familia, jumuiya na jamii nzima, inahusika sana kuipokea zawadi ya miito kwa kujijengea mazingira bora yanayovutia kwa wale walioitwa, kuitikia wito mtakatifu.
Mwitiko wa wito wa ndoa, upadre na maisha ya wakfu huzaa matunda pale ambapo mazingira yameandaliwa, kwenye udongo uliorutubishwa na Neno la Mungu, madhimisho ya kiliturujia, imani kwa Yesu Kristo, maadili mema na uadilifu, uchaji Mungu, moyo wa sadaka na majitoleo ya kila siku.
Kumbukeni kwamba maji hufuata mkondo au mfereji, tena udongo uliokulia huathiri sana namna yetu ya kuitikia wito au kuukata wito mtakatifu.
Kuandaa mazingira mazuri na malezi bora ni hatua za mwanzo katika kuitikia wito wowote. Maandalizi maridhawa ni pamoja na sala, mahubiri yanayobainisha umaana wa wito mtakatifu, faida na changamoto zake.
Mahali pengi ambapo miito ya ndoa, upadre na maisha ya wakfu imepungua, kuna uwezekano mkubwa kwamba kuna ukimya mkubwa kuhusu sala juu ya miito, na mafundisho juu ya miito yaliyoshehenishwa ushuhuda na uzuri wa maisha ya Jumuiya kwa wale waliokwishaingi katika maisha hayo.
Huenda sauti ya unabii imeshafifia mno na wanaoyaishi maisha yale hawatoi mwaliko wa furaha na matumaini kwa wale ambao wanawahudumia, katika hilo, jitihada inahitajika sana kufufua tena roho ya maisha ya kikristo.
Wanaohusika huenda wamekaa kimya au hawajali hali iliyopo kana kwamba kuna mambo mengine ya muhimu zaidi.
Miito iwe ni ya ndoa, utawa au upadre ni lazima ihubiriwe, isakwe na kuhamasishwa usiku na mchana, wakati ufaao na wakati usiofaa.
Hii ni changamoto kwa wale ambao wamepewa dhamana ya kuisakanya na kulea miito. Ni jukumu la wale wanaolea vyama vya kitume ambamo humo ni chimbuko la miito mingi.
Hatuwezi kusubiri kusema kwamba watakuja. Mtume Paulo anasema watakujaje wasipohubiriwa na kuhamasishwa?
Fr. Innocent Bahati Mushi OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208
No comments:
Post a Comment
"Asante sana kwa maoni yako"