Friday, 12 May 2017

BWANA, NATAMANI DAIMA KUWA NAWE.

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU.
Ijumaa, Mei 12, 2017,
Juma la 4 la Pasaka


Mdo 13: 26-33;
Zab 2: 6-11;
Yn 14: 1-6.


MBINGUNI NI NYUMBANI KWETU!

          Mara kwa mara ni muhimu kuweka jitihada kuelekea kwenye utukufu wa Mbinguni! Mbingu ipo na ni mapenzi ya Mungu sisi wote siku moja tufurahi na Utatu Mungu mmoja. Kama tunatambua kwa hakika kuhusu mbingu, tunakuwa tunaitamani kwa moyo wote na tunawaka mapendo na kuitazamia kwa nguvu kubwa, tukiwa tumejazwa na Amani na furaha kila wakati tuki ifikirie. Kwa bahati mbaya, habari za kuacha ulimwengun huu na kwenda kukutana na Muumba wetu kwa wengi zina ogopesha. Pengine ni hofu ya mambo yasio julikana, utambuzi wa kwamba tutawaacha wapendwa wetu, au hofu ya kwamba huenda tusiende mbinguni.

     Kama Wakristo, ni vizuri kujishughulisha tukitambua upendo wetu mkubwa mbinguni kwa kupata utambuzi mkubwa wa sio mbinguni pekee, bali kutambua jukumu la maisha yetu hapa duniani. Mbingu inasaidia sisi tuweze kupanga maisha yetu kwa kupitia ile njia inayo tuongoza kwenye heri hiyo. Katika Injili, tunapewa picha  zuri sana yenye kufariji kuhusu Mbinguni, ambayo ni “Nyumba ya Baba”. Nyumbani ni sehemu salama. Ni sehemu ambayo tunaweza kufurahia na kuishi bila kujifanya, kuwa na wapendwa wetu, kupumzika, na kujisikia ni sehemu ya familia. Sisi ni watoto wa Mungu na hivyo Mungu anapenda sisi tuwe nyumbani pamoja naye.

         Kwa kutafakari juu ya picha hii, inapaswa pia iwe faraja kwa wale wote waliopoteza wapendwa wao. Hali ya kusema kwaheri, ni ngumu. Na inapaswa kuwa ngumu. Ugumu wa kupoteza wapendwa wetu inaonesha uwepo wa upendo wa kweli katika mahusiano. Lakini Mungu anapenda hali ya hisia za kupoteza wapendwa wetu ichanganyike na furaha tunapo tafakari ukweli wa wapendwa wetu kuwa wapo na Baba nyumbani milele. Wana furaha kule zaidi ya jinsi tunavyo weza kudhania, na siku moja nasi tutaitwa kushiriki furaha hiyo.

      Sala: Bwana, natamani daima kuwa nawe. Nisaidie daima niweke lengo hili daima akilini mwangu, na kukuwa nalo siku zote kwa tamaa ya kufurahi nawe milele. Yesu, nakuamini wewe. Amina.


    Copyright: © 2016-2017   shajara and published. by MAMBO YAHUSUYO IMANI  BLOG

Thursday, 11 May 2017

NENO LA MUNGU, 12/05/2017.

MASOMO YA MISA, MEI 12, 2017
IJUMAA, JUMA LA 4 LA PASAKA



SOMO 1
Mdo. 13:26-33

     Paulo alisimama akawapungia mkono, akasema: Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa. Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu. Na ijapokuwa hawakuona sababu ya kumfisha wakamwomba Pilato auawe.     Hata walipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamtelemsha katika ule mti, wakamweka kaburini. Lakini Mungu akamfufua katika wafu; akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hata Yerusalemu, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu.
      Na sisi tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliyopewa mababa, ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 2:6-11 (K) 7

(K) Ndiwe Mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.
Au: Aleluya.

   (1). Nami nimemweka mfalme wangu
Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.
Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia,
Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. (K)

    (2). Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako,
Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
Utawaponda kwa fimbo ya chuma,
Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. (K)

    (3). Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili,
Enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe.
Mtumikieni Bwana kwa kicho,
Shangilieni kwa kutetemeka. (K)


SHANGILIO
Yn. 20: 29

     Aleluya, aleluya,
Wewe Toma, umesadiki kwa kuwa umeniona, wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Aleluya.


INJILI
Yn. 14:1-6

      Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yngu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia, maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia.
   Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?
Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.



Copyright © 2017 shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG 

Wednesday, 10 May 2017

MASOMO YA MISA, MEI 10, 2017
JUMATANO,JUMA LA 4 LA PASAKA


SOMO 1
Mdo. 12:24-13:5

    Siku zile, Neno la Bwana likazidi na kuenea. Na Barnaba na Sauli, walipokwisha kutimiza huduma yao, wakarejea kutoka Yerusalemu, wakamchukua pamoja nao Yohane aitwaye Marko.
Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.
    Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro. Na walipokuwa katika Salami waklihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi.


Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI

Zab. 67:1-2, 4, 5, 7 (K) 3

(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, Watu wote na wakushukuru.
Au Aleluya.

Mungu na atufadhili na kutubariki,
Na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulikane duniani,
Wokovu wake katikati ya mataifa yote. (K)

Mataifa na washangilie,
Naam, waimbe kwa furaha,
Maana kwa haki utawahukumu watu,
Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)

Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
Mungu atatubariki sisi;
Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)


SHANGILIO
Yn. 10:14

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema,
Nao walio wangu nawajua, nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.



INJILI
Yn. 12:44-50

     Siku ile Yesu alipaza sauti, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka. 
  Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. Yeyey anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumu siku ya mwisho.          Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. 
  Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.


Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.



    Copyright : ©2017  by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG.

Saturday, 7 January 2017

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU, Sherehe ya Tokeo la Bwana (Epifania)


Januari 8, 2017. 

Sherehe ya Tokeo la Bwana (Epifania)

Isa 60: 1-6; 
Zab 72: 1-2, 7-8, 10-13; 
Efe 3: 2-3, 5-6; 
Mt 2: 1-12.


ZAWADI KWA DUNIA NZIMA!

         Katika somo la kwanza, katika ono lake la kinabii, Isaya anaona ujio wa Mungu ulimwenguni. Utakuja muda ambapo watu wote wataletwa pamoja mbele ya Bwana na watabarikiwa sana. Utukufu wa Bwana utashuka ulimwenguni na utukufu wake utauzunguka uumbaji wote.
Tukio hili takatifu litalibadilisha jiji la Yerusalemu na wale wote wanaofanya kazi na kuvumilia watapokea mwanga wa uhai. 
Katika somo la pili, Paulo anaifumbua siri ambayo Mungu anaitoa kwa utukufu wake watu wote pamoja na wapagani, kuwafanya warithi wa ufalme wake. Anasema “sasa imefunguliwa kuwa wapagani wanashiriki urithi ule ule”. Ukombozi wa ulimwengu, Mungu pia anawapenda wasio Wakristo kwani wao pia ni wapokeaji.  
Leo tunasherehekea sherehe ya Tokeo la Bwana. Ni sherehe ya dhihirisho la Bwana wetu kwa watu wa Mataifa. Kulikuwa na mamajusi watatu kutoka mashariki waliokuja kwa Mfalme mpya aliyezaliwa. Mamajusi hawa, watu wa mataifa, ambao hawakuwa katika utajiri wa pamoja wa Waisraeli, walikuwa ni watu waliosoma nyota kwa lengo la kubaini siri na ujumbe wake. Walipokuja katika mahakama ya mfalme, walimuuliza Herode, yuko wapi mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa? Hawakuuliza kama mfalme wa wayahudi amezaliwa? Walikuwa na uhakika kuwa mfalme alikuwa amekwisha zaliwa. Walikuwa tu hawana uhakika wa sehemu yake alipozaliwa, bali juu ya ukweli kwamba amezaliwa walikuwa nao.  
Kama tu vile Yeye alivyo jidhihirisha Yeye Mwenyewe kwa wale mamajusi, kila siku Mungu anajidhihirisha mwenyewe kwetu sisi katika Ekaristi Takatifu. Tunamtukuza Yeye, tunamshukuru na kumfanya yeye afahamike ulimwenguni kote. Basi tujitoe sisi wenyewe kama zawadi na tuunganike naye na  kuhubiri:Mungu amejidhihirisha mwenyewe duniani. Yesu anajitoa mwenyewe zawadi kwa dunia nzima.

Sala: Bwana, niwezeshe niweze kujitoa Mimi mwenyewe kama zawadi kwako. Amina..

MASOMO YA MISA JANUARI 8, 2017SHEREHE YA EPIFANIA


MASOMO YA MISA JANUARI 8, 2017

SHEREHE YA EPIFANIA


SOMO 1
Isa. 60:1-6
       Ondoka, ee Yerusalemu, uangaze; Kwa kuwa nuru yako imekuja. Na utukufu wa Bwana umekuzukia. Maana, tazama, giza litaifunika dunia, Na giza kuu litazifunika kabila za watu; Bali Bwana atakuzukia wewe, Na utukufu wake utaonekana juu yako. Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako. Inua macho yako, utazame pande zote; Wote wanakusanyana; wanakujia wewe; Wana wako watakuja kutoka mbali, Na binti zako watabebwa nyongani. Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa utakuwasilia. Wingi wa ngamia utakufunika, Ngamia vijana wa Midiani na Efa; Wote watakuja kutoka Sheba; Wataleta dhahabu na uvumba; Na kuzitangaza sifa za Bwana.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 72:1-2, 7-8, 10-13 (K) 11
(K) Mataifa yote ya ulimwengu, watakusujudia, ee Bwana.
       (1).   Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako.
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)
       (2).   Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa Amani hata mwezi utakapokoma
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka mto hata miisho ya dunia. (K)
      (3).   Wafalme wa Tarshisi na visiwa walete kodi,
Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.
Naam, wafalme wote na wamsujudie;
Na mataifa yote wamtumikie. (K)
     (4).   Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)


SOMO 2
Efe. 3:2-3, 5-6
Ndugu zangu: Ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo.
Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO
Mt. 2:2
Aleluya, aleluya,
Tuliona nyota yake mashariki, Nasi tumekuja kumsujudia.
Aleluya.


INJILI
Mt. 2:1-12
Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, ansi tumekuja kumsujudia. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao: Kristo azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika Bethlemu ya Uyahudi; kwa maana ndiyvo ilivyoandikwa na nabii, Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda, Kwa kuwa kwako atatoka mtawala atakayewachunga watu wangu Israeli.
Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota, Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie. Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, hata ikaenda ikasimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...