MASOMO YA MISA, MEI 10, 2017
JUMATANO,JUMA LA 4 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 12:24-13:5
Siku zile, Neno la Bwana likazidi na kuenea. Na Barnaba na Sauli, walipokwisha kutimiza huduma yao, wakarejea kutoka Yerusalemu, wakamchukua pamoja nao Yohane aitwaye Marko.
Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.
Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro. Na walipokuwa katika Salami waklihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 67:1-2, 4, 5, 7 (K) 3
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, Watu wote na wakushukuru.
Au Aleluya.
Mungu na atufadhili na kutubariki,
Na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulikane duniani,
Wokovu wake katikati ya mataifa yote. (K)
Mataifa na washangilie,
Naam, waimbe kwa furaha,
Maana kwa haki utawahukumu watu,
Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)
Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
Mungu atatubariki sisi;
Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)
SHANGILIO
Yn. 10:14
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema,
Nao walio wangu nawajua, nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.
INJILI
Yn. 12:44-50
Siku ile Yesu alipaza sauti, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka.
Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. Yeyey anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumu siku ya mwisho. Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema.
Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright : ©2017 by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG.
No comments:
Post a Comment
"Asante sana kwa maoni yako"