Thursday, 17 November 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 33 YA MWAKA-C



ALHAMISI WIKI YA 33 YA MWAKA-C

             Somo: Ufu 5:1-10
                      Zab/kit: 149:1-2, 3-4, 5-6a, 9b
               Injili: Lk 19:41-44
  
             Nukuu:
“Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba,” Ufu 5:1
                        “Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba,” Ufu 5:5
                        “akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako,” Lk 19:42
                       “watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako,” Lk 19:44
         TAFAKARI:
                     “Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.”
                 Wapendwa wana wa Mungu, bila shaka jamii yetu leo imehathirika na ugonjwa huu wa “UDHAHAMO,” Upungufu wa Dhamira Hai Moyoni.
Iweje leo unaona binadamu mwenzako anauwawa kikatili nawe waona jambo hili ni sawa na halisemi kitu chochote ndani ya nafsi yako? Inaingiaje akili leo kwa mkono wako unamwua binadamu mwenzako kikatili na bado unajiona upo sawa? Unajionaje upo sawa pale unapotoa ushauri juu ya kumdhuru mwenzako na hata kupoteza uhai wake? Wengi husema mtu fulani kauliwa kinyama. Mnyama hawezi kumwua mnyama mwenzake wa familia ile ile kikatili hivyo.
Huwezi kuona Simba akimwua simba mwenzake kikatili kama anavyofanya binadamu kwa binadamu mwenzake. Tuyaonayo kwa wanadamu leo ni ugonjwa wa UDHAHAMO. Binadamu aliyekufa dhamiri ni sawa na Gari jipya lisilokuwa na breki.
Hata kama dereva wake kafuzu vizuri katika fani ya udereva lolote laweza kutokea njiani na kuwashangaza wengi.
Mshango kama huo unamkuta Yesu anapoutazama mji wa Yerusalemu na wakazi wake na uzuri wa Hekalu. Kipindi cha Yesu, Wayahudi wengi hawakuwa wanaishi yale yaliyokuwa yanampendeza Mungu. Torati haikufuatwa kama ilivyo, bali walifuata tafsiri ya Torati na masimulizi ya wazee, TALMUD, ambao ulikuwa ukweli wa Mungu ulipotoshwa. Yesu alijua mwisho wa kila kitu kuhusu mji huu wa Yerusalema na fahari yake. Aliutazama, “akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako,” Lk 19:42.
Salama ya mji huu wa Yerusalemu ilikuwa ni kupatanishwa na Mungu kwa kuyaacha matendo yao mabaya na kumrudia Mungu. Hekalu lenyewe lilikuwa kituo cha biashara. “Akaingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi,” Lk 19:45-46.
          Michanganyo katika Imani ni hatari sana. Hata Yesu hakupenda michanganyo hiyo. Ni jukumu na wajibu wako na wangu kuishi imani ya kweli, na yeye kuenenda na matendo. Na kadiri tuishivyo ndivyo hivyo hivyo tunavyojiandalia hukumu yetu ya mwisho.
Na siku hiyo ya mwisho kitakacho tokea ni hakikisho tu juu ya yale yote tuliyoyaishi hapa duniani.
Hakikisho hili ndilo litakalo amua uwe upande upi wa Mwana-Kondoo. Kristo Yesu ndiye atakaye kuwa hakimu wetu wa haki na kweli.
Hali na mazingira hayo juu ya siku ile ya mwisho ndiyo anayotusimulia Yohana katika maono yake, nakusema, “Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba,” Ufu 5:1.
            Aliye keti juu ya kiti cha enzi ni Mungu mwenyewe. Simba wa Yuda, na Shina la Daudi, ambaye ndiye mwana wa Adamu, ndiye mwenye kukifungua kitabu kile ikiwa ni pamoja na mihuri yake saba, kama alama ya ukamilifu. Huyu ndiye mwenye kuisoma hukumu ya haki na kweli. Hapata kuwa na uonevu wowote, kwani epuko la kutokuingia hatia ni idadi ya miaka uliyopewa kuishi hapa duniani.
         Kila siku ni mwaliko kwako na kwangu kuanza maisha mapya na yenye kumpendeza Mungu. Na hali itakuwa hivi, “Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba,” Ufu 5:5. Huyu ndiye Mwana-Kondoo wa Mungu.
Hukumu hii itashuhudiwa na walio safi, na waliohesabiwa haki tayari, yaani, malaika na wateule wa Mungu, Watakatifu.
Naye Yohana anasema, “Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote,” Ufu 5:6.
         Yesu Kristo, Mwana-Kondoo, ndiye atakaye kitwa “kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi,” Ufu 5:7. 
Kwa vile hakutakuwa na utetezi zaidi ya hakikisho kwa yale uliyotenda, zoezi hili litasindikizwa na burudani. Kwa walio haki baada ya hakikisho hilo watafurahia milele, na wasio haki baada ya hakikisho hilo itakuwa huzuni yao milele. Huzuni hii ni kiu au tamanio la kile ukipendacho lakini hutokuwa na uwezo wa kikipata katika umilele wake.
     Na hali itakuwa hivi juu ya burudani hiyo; na “Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wane wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu,” Ufu 5:8. 
Hakika ni furaha na masikitiko! Furaha kwa wenye haki, na masikitiko kwa wasio haki. Na ujumbe wa wimbo huo mpya usindikizao hukumu hiyo ni huu; “Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi,” Ufu 5:9-10. Wimbo huu umebeba wasifu wa Mwana-Kondoo, Yesu Kristo, na hasa ukitukumbusha thamani ya sadaka yake aliyoitoa kwa ajili yako na yangu pale Msalabani.
Ndugu yangu, wimbo huu uziamshe dhamiri zetu zilizolala au kufa. Amina!
           
          Tumsifu Yesu Kristo!
           
            “watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako,” Lk 19:44

           Tusali:-Ee Yesu, yaongoze maisha yetu katika dhamiri njema kila siku. Amina

Copyright ©2016 by Fr Tanga Ngowi, OSA.  and  published  by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
     see:  imani-katoliki.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

"Asante sana kwa maoni yako"

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...