Thursday, 17 November 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 33 YA MWAKA-C



ALHAMISI WIKI YA 33 YA MWAKA-C

             Somo: Ufu 5:1-10
                      Zab/kit: 149:1-2, 3-4, 5-6a, 9b
               Injili: Lk 19:41-44
  
             Nukuu:
“Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba,” Ufu 5:1
                        “Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba,” Ufu 5:5
                        “akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako,” Lk 19:42
                       “watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako,” Lk 19:44
         TAFAKARI:
                     “Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.”
                 Wapendwa wana wa Mungu, bila shaka jamii yetu leo imehathirika na ugonjwa huu wa “UDHAHAMO,” Upungufu wa Dhamira Hai Moyoni.
Iweje leo unaona binadamu mwenzako anauwawa kikatili nawe waona jambo hili ni sawa na halisemi kitu chochote ndani ya nafsi yako? Inaingiaje akili leo kwa mkono wako unamwua binadamu mwenzako kikatili na bado unajiona upo sawa? Unajionaje upo sawa pale unapotoa ushauri juu ya kumdhuru mwenzako na hata kupoteza uhai wake? Wengi husema mtu fulani kauliwa kinyama. Mnyama hawezi kumwua mnyama mwenzake wa familia ile ile kikatili hivyo.
Huwezi kuona Simba akimwua simba mwenzake kikatili kama anavyofanya binadamu kwa binadamu mwenzake. Tuyaonayo kwa wanadamu leo ni ugonjwa wa UDHAHAMO. Binadamu aliyekufa dhamiri ni sawa na Gari jipya lisilokuwa na breki.
Hata kama dereva wake kafuzu vizuri katika fani ya udereva lolote laweza kutokea njiani na kuwashangaza wengi.
Mshango kama huo unamkuta Yesu anapoutazama mji wa Yerusalemu na wakazi wake na uzuri wa Hekalu. Kipindi cha Yesu, Wayahudi wengi hawakuwa wanaishi yale yaliyokuwa yanampendeza Mungu. Torati haikufuatwa kama ilivyo, bali walifuata tafsiri ya Torati na masimulizi ya wazee, TALMUD, ambao ulikuwa ukweli wa Mungu ulipotoshwa. Yesu alijua mwisho wa kila kitu kuhusu mji huu wa Yerusalema na fahari yake. Aliutazama, “akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako,” Lk 19:42.
Salama ya mji huu wa Yerusalemu ilikuwa ni kupatanishwa na Mungu kwa kuyaacha matendo yao mabaya na kumrudia Mungu. Hekalu lenyewe lilikuwa kituo cha biashara. “Akaingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi,” Lk 19:45-46.
          Michanganyo katika Imani ni hatari sana. Hata Yesu hakupenda michanganyo hiyo. Ni jukumu na wajibu wako na wangu kuishi imani ya kweli, na yeye kuenenda na matendo. Na kadiri tuishivyo ndivyo hivyo hivyo tunavyojiandalia hukumu yetu ya mwisho.
Na siku hiyo ya mwisho kitakacho tokea ni hakikisho tu juu ya yale yote tuliyoyaishi hapa duniani.
Hakikisho hili ndilo litakalo amua uwe upande upi wa Mwana-Kondoo. Kristo Yesu ndiye atakaye kuwa hakimu wetu wa haki na kweli.
Hali na mazingira hayo juu ya siku ile ya mwisho ndiyo anayotusimulia Yohana katika maono yake, nakusema, “Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba,” Ufu 5:1.
            Aliye keti juu ya kiti cha enzi ni Mungu mwenyewe. Simba wa Yuda, na Shina la Daudi, ambaye ndiye mwana wa Adamu, ndiye mwenye kukifungua kitabu kile ikiwa ni pamoja na mihuri yake saba, kama alama ya ukamilifu. Huyu ndiye mwenye kuisoma hukumu ya haki na kweli. Hapata kuwa na uonevu wowote, kwani epuko la kutokuingia hatia ni idadi ya miaka uliyopewa kuishi hapa duniani.
         Kila siku ni mwaliko kwako na kwangu kuanza maisha mapya na yenye kumpendeza Mungu. Na hali itakuwa hivi, “Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba,” Ufu 5:5. Huyu ndiye Mwana-Kondoo wa Mungu.
Hukumu hii itashuhudiwa na walio safi, na waliohesabiwa haki tayari, yaani, malaika na wateule wa Mungu, Watakatifu.
Naye Yohana anasema, “Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote,” Ufu 5:6.
         Yesu Kristo, Mwana-Kondoo, ndiye atakaye kitwa “kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi,” Ufu 5:7. 
Kwa vile hakutakuwa na utetezi zaidi ya hakikisho kwa yale uliyotenda, zoezi hili litasindikizwa na burudani. Kwa walio haki baada ya hakikisho hilo watafurahia milele, na wasio haki baada ya hakikisho hilo itakuwa huzuni yao milele. Huzuni hii ni kiu au tamanio la kile ukipendacho lakini hutokuwa na uwezo wa kikipata katika umilele wake.
     Na hali itakuwa hivi juu ya burudani hiyo; na “Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wane wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu,” Ufu 5:8. 
Hakika ni furaha na masikitiko! Furaha kwa wenye haki, na masikitiko kwa wasio haki. Na ujumbe wa wimbo huo mpya usindikizao hukumu hiyo ni huu; “Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi,” Ufu 5:9-10. Wimbo huu umebeba wasifu wa Mwana-Kondoo, Yesu Kristo, na hasa ukitukumbusha thamani ya sadaka yake aliyoitoa kwa ajili yako na yangu pale Msalabani.
Ndugu yangu, wimbo huu uziamshe dhamiri zetu zilizolala au kufa. Amina!
           
          Tumsifu Yesu Kristo!
           
            “watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako,” Lk 19:44

           Tusali:-Ee Yesu, yaongoze maisha yetu katika dhamiri njema kila siku. Amina

Copyright ©2016 by Fr Tanga Ngowi, OSA.  and  published  by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
     see:  imani-katoliki.blogspot.com

MASOMO YA MISA, 17/11/2016 Alhamisi ya 33 ya Mwaka - C


Mt. Elizabeth wa Hungaria

        SOMO LA 1
                  Ufu 5:1-10

              Mimi Yohane niliona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba. Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, N'nani astahiliye kukifungua kitabu, na kuzivunja muhuri zake? Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama.
Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba. Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote. Akaja, akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi. Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu. Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.

Neno la Bwana ...... Tumshukuru Mungu.

           WIMBO WA KATIKATI
               Zab 149:1-6, 9

           (1).    Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Sifa zake katika kusanyiko la watauwa. Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya, Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
                    (K) Ulitufanya kuwa wafalme na makuhani
          (2).    Na walisifu jina lake kwa kucheza, Kwa matari na kinubi wamwimbie. Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake, Huwapamba wenye upole kwa wokovu.
                    (K) Ulitufanya kuwa wafalme na makuhani
         (3).   Watauwa na waushangilie utukufu, Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao. Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao, Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote. Aleluya.
                     (K) Ulitufanya kuwa wafalme na makuhani

       SOMO LA INJILI
            Lk 19:41-44

                  Yesu alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.
Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.

Neno la Bwana ......  Sofa kwako Ee Kristu.

Copyright ©2016  by  shajara  and  published  by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
     see: imani-katoliki.blogspot.com

Wednesday, 16 November 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 33 YA MWAKA-C

    
    JUMATANO WIKI YA 33 YA MWAKA-C

        Somo: Ufu 4:1-11
                  Zab/kit: 151:1-2, 3-4, 5-6
           Injili: Lk 19:11-28

             Nukuu: “Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti,” Ufu 4:3
                “Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu,” Ufu 4:4
              “Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye,” Ufu 4:7
             “Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi,” Lk 19:17
               “Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho,” Lk 19:26

         TAFAKARI:
                              “Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho.”
                 Wapendwa wana wa Mungu, kila mmoja wetu kapewa uwezo wa kupambana na mazingira yoyote yale atakayokutana nayo. Uwezo huu siyo wa kuufungia sehemu fulani na kutokufanya chochote.
Na kadiri tutumiavyo uwezo na maarifa hayo ndivyo Mungu anavyozidi kutukirimia kadiri ya hitaji letu na wenzetu. Na ikiwa maisha yetu hapa duniani ni jukumu la muda mfupi, safari yetu kuelekea uzima wa milele ni pamoja na kutumia vyema karama na vipaji aliyotujalia Mungu kama sehemu ya maandalizi hayo. Injili ya leo inafafanua jambo hili kwa mifano ya watu waliopewa fedha za biashara na mtu mmoja Kabaila. Aliyepewa kumi alizalisha nyingine kumi, aliyepewa tano alizalisha nyingine tano, na aliyepewa moja hakufanya chochote zaidi ya kulalamika. Naye alipotakiwa kutoa hesabu yake alijibu kwa jeuri, “Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda,” Lk 19:21.
           Mara nyingi huwa tunajihukumu wenyewe kwa kutokuviendeleza vipaji alivyotupa Mungu na kubaki kutamani vipaji vya wengine. Wapo pia wengine kati yetu ambao muda wao wote katika maisha ni kuyatafuta yale ambayo yapo nje ya uwezo wao, na mwisho wa siku wanabaki kuwa vivuli vya wengine na kukosa furaha ya kweli ndani yao. Kumbe leo Kristo anatuambia tuthamini aliyotupatia Mungu, na tuyaendeleze kwa sababu, “Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho,” Lk 19:26.
Usipo kithamini ulicho nacho na kukiendeleza kitachukuliwa na kupewa mwingine. Kwa maneno mengine, wewe mwenyewe wakati mwingine ni sababu tosha ya kuyadumaza yale aliyokujalia Mungu kwa kutojishughulisha.
Hatua ya kwanza ya kuthamini kile ulichonacho huanza kwa wewe mwenyewe kuwa mwaminifu kwa yale madogo madogo ya kila siku na hasa kwa yale tunayopewa dhamana. Watumwa wale waliofanya vizuri walipewa hakikisho la utendaji wao. “Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi,” Lk 19:17.
Je, wajua vipaji vyako na uwezo wako? Tunzo ya kuvitumia vipaji na karama zetu vyema, kwa ajili yetu na wengine, ni ezekano lile la kuhesabiwa haki na kuurithi ufalme wa mbinguni.
Hivyo somo letu la kwanza leo linaelezea manndari hiyo ya Mbinguni. Kwanza huko mbinguni uishi Mungu aliye Mtakatifu na ndiyo makazi yake ya milele.
Yohana katika maono yake anatuambia kile alichokiona: “Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti,” Ufu 4:3.
Kiti hiki cha Mungu ni ishara wazi ya ukamilifu wake. Na ishara hii ya ukamilifu imejifunua kwa uwepo wa taa saba za moto zikiwaka. “Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zilikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu,” Ufu 4:5.
Mungu wetu ni hai, tena ni mwanzo na mwisho-ALFA NA OMEGA.
           Kundi la pili ni wateule wake Mungu, yaani, watakatifu. Nao hawa wanawakilishwa kwa viti vile ishirini na vinne.
Idadi hii ya vitu yamaanisha idadi ya kutosha, na iliyo kamili. Hawa wateule wa Mungu ukizunguka kiti kile cha enzi cha Mungu. “Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu,” Ufu 4:4.
Mavazi yao maupe ni alama uthibitisho tosha wa utakaso na Utakatifu wao. Wateule hawa wa Mungu wanayo kazi moja tu huko mbinguni. Kazi hiyo ni kumsujudu yule aliye hai hata milele na milele. Na “ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema,” Ufu 4:10.
Kusujudu huku ndiko kujisalimisha pasipo kujibakiza, na ndiyo maana halisi ya kuabudu. Ni kuunganishwa na furaha ile ya Mungu na utukufu wake milele yote. “Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele,” Ufu 4:9 Kundi lingine la tatu huko mbingini ni kundi la Malaika wa Mungu.
         Hawa ndio wale walindao malango yale pande zote nne za Utukufu huo huko mbinguni. Malaika hawa hujulikana kwa kazi na muono wao kama anavyosimulia Yohana. “Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye,” Ufu 4:7. Nao hawa Malaika kazi yao kubwa licha ya ulizi, humzunguka Mungu na kuimba ‘Mtakatifu’ pasipo ukomo. “Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja,” Ufu 4:8.
Je, kuna kwaya gani na yenye uwezo hapa duniani kama hii ya kundi hili la malaika? Leo tuolio na vipaji vya kuimba wakati mwingine twa jaa kiburi kwa vile bado hatujajua ni nani tunayemwimbia. Hakika, sifa na shukrani ni kwa Mungu tu.
Na zoezi hilo la kumpa Mungu sifa na shukrani linaanza hapa hapa duniani kwa kutoa kile ulicho nacho kwa moyo mkunyufu na usio jibakiza. Hivi ndivyo vile vipaji ulivyo jaliwa na Mungu kwa ajili yako na wengine. Hizi ndizo karama zile Mungu alizokujalia bila mastahili yako. Na huu ndio ule utajiri aliokuazimisha Mungu kwa wakati tu ungali hapa duniani.
Na unafanya yote hayo kwa sifa na Ufalme wake Mungu ukijua wazi anayestahili hayo yote ni Mungu peke yake kwa kuwajali jirani zetu, na wale wote wenye uhitaji. Hakika, “umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa,” Ufu 4:11.
Ni Mungu peke yake apaswa kuabudiwa na kutukuzwa milele. Amina Tumsifu Yesu Kristo! “Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele,” Ufu 4:9

         Tusali:-Ee Mungu, tujalie neema na nguvu tukusifu milele yote. Amina

Copyright ©2016 by Fr Tanga  Ngowi and  published  by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
    see:  imani-katoliki.blogspot.com

MASOMO YA MISA, 16/11/2016 Jumatano ya 33 ya Mwaka.


Jumatano ya 33 ya Mwaka

               SOMO LA 1
          Ufu 4:1-11

                Mimi Yohane, niliona mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo. Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti; na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi. Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu. Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zilikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu.
Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma. Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye. Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja.
Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele, ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema, Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.

Neno la Bwana .......  Tumshukuru Bwana.

   WIMBO WA KATIKATI
            Zab 150

          (1).  Msifuni Mungu katika patakatifu pake; Msifuni katika anga la uweza wake. Msifuni kwa matendo yake makuu; Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.
                      (K) Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa Mwenyezi
          (2).  Msifuni kwa mvumo wa baragumu; Msifuni kwa kinanda na kinubi; Msifuni kwa matari na kucheza; Msifuni kwa zeze na filimbi;
                      (K) Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa Mwenyezi
          (3).    Msifuni kwa matoazi yaliayo; Msifuni kwa matoazi yavumayo sana. Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana. Aleluya.
                     (K) Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa Mwenyezi
 
         SHANGILIO
                    Yn. 8:12

              Aleluya, aleluya, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima. Aleluya.

        SOMO LA INJILI
              Lk 19:11-28

                Makutano waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara. Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi. Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja.
Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.
Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.
Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi. Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi. Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.
Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano. Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso. Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda. Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi. Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.
Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho. Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu. Na alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu.

Neno la Bwana ..... Sifa kwako Ee Kristu.

Copyright ©2016  shajara  and  published  by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
    see: imani-katoliki.blogspot.com

Tuesday, 15 November 2016

TAFAKARI 15/11/2016 Juma la 33 la Mwaka - C wa Kanisa. " Furaha ya upendo wa Yesu "


TAFAKARI

       Jumanne, Novemba 15, 2016, Juma la 33 la Mwaka wa Kanisa

      Ufu 3:1-6, 14-22;
           Zab 14:2-5,
                Lk 19:1-10

     FURAHA YA UPENDO WA YESU
              Ni kitu ghani kilichomfanya Zakayo akafungua moyo wake, katika Injili ya leo? Ni furaha ya upendo wa Yesu.
Watu walimchukia Zakayo sana na kadiri walivyo mchukia ndivyo alivyo jitenga mbali nao. Yesu anaingia katika nyumba ya Zakayo na tazama mtu aliyekuwa na moyo mgumu, unayeyuka nakuanza kuahidi maisha ya fadhila ya baadae.
Je, ni kitu ghani utafanya Yesu akija kugonga katika moyo wako leo nakusema “nataka kukaa katika nyumba yako leo?” je utafurahi au utakuwa na mashaka na kudhani utadhalilika? Bwana yupo tayari daima kufanya maskani yake ndani mwetu. Je, unampa nafasi katika moyo wako na nyumbani mwako?

       Sala: Jaza nyumbani mwangu kwa uwepo wako Ee Bwana, nisaidie niweze kuonesha ukarimu na huruma kwa wote, hata kwa wale walioniumiza. Amina

Copyright ©2016 by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
   see: imani-katoliki.blogspot.com

MASOMO YA MISA, 15/11/2016 Jumanne ya 33 ya Mwaka - C wa kanisa


Jumanne ya 33 ya Mwaka
 
           SOMO LA 1
            Ufu. 3:1 – 6, 14 – 2

                  Mimi Yohane, nilisikia Bwana anayeniambia: Kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa. Uwe mwenye kukesha, ukayaimarishe, ukayaimarishe mambo yaliyosalia, yanayotaka kufa. Maana sikuona matendo yako kuwa yametimilika mbele za Mungu wangu. Basi kumbuka jinasi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako. Lakini unayo majina machache katika Sardi, watu wasioyatia mavazi yao uchafu.
Nao watakwenda pamoja nami hali wamevaa mavazi meupe, kwa kuwa wamestahili.
Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Sahahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununu kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri; na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako usionekane; na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidi, ukatubu. Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.

Neno la Bwana  ...... Tumshukuru Mungu

        WIMBO WA KATIKATI
            Zab. 15:1 – 4

         (1).   Bwana, ni nani atakayekaa Katika hema yako? Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, Na kutenda haki.
                       (K) Yeye ashindaye, nitamketisha pamoja nami.
         (2).   Asemaye kweli kwa moyo wake, Asiyesingizia kwa ulimi wake. Wala hakumtenda mwenziwe mabaya. Wala hakumsengenya jirani yake. Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa, Bali huwaheshimu wamchao Bwana.
                       (K) Yeye ashindaye, nitamketisha pamoja nami.
         (3).    Hakutoa fedha yake apate kula riba, Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo hataondoshwa milele.
                        (K) Yeye ashindaye, nitamketisha pamoja nami.

            SHANGILIO
            Lk. 8:15

                    Aleluya, aleluya, Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu, na kulishika. Aleluya.

          SOMO LA INJILI
           Lk. 19:1-10

                Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake.
  Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri.
Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile.
Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha.
Hata watu walipoona, walinung’unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi.
Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.
Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.
Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

Neno la Bwana ...... Sifa kwako Ee Kristu.

Copyright ©2016  by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
    see: imani-katoliki.blogspot.com

Saturday, 12 November 2016

TAFAKARI 12/11/2016 Jumamosi ya 32 ya Mwaka - C

TAFAKARI


Jumamosi, Novemba 12, 2016, Juma la 32 la Mwaka wa Kanisa

Kumbukumbu ya Mt. Josafati, Askofu na Shahidi

3Yn 1:5-8; Zab 111:1-6; Lk 18:1-

KUVUMMILIA KATIKA SALA!

         Katika Injili ya leo, Yesu anatueleza habari ambayo ni kweli kabisa, kuhusu mjane ambaye hakuchoka kumsumbua kadhi dhalimu mpaka alivyompa haki yake. Kuvumilia kunalipa, na hili ni kweli kabisa na hasa kwa wale wanaomwamini Mungu. Yesu anatuelezea ni kwajinsi ghani Mungu alivyo mwepesi wakutuletea haki yake, baraka na msaada tunapo muhitaji. Lakini tunaweza kukata tamaa haraka na kuwa na mioyo hafifu katika kumwomba Baba yetu wa Mbinguni neema zake na msaada. Yesu anawapa matumaini mapya na ujasiri wafuasi wake. Katika maisha ya sasa, tunaweza kukumbana na matatizo makubwa sana na majaribu na magumu mengi lakini hatupaswi kupoteza tumaini la kumwamini Mungu. Hukumu ya mwisho itafunua kwamba haki ya Mungu itakuwa juu ya wasio haki yaliyotendwa na viumbe vyake. Yesu anamalizia kwa swali lakujiuliza sisi, je mimi na wewe tunaimani, Imani inayovumilia mpaka mwisho?


  SALA: Baba Mungu, nisaidie nikuamini wewe na nikutafute wewe kila wakati katika sala bila kuchoka. Amina.

MASOMO YA MISA, 12/11/2016 Jumamosi ya 32 ya Mwaka - C

Jumamosi ya 32 ya Mwaka

     SOMO LA 1
             3 Yn 1:5-8
         Mpenzi, kazi ile ni ya uaminifu uwatendeayo hao ndugu na hao wageni nao, waliokushuhudia upendo wako mbele ya kanisa; utafanya vizuri ukiwasafirisha kama ipasavyo kwa Mungu. Kwa maana, kwa ajili ya Jina hilo, walitoka, wasipokee kitu kwa Mataifa. Basi imetupasa sisi kuwakaribisha watu kama hao, ili tuwe watenda kazi pamoja na kweli.


       WIMBO WA KATIKATI
                  Zab 112:1-6
            Aleluya. Heri mtu yule amchaye Bwana, Apendezwaye sana na maagizo yake. Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
                          (K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
            Nyumbani mwake mna utajiri na mali, Na haki yake yakaa milele. Nuru huwazukia wenye adili gizani; Ana fadhili na huruma na haki.
                         (K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
             Heri atendaye fadhili na kukopesha; Atengenezaye mambo yake kwa haki. Kwa maana hataondoshwa kamwe; Mwenye haki atakumbukwa milele.
                         (K) Heri mtu yule amchaye Bwana.


           SHANGILIO
               Zab. 130:5
                   Aleluya, aleluya, Roho yangu inamngoja Bwana, na neno lake nimelitumainia. Aleluya.


       SOMO LA INJILI
              Lk 18:1-8
                    Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu.
Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.
Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?

Friday, 11 November 2016

TAFAKARI 11/11/2016 Juma la 32 la Mwaka - C " Kujiweka tayari kwa upendo ".


TAFAKARI
      Ijumaa, Novemba 11, 2016,
  Juma la 32 la Mwaka wa Kanisa
    
         Kumbukumbu ya Mt. Martini wa Tours. Askofu.

                 2Yn 1:4-9
           Zab 118:1-2, 10-11, 17-18
                   Lk 17:26-37

             KUJIWEKA TAYARI KWA UPENDO!
        Tunavyokaribia mwisho wa mwaka wa Lirtujia, masomo huwa yana elekeza akili zetu katika maisha ya wakati ujao, maisha baada ya maisha ya hapa duniani. Kwa kila mmoja wetu, anaelewa kwamba kifo chetu binafsi ni mwisho wa maisha yetu hapa duniani na kuingia katika maisha yajayo. Je, kuna mmoja wetu ambaye hana hofu hata kidogo juu ya kufunuliwa wakati wa hukumu kila eneo la mioyo yetu na matendo yetu yote kufunuliwa? Ni kweli kwamba tuna hofu kidogo kama tupo sawa. Yesu leo anatuambia leo tujiweke tayari. Tuna leo tu. Jana imeshapita na haipo juu ya uwezo wetu tena, na kesho haijawapo bado.
Lakini leo ipo hapa mbele yangu. Nina uwezo juu ya siku ya leo. Naweza kuchagua kupenda au kukataa. Naweza kusaidia au kuumiza.
Naweza kuamini au kuwa na wasi wasi. Naweza kutumaini au kuwa na mashaka. Naweza kuishi kwa ajili ya wengine au kuishi kwa ajili ya mimi binafsi. Siku nzima imejazwa na hali zote zinazo niwezesha nipende na kumchagua Mungu. Kama kweli tunampenda Mungu na jirani hatuna haja ya kuogopa kifo na hukumu. Kinacholeta hofu na mashaka ni dhambi.
Dhambi haileti raha inavyokaa moyoni au zinavyokaa moyoni. Tujipatanishe na Mungu daima ili tuishi kwa furaha tukiwa na matumaini ya wakati ujao. Tujiwekee mazoea ya kuijongea sakramenti ya kitubio ili tubaki tukiwa tumeunganika na Mungu daima.
     
           Sala: Bwana nisaidie mimi niweze kujishughulisha kukupenda Wewe na jirani yangu. Amina

Copyright ©2016 shajara  and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
     see:  imani-katoliki.blogspot.com

MASOMO YA MISA, Ijumaavya 32 ya Mwaka - C 11/11/2016.


Ijumaa ya 32 ya Mwaka

      SOMO LA 1
              2 Yn 1:4-9

        Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba.
Na sasa mama, nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane. Na huu ndio upendo: tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo.
Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia.

Neno la Mungu ...... Tumshukuru Mungu.

       WIMBO WA KATIKATI
             Zab 119:1-2, 10-11, 17-18

           (1).    Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana. (K) Heri waendao katika sheria ya Bwana. Heri wazitiio shuhuda zake, Wamtafutao kwa moyo wote.
                    (K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.
           (2).    Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
                    (K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.
           (3).   Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.
                      (K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.
            (4).   Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
                      (K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.
             (5).   Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako.
                      (K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.

        SHANGILIO
                  Zab. 119:28, 33

             Aleluya, aleluya, Unitie nguvu sawasawa na neno lako, Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako. Aleluya.

        SOMO LA INJILI
             Lk 17:26-37

           Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya. Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.
Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.] Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai.

Neno la Bwana ..... Sifa kwako Ee Kristu.

Copyright ©2016. shajara  and  published  by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
   see: imani-katoliki.blogspot.com

Thursday, 10 November 2016

TAFAKARI, 10/11/2016 Alhamisi ya 32 ya Mwaka - C wa Kanisa " Uflme wa Mungu upo kati yetu".


TAFAKARI
        Alhamisi, Novemba 10, 2016 ,
   Juma la 32 la Mwaka wa Kanisa
      
         Kumbukumbu ya Mt. Leo Mkuu, Papa na Mwalimu wa Kanisa.

           Flm1:7-20;
        Zab 145:7-10;
                Lk 17:20-25

          UFALME WA MUNGU UPO KATI YETU.
            Barua ya Mt. Paulo kwa Filemoni, ni barua fupi sana, ina aya tu, lakini ni barua ilioandikwa kwa utaalamu mkubwa.
Mt. Paulo anaianza kwa kukiri uzuri wa Filemoni na kwa jinsi alivyo wawekea na kuwaonesha wema jumuiya ya Kikristo.
Mt. Paulo anasisitiza juu ya Onesimo, ambaye alikuwa mtumwa wa Filemoni, na anamuomba amchukue Onesimo kama ndugu katika Kristo.
Na anamuomba Filemoni amsamehe Onesimo kwa kosa lolote alilotenda kabla. Unaweza kuona ni kwa jinsi ghani Ufalme wa Mungu ulivyowekwa wazi na Paulo.
Ufalme wa Mungu ambao upo wazi kwa kila mtu. Kazi yetu ni kuutambua ufalme huo ndani yetu.

 
          Sala: Bwana Yesu nisaidie mimi niweze kueneza Ufalme wako kwa njia ya maneno na matendo yangu.

Copyright © 2016  shajara  and  published  by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
     see:  imani-katoliki.blogspot.com

MASOMO YA MISA, Alhamisi ya 32 ya Mwaka - C.


Alhamisi ya 32 ya Mwaka

           SOMO LA 1
             Flm 1:7-20

              Nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu. Kwa hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasalo; lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili.
    Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe.
Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu, ukiandike hicho juu yangu. Mimi Paulo nimeandika kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Sikuambii kwamba nakuwia hata nafsi yako. Naam, ndugu yangu, nipate faida kwako katika Bwana; uniburudishe moyo wangu katika Kristo.

Neno la Mungu ...... Tumshukuru Mungu.

         WIMBO WA KATIKATI
      Zab 146:7-10

             (1).   Huwafanyia hukumu walioonewa, Huwapa wenye njaa chakula; Bwana hufungua waliofungwa;
                     (K) Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake.
             (2).   Bwana huwafumbua macho waliopofuka; Bwana huwainua walioinama; Bwana huwapenda wenye haki; Bwana huwahifadhi wageni;
                     (K) Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake.
            (3).   Huwategemeza yatima na mjane; Bali njia ya wasio haki huipotosha. Bwana atamiliki milele, Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. Haleluya.
                      (K) Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake.
     
           SHANGILIO
         Zab. 27:11

                   Aleluya, aleluya, Ee Bwana, uifundishe njia yako, na kuniongoza katika njia iliyonyoka. Aleluya.

            SOMO LA INJILI
                Lk 17:20-25

            Yesu alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu.
   Akawaambia wanafunzi, Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione. Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate; kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake.
Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki.

Neno la Bwana ...... Sifakwako Ee Kristu.


Copyright © 2016  shajara  and  published  by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
     see: imani-katoliki.blogspot.com

Wednesday, 9 November 2016

TAFAKARI Jumatano, Novemba 9, 2016, Juma la 32 la Mwaka wa Kanisa. " Sikukuu ya kutabarukiwa kwa Basilika la Laterani"


TAFAKARI
     
         Jumatano, Novemba 9, 2016,
     Juma la 32 la mwaka wa Kanisa
                Sikukuu ya Kutabarukiwa kwa Basilika la Laterani

         Ez 47:1-2, 8-9, 12;
                Zab 45:2-3, 5-6, 8-9;
         1Kor 3: 9-11, 16-17;
                    Yn 2:13-22


        HEKALU LA MUNGU!
                Katika mwaka 592 Kabla ya kuja Kristo, Eziekeli alikutana na Mungu aliyemtumia kama chombo, kwanza kuwaandaa watu wadhambi kwa maangamizi na baadae kutabiri juu ya utengenezwaji upya wa hekalu. Baada ya muda mfupi 535 BC, ukaanza ujenzi wa hekalu chini ya Zerubabeli aliyerudi kutoka utumwani Babeli na wayahudi zaidi ya 42,000. Ujenzi ulikamilika 518 BC.. Hili hekalu la pili lilijengwa katika hali ya kifahari chini ya Herodi mkuu ambaye alitaka kumua Yesu, kama familia takatifu isingekimbilia Misri. Hili ni hekalu ambalo Wayahudi walifanya sehemu ya kuuzia vitu na Yesu akawafukuza. Alitawanya fedha zao na kupindua meza, akiwatoa ngombe na kondoo njee na alisema “…achene kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa sehemu nyumba ya biashara”. Maneno haya ya Yesu mara nyingi yaliwakasirisha viongozi. Lakini zaidi, jibu la Yesu juu ya wao kutaka ishara ili kutoa ushuhuda wa anayo yafanya ulikuwa juu ya uwezo wao wa kufikiri.
Yesu alikuwa akiongelea kuhusu hekalu ambalo lilikuwa mwili wake mwenyewe, ambao haujajengwa na mawe, lakini wao walikuwa wakiongelea kuhusu hekalu lilojengwaa na Herodi.
Kwa hili hekalu jipya la Agano jipya, Mt. Paulo anasema leo katika somo la pili “hamkujua kwamba miili yenu ni hekalu la Mungu ambapo Roho wa Mungu anaishi ndani yenu?” Mwili wa Kristo (Kanisa) lilizaliwa baada ya mwili wa Yesu kufa pale kalvari na pazia la hekalu kupasuka kutoka juu mpaka chini (Mt 27: 50-51).
Yesu anatuambia leo, sisi pia ni mahekalu ya Roho Mtakatifu, wa Mungu. Tukiwa tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, sisi ni mahekalu yalio barikiwa. Kama viumbe wanao jitambua tunaweza na tunaalikwa kuitikia uwepo wa Mungu ndani mwetu, kuwa hekalu binafsi na katika hali ya pekee.
Leo tukiwa tunasherekea kutabarukiwa kwa basilika la Laterani, mama wa makanisa yote ya Kikatoliki ulimwenguni pote, tujenge tena upya hali ya umoja na mshikamano ambazo zitatujenga na kututambulisha kila wakati kama wajumbe wa mwili wa Kristo.

        Sala: Bwana Yesu, kama ulivyo takasa hekalu, nitakase nami pia, nioshe, nifanye mpya, nifanye nistahili kukupokea. Amina

Copyright © 2016  shajara  and  published  by  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
     see: imani-katoliki.blogspot.com

MASOMO YA MISA Jumatano, 9 2016 " Sikukuu kutabarukiwa Basilika la Laterani".

   
  Sikukuu Kutabarukiwa Basilika la Laterani

        SOMO LA 1
              Eze 43:1-2, 4-7

           Malaika alinileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki; na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling'aa kwa utukufu wake. Na huo utukufu wa Bwana ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki.
Kisha Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa Bwana uliijaza nyumba. Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu akasimama karibu nami. Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele;

     Neno la Mungu ...... Tumshukuru Mungu.

         WIMBO WA KATIKATI
                 Zab 122:1-5, 7-8

       (1).   Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana. Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.
                 (K)Nalifurahi waliponiambia,na twende nyumbani kwa Bwana.
       (2).    Ee Yerusalemu uliyejengwa Kama mji ulioshikamana, Huko ndiko walikopanda kabila, Kabila za Bwana; Ushuhuda kwa Israeli, Walishukuru jina la Bwana.
               (K)Nalifurahi waliponiambia,na twende nyumbani kwa Bwana.
      (3).   Maana huko viliwekwa viti vya hukumu, Viti vya enzi vya mbari ya Daudi. Amani na ikae ndani ya kuta zako, Na kufanikiwa ndani ya majumba yako. Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu Niseme sasa, Amani ikae nawe.
                 (K)Nalifurahi waliponiambia,na twende nyumbani kwa Bwana.
       

           SOMO LA 2
                1Kor 3:9-11, 16-17

           Ninyi ni jengo la Mungu. Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake.
Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo. Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.

  Neno la Mungu ......  Tumshukuru Mungu.

         SHANGILIO
               2 Nya. 7:16

        Aleluya, aleluya, Nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, asema Bwana, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele. Aleluya.


           SOMO LA INJILI
                 Lk Yn 2:13-22

          Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng'ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng'ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara. 
        Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila. Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuonyeshayo, kwamba unafanya haya? Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.
         Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu.

Neno la Bwana ......  Sifa kwako Ee Kristu.

Copyright © 2016  by shajara  and  published  MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
    see: imani-katoliki.blogspot.com

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...