Somo I: 2Fal 5:14-17
Zab/Kit: 98:1-2, 3ab, 3cd-4
Somo II: 2Tim 2:8-13
Injili: Lk 17:11-19
Nukuu
“Ndipo
akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake
yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya
mwili wa mtoto mchanga, akawa safi,” 2Fal 5:14
“Akamrudia
yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele
yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote,
ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa iwako,” 2Fal
5:15
“Na alipoingia katika kijiji kimoja,
alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti
wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!” Lk 17:12-13
“Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika,” Lk 17:14
“Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?” Lk 17:17
“Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu,” 2Tim 2:8
“Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi,” 2Tim 2:9
TAFAKARI:
“Kujishusha na kujinyenyekesha mbele ya Mungu ndio ufunguo wa maarifa na siri ile ihusuyo uzima ule wa milele.”
Wapendwa
wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 28 ya mwaka “C”
wa Kanisa. Na kwa namna ya pekee, Mama Kanisa leo anatutaka kwa pamoja
tutafakari, “unyenyekevu ukiwa ndio msingi wa Fadhila zote, ndio ufunguo
wa maarifa na siri ile ihusuyo uzima wa milele.” Na tufanyavyo hivyo na
kuishi, Mungu atatenda. Masomo yote matatu ya leo yanatuwasa kutafakari
sana tendo hili la unyenyekevu na kujinyenyekesha. Bila shaka wote
twafahamu vizuri habari za Jemadari Naamani, na uponyaji wake kupitia
Nabii Elisha. Safari ya uponyaji wake haikuwa rahisi, kutokana na njia,
na namna ya uponyaji ule ulivyokuwa uwe kwa namna Mungu alivyopenda.
Hata
hivyo mara nyingi hatuyapati yale tuombayo, na hata uponyaji wa yale
yatusumbuayo kutokana na mitazamo yetu kimaisha, na namna tutakavyo
Mungu kufanya huruma na upendo wake kwetu. Mtume Yakobo anasema hivi,
“hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa
tamaa zenu,” Yak 4:3. Kumbe niwapo mbele ya Mungu, ni jambo la msingi na
muhimu sana kujishusha na kujinyekesha huku nikitambua ubinadamu wangu,
na kwa huo ubinadamu sote ni wahitaji na waja wa Mungu.
Mungu
utukweza tu pale tunapojishusha na kujinyenyekesha kwake na kuukubali
ubinadamu wetu. Mungu daima anabaki kuwa Mungu. “Kwa maana kila
ajikwezaye atadhiliwa, na ajidhiliye atakwezwa,” Lk 14:11. Mtoza ushuru
katika sala yake hekaluni, kinyume na Mfarisayo, sala yake (Mtoza
ushuru) ilisikika mbele ya Mungu kwa sababu alijishusha na kusema kwa
unyenyekevu na kwa uchache wa maneno kabisa, “Ee Mungu, uniwie radhi
mimi mwenye dhambi,” Lk 18:13. Kwa tendo hili la unyenyekevu la
mtoza ushuru, Yesu anasema, “Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani
kwake amehesabiwa haki kuliko yule; (Mfarisayo) kwa maana kila
ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa,” Lk 18:14
Jemadari
Naamani anapata uponyaji wa ukoma wake baada tu ya kujishusha na
kufanya kadiri ya mapenzi ya Mungu. “Ndipo akashuka, akajichovya mara
saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama
ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa
safi,” 2Fal 5:14. Ndugu yangu, Mungu ana njia nyingi na mbalimbali za
kufikishia ujumbe wake kwetu kadiri ya hitaji letu, na kwa kupitia jambo
hilo au uponyaji huo iwe au liwe somo la maisha.
Mwanzoni
tunaona Naamani anashindwa kupokea njia ya uponyaji ule, yaani,
kujichovya mara saba katika mto Jordani, kwa kujitazama historia yake,
na ufahamu wake. Mpendwa, “Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili
zake hazina mipaka,” Zab 147:5. Hatuwezi kumpangia Mungu namna ya
kufanya hata kama tukiwa na nia njema afanye yale tumwombayo na
tunayotamani.
Ndugu yangu, hata Yesu
mwenyewe, alimwachia Baba yake-Mungu atende kadiri ya mapenzi yake.
“Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba
yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo
mimi, bali kama utakavyo wewe,” Mt 26:39. Kama huyu, yaani, Mwana wa
Mungu na Mwenye Uweza wote anajinyenyekeza na kujiachia mikoni mwa Baba
yake, mimi na wewe tuna nini cha kujikweza hata kama historia yetu
inaonyesha hatujawahi kushindwa?
Naamani
Jemadari, anapojishusha, jinyenyekeza, na kumwachia Mungu atende kadiri
ya neno lake kupitia Mtumishi wa Mungu Nabii Elisha, Mungu anatenda mara
moja. “Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa
na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa
nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi,” 2Fal 5:14. Kujinyenyekesha
na kujishusha ni kukiri Ukuu wa Mungu kabla na baada atendapo mema yake
kwako. Uponyaji wa Naamani Jemadari, unaibua hisia za uchaji na
utambuzi wa Mungu huyu wa Ajabu, na kusema, "Sasa tazama, najua ya
kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli,” 2Fal 5:15.
Ndugu
yangu, tunachojifunza katika maisha yetu ya sala na unyenyekevu ni
kwamba tunapokuwa mbele ya Mungu yatupasa kujua kwamba sisi ni viumbe
tu, na wahitaji na waja wake Mungu. Mungu haitaji kujua mazuri yetu kwa
sababu hayatampunguzia Wema, Upendo, Uzuri, na Ukuu wake. Mungu pia
haitaji historia ya yale tuyafanyayo kama alivyofanya Mfarisayo, bali
tusiache kutenda mema kwani Yeye aliye Mwema katika yote na uzuri wote
ataonekana katika matendo hayo mema, na hasa tunapoyatenda kwa wale
aliowaumba kwa sura na mfano wake.
Naamani
baada ya kutendewa tendo hili kuu na Mungu kupitia Nabii wake Elisha,
anataka kumtolea Elisha kitu kama tendo la shukrani. Elisha anakataa
tendo lile kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kujifananisha na Mungu.
Elisha kwa unyenyekevu anatambua nafasi yake kama mtumishi tu, tena
asiye na faida. Katika tendo hili la Nabii Elisha, tunajifunza pia kile
anachotufundisha Kristo Yesu kuhusu utumishi. Naye Yesu anasema, “vivyo
hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu
watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10.
Hakika yatupasa kutumika na siyo kutumikiwa.
Kutokana
na msimamo wake Elisha, tendo lile la kukataa kutolewa kitu linagusa
mtima wa Naamani, naye anaweka ahadi yake kwa Mungu aliye hai. Naye
anasem, “Kama sivyo (kutokupokea kitu), lakini mtumwa wako na apewe
mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena
sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa Bwana,”
2Fal 5:17. Tumwache Mungu aitwe Mungu, na ndivyo alivyo.
Ni
kwa upendo wake Mungu katuumba kama tulivyo, yaani, kwa sura na mfano
wake, na ndivyo tulivyo wanadamu. Na kuishi ubinadamu wetu kwa uaminifu
na hofu ya Mungu kwa lengo lile alilotuumba, yaani, tumjue, tumpende,
tumtumikie, na mwisho turudi kwake mbinguni, ndipo lilipo taji letu,
yaani, utakatifu wako. Ni utakatifu huo ambao ndio cheo chako ndio
wezesho la wewe kuuona uso wa Mungu. Bila utakatifu huwezi kumwana
Mungu, kwa sababu Yeye ni Mtakatifu.
Hivyo ni
mwaliko kwako na mwangu leo na kila kutenda kama wa watoto wachanga.
Watoto wachanga ndiyo hufunuliwa mambo ya Mungu kutokana na kujiaminisha
pasipo shaka kwa wazazi wao. Katika hili Yesu anasema, “Nakushukuru,
Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye
hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga,” Mt 11:25. Utendaji huu
kama watoto ndio utupao fursa ya kuurithi ufalme wa Mungu. “Waacheni
watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao,
ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 19:14.
Mwisho
wa siku ndugu yangu, “tutahukumiwa au kutathminiwa kwa upendo wetu,”
kama asemavyo Mtakatifu Yohana wa Msalaba. Kwa hiyo, yale yote tufanyayo
na tujihesabie tu kuwa tumefanya yale yampendezayo Mungu. Hatuna
chochote za kujivunia mbele ya Mungu zaidi ya kujishusha na
kujinyeyekesha. Mafanikio yetu ni moja ya uzuri wake Mungu. Mapungufu
yetu ni sababu ya ubinadamu wetu, na katika kujishusha na kujinyenyekeza
mbele zake Mungu hatachoka kuzifungua neema na huruma yake kwetu. Mtume
Paulo anasema, “Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho
chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu
umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Kumbe mimi kama
Mkristo kujivuna kwangu iwe Msalaba wake Kristo kwani hakuna Utukufu
pasipo Msalaba.
Katika
jambo hili ndugu yangu, yatupasa kujua kwa uhakika kwamba Yesu Kristo
ndiye kielelezo cha UNYENYEKEVU. Kifo cha Msalaba na cha Aibu ni kwa
sababu yangu na wewe. Basi, tujivunie tu Msalaba kwani kwayo kuna
Utukufu. Vingine vyote ni vya kupita tu. Mtume Paulo anatuambia makusudi
ya Yesu kufanya hayo yote ni kwamba, “ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna
namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha
kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya
mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu, tena, alipoonekana ana umbo kama
mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya
msalaba,” Flp 2:6-8. Je, ndugu yangu, una cho chote cha kujivunia na na
kukufanya kutokushuka na kujinyenyekesha kwa Mungu?
Katika Injili ya leo tunaona ‘fanya zaidi’ ya waleo wakoma kumi walivyo yakazi macho yao kwa Kristo Yesu, na kwa ummoja wao, “wakapaza
sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!” Lk 17:13. Ndugu
yangu, lazima ufahamu msaada wako unatoka wapi hasa pale unapoona giza
tupu katika maisha yako. Uponyaji wa wakoma hawa ni tofauti kabisa na
ponyaji nyingine alizokwisha kuzifanya Yesu. Yesu anawataka ‘kufanya
zaidi’ na kuwaambia, “Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa
walipokuwa wakienda walitakasika,” Lk 17:14. Wakoma hawa wanatakasika
wakiwa njiani. Kumbe wakati mwingine kupona kwako kwaweza chukua hatua
kwa lengo la kukuimarisha kiimani, na kukupatia utakaso kamili. Kumbe
yote ni neema na heri, na kamwe nisilitoe tumaini langu kwa yule anipaye
uzima huo, yaani, Mungu muumba wangu.
Katika
tendo hili la uponyaji lililo la baraka na neema, unyenyekevu
unajidhihirisha kwa tendo la shukrani. Ni mambo mangapi tunakutana nayo
njiani ya neema na baraka ila hatuoni sababu ya kushukuru? Ni mmoja tu
kati ya wale kumi aliyekuja kwa Yesu na“akaanguka kifudifudi
miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria,” Lk 17:16. Tendo hili
linamshangaza sana Yesu, naye akamjibu, “Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?,” Lk 17:17.
Ona
jinsi tunavyomshangaza Mungu tunavyokoswa moyo wa shukrani kwa yale
anayotutendea. Ndugu yangu tuliyesafiri pamoja katika tafakari hii, bado
tu hauna cha kumshukuru Mungu?
Jambo lingine
la pekee katika tukio hili la uponyaji ni kile mtu apatacho mwisho wa
uponyaji huo. Wale tisa ambao hawakuja kutoa shukrani walipokea uponyaji
wa mwili, na kuwa huru kutoka mateso yale ya ukoma. Ni huyu mmoja tu,
tena Msamaria aliyepata vyote, yaani, uponyaji wa mwili na wokovu.
Katika kweli hii Yesu anamwambia, “Inuka, enenda zako, imani yako
imekuokoa,” Lk 17:19. Hakika moyo usio na shukrani ukausha mema yote!
Tunapoutazama kwa ukaribu uhusisano kati ya Wayahudi na Wasamaria,
katika uponyaji huu unaweka wazi maneno haya ya Yesu, kwamba, “vivyo
hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho,” Mt
20:16. Mungu wetu hana upendeleo, Mdo 10:34-35, hasa pale
tunapomwelekea kwa hofu na uchaji wa kweli.
Wapendwa
wana wa Mungu, mwanadamu kwa kuumbwa kwake, Mwa 1:27, na uwepo wake
hapa duniani, mara zote hutafuta maana ya maisha yake. Hufanya hivyo si
kwa bahati mbaya, au udadisi fulani usio na mwalekeo, bali kama alivyo,
mwanadamu usukumwa kufanya hivyo kama tokeo la historia yake kijamii na
jamii anayoishi leo na sasa. Hivyo, mwanadamu huyu hapo alipo kadiri ya
imani na maadili yake, hakosi kuifikiria kesho ambayo bado kuiishi
akiwa na matumaini kuwa ipo na yaja.
Na kama
ni Mkristo achoki kuyafikiria maisha yale ya umilele na hukumu yake ya
mwisho, kwa sababu anatambua wazi maisha ya hapa duniani ni jukumu la
muda mfupi tu.“Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa
mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo
aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya,”
2Kor 5:10. Kwa hali hii, mazingira haya, na mtazamo huo, mwanadamu
hakosi kutafuta maana ya maisha yake. Utafutaji wa maana juu ya maisha
yake humpa pia maana ya mahangaiko na mateso yake.
Katika hali hii Mtume Paulo anasema, “Nami
katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la
Mungu halifungwi,” 2Tim 2:9. Neno la Mungu ni hai, na pia ni uhai.
Tulisadiki neno kama alivyofanya Diwani yule wa Kana ya Galilaya, Yoh
4:46, mwanaye aliyekuwa hajiwezi, naye akapata uponyaji. “Yesu akamwambia, Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia,” Yoh 4:50
Maisha
yakikosa maana, binadamu hujikabidhi katika ‘ovu’ lolote lile bila
kujali chochote kwa sababu maisha yake kesha yahesabu kuwa si chochote.
Huku ni kutaka tamaa pale tunapokosa tumaini la kweli. Matendo ya uovu
tunayoyashuhudia kila siku katika jamii yetu ni ishara ya watu kukata
tamaa na kupoteza tumaini la kweli katika maisha yao. Ni vyema kama
jamii tukajiuliza ni wapi tulipoupoteza ufunguo huo wa tumaini la kweli.
Utoaji wa matamko kila siku na kwa kila tukio bila ukomo kamwe hatuta
upata ufunguo huo wa tumaini la kweli. Kumbe yatupasa kila mmoja na kwa
nafasi aliyokuwa nayo katika jamii, ikiwa ni pamoja na wale wenye weledi
wa mambo haya ya kijamii kufanya tathmini ya kina kuhusu mwenendo mzima
wa jamii yetu leo. Swali ni hili: Kwa nini tunafanya kama tunavyofanya?
Tunapo
mtazama Mtume Paulo tunagundua kuna kitu tofauti. Yesu Kristo ndiye
nahodha wa maisha yake, na kwake, yaani kwa Kristo, maisha yake (Paulo
Mtume) yamepata maana halisi. “Kwa ajili ya hilo nastahimili
mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio
katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa.
Kwa
maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; Kama
tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye
atatukana sisi; Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana
hawezi kujikana mwenyewe,” 2Tim 2:10-13. Huyu ndiye Kristo ambaye kwake
kama wafuasi wake, kuna tumaini la kweli.
Hata pamoja na ukweli huo, “Jitahidi
kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya
kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli,” 2Tim 2:15. Ndani na
katika Yesu Kristo hakuna sababu ya kuishi kwa hofu. Na kujishusha na
kujinyenyekesha mbele ya Mungu ndio ufunguo wa maarifa na siri ile
ihusuyo uzima ule wa milele.
Basi nikuache na
mfano huu: ‘kwa wale ambao ni madereza, na hata sisi ambao ni wasafiri
tu, bila shaka tumewahi kukutana na kitu kinachoitwa “shokamzoba.”
Shokamzoba ni aina ya chuma fulani imara na chenye umbo la kujisokota
katika mtindo wa duara na kufanya mnaso fulani.
Pamoja
na kazi kubwa ya shakamzoba kuzuia uharibufu au uvunjikaji wa vitu
vilivyo kwenye mwendo, shokamzoba utujengea hisi fulani tofauti ya pale
tulipo na kile kinachoendelea nje ya mazingira yale tuliyopo. Mara
nyingi katika kweli hii wengi hatuguswi kwa sababu utulivu tulionao
wakati huo upoteza kweli hii. Katika hali hii ya utulivu ilhali tupo
kwenye mwendo kasi, shokamzoba huwa mwimili wa kila kitu.
Hivyo
vyote vibebwavyo juu yake hubaki salama tu iwapo shokamzoba hizi
zitabaki katika hali yake ya usalama. Katika maisha ya mwanadamu,
shokamzoba ndiyo fadhila kuu ya unyenyekevu. Bila unyenyekevu, yote
tuyajengayo juu yake, yaani, fadhila nyingine zote, hukosa msingi
imara.
Kuijenga jamii mpya na yenye mwelekeo chanya, mimi na wewe lazima yatupasa pasipo shuruti kuwa shokamzoba.’
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi,” 2Tim 2:9
Tusali:- Ee Yesu Mwema, nijalie fadhila ya Unyenyekevu. Amina
Copyright © 2016 by Fr Edgar Tanga Ngowi, OSA and. Published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG