Saturday, 7 July 2018

TAFAKARI YA MASOMO YA MISA, DOMINIKA YA 14 YA MWAKA, "B"

MBEGU ZA UZIMA
    Julai 8, 2018
  Dominika ya 14 ya Mwaka
       Eze 2:2-5
       Zab 123 (K. 2);
        2 Kor 12:7-10;
         Mk 6:1-6.
 
     KUTESEKA KWA NABII
                 Watu wengi ambao ni wakuu katika sehemu nyingi wamepeita mateso na changamoto mbali mbali na hivyo hata kuvishinda na kusimama imara.
        Huenda, watu wao wenyewe waliwakataa na walikuwa na wakati mgumu sana kuikabili jamii. Wale wote waliotumwa na Mungu nao pia wanakutana na magumu.
          Hata Mwana wa Mungu, ambaye watu walimsubiri kwa muda bado alipokuja walimpinga na hata watu wa nyumbani kwake hawakumuelewa.
        Katika somo la kwanza, Ezekieli anakuwa kama chombo cha Mungu cha amani, akiwa kama balozi wa Mungu kati ya watu wake katika miaka hiyo kabla na baada ya Wayahudi hawajaanguka kwa Wababiloni. Manabii walipewa nguvu ya Roho wa Mungu kubainisha ukweli na haki na uaminifu katika hali ambayo sifa hizi zilifunikwa kwa uongo, ukosefu wa haki, na kutokuwa na imani kwa vizazi kadhaa. Unabii Wake ulikuwa katika hali husika ya kitaifa hususani ya kisiasa na ya kidini. Watu walikuwa wasumbufu kwasababu hawakutaka kumsikiliza Mungu.
   
        (Ez 3:7). “Usiwaogope hao, wala usiyaogope maneno yao.” (Ez 2:6). Wanaweza wasiyaogope maneno yako, lakini walau “watajua yakuwa nabii amekuwapo miongoni mwao.” (Ez 2:5). Huu ni wito wa nabii.
          Ni mtu ambaye Mungu ameudhihirisha ukweli wake ili kuuwasilisha kwa watu wake.
 
        Katika somo la pili, Paulo anaelezea upinzani wake. Inawezekana pia Paulo aliyafikiria matatizo mengi ya kichungaji yaliyolikabili kanisa la Korintho kama ni mwiba katika nyama yake. Mwanzo aliuliza kuwa mwiba huu utolewe kwake, lakini mwishowe aliukubali, na hata kutukuzwa katika kejeli, mateso, na magumu ambayo aliteseka nayo kwa ajili ya Kristo (2Kor 12:10).

         Katika Injili, tunaona kukataliwa kwa Yesu na ndugu zake wa mitaa yake.
        Zaidi ya hili, Yesu alikutana na vikwazo kutoka katika mamlaka ya Wayahudi.
        Marko anahesabu muendelezo wa matukio matano ya upinzani ambapo Yesu ilimpasa ajitetee yeye mwenyewe: nguvu yake ya kusamehe dhambi (2:1-12); upendo wake kwa watoza ushuru na wadhambi (2:13-17); mitazamo yake juu ya kufunga (2:18-22); uelewa wake juu ya usafi wa utamaduni (2:23-28); na nguvu zake za kuponya siku ya Sabato (3:1-6).

        Katika Injili ya leo, ni kusanyiko la watu wa nyumbani ndio waliomsaliti Yesu. Alipitia kile walichokipitia Isaya, Yeremia na Ezekieli – yakuwa nabii hakubaliki nyumbani kwake. Ingawa watu wa Nazareti walifurahishwa sana na mafundisho ya kukubali asili yake ya miujiza na matendo yake, hawakuenda mbali na kushangawa kwao. Badala yake, waliishia kuoanza kutazama hali yake ya zamani na familia aliotoka.
        Badala ya kuwa na Imani wanaanza kuangalia mambo ya nje ambayo sio muhimu kwa wokovu wao.
         Wanashindwa kupokea ujumbe wa kiroho. Pengine nasi tunaweza kuwa kama watu wa Nazareti, tukawa tumejijengea kwamba unabii wa kweli hauwezi kutoka sehemu fulani au tukashindwa kupokea ukweli kwasababu tunadhani huyu hawezi kutuambia kitu. Pengine Padre fulani, ulimuona akikuwa au akiwa mseminari na sasa anakuhubiria unaanza kusema haka katoto kajuzi mbona nakifahamu vizuri hakina lolote? Tuangalie sana tusije tukamfukuza Yesu katika maisha yetu akashindwa kutenda miujiza akaenda kutenda miujiza sehemu nyingine. Katika hali ya leo pia, hali haijabadilika.
        Tumeitwa kuwa manabii kwa watu wetu wenyewe, huenda ikahitaji kusimama kwa ajili ya matendo maovu ndani ya jamii, kuongea kwa ajili ya watu wasio na sauti au kuwatetea masikini na wananyanyaswaji.
         Tunapaswa kujiandaa na hata kutukanwa. Huu ndio wito wetu. Wito wetu wakushiriki katika unabii ya Kristo.

       Sala: Bwana, niimarishe mimi katika utume wangu kama nabii nihubiri ujumbe wako.

Copyright ©; 2018 by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG
see: imani-katoliki.blogspot. com

MASOMO YA MISA LEO

MASOMO YA MISA, JULAI 8, 2018 DOMINIKA YA 14 YA MWAKA B

       SOMO 1 Eze. 2 :2-5 
                  Bwana aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami. Akaniambia, Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi, wao na baba zao wamekosa juu yangu, naam, hata hivi leo.
          Na wana hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana Mungu asema hivi. Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao.

      Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.

       WIMBO WA KATI KATI 
                 Zab. 123 (K) 2 
          (K) Macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu.


       (1). Nimekuinulia macho yangu, Wewe uketiye mbinguni. Kama vile macho ya watumishi Kwa mkono wa bwana zao. Kama macho ya mjakazi Kwa mkono wa bibi yake; Hivyo macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu. Hata atakapoturehemu. (K)

       (2).  Uturehemu, Ee Bwana, uturehemu sisi, Kwa maana tumeshiba dharau. Nafsi zetu zimeshiba mzaha wa wenye raha, Na dharau ya wenye kiburi. (K)
     
        SOMO 2 
            2 Kor 12:7-10 
         Makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili; mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. 
  Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. 
      Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo.
       Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.

     Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
        SHANG1LIO
               Yn. 14:23 
          Aleluya, aleluya, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake. Aleluya.

       
          INJILI
            Mk. 6:1-6
            Yesu alitoka, akafika mpaka nchi ya kwao, wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipowa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yaoYakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake.
     Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko; isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache akawaponya. 
     Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao.
       
           Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristu.

Copyright ©: 2018  by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG

Thursday, 5 July 2018

MASOMO YA MISA

MASOMO YA MISA, JULAI 6, 2018 IJUMAA, JUMA LA 13 LA MWAKA


     SOMO 1 
Amo. 8:4 – 6, 9 – 12
           Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi, tupate kuuza kuuza nafaka? Mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu, tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano. 
         Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana Mungu, nitalifanya jua litue wakati wa adhuhuri, nami nitaitia nchi giza wakati wa nuru wa mchana. 
         Nami nitazigeuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio; nami nitatia nguo za magunia katika viuno vyote, na upaa katika kila kichwa; nami nitayafanya haya kuwa kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu. Angalia, siku zinakuja, asema Bwana Mungu, ambazo nitaleta njaa katika nchi, si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana.
           Nao watatangatanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazini hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione. 
       
       Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.



       WIMBO WA KATIKATI
        Zab. 119:2, 10, 20, 30, 40, 131
(K) Mt. 4:4

                        (K) Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

         (1). Heri wazitiio shuhuda zake, wamtafutao kwa moyo wote. Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, usiniache nipotee mbali na maagizo yako. (K)

         (2). Roho yangu imepondeka kwa kutamani, hukumu zako kila wakati. Nimeichagua njia ya uaminifu, na kuziweka hukumu zako mbele yangu. (K)

         (3).  Tazama, nimeyatamani mausia yako, unihuishe kwa haki yako. Nalifungua kinywa changu nikatweta, maana naliyatamani maagizo yako. (K)


           SHANGILIO
                 Zab. 147:12, 15 
          Aleluya, aleluya, Msifu Bwana, Ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi. Aleluya.



               INJILI
                      Mt. 9:9 – 13 
         Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata. 
         Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. 
          Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.


       Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristu.


  Copyright ©: 2018 by shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG.

HISTORIA YA MT. MARGARETA MARIA ALAKOK, MTAWA.

Historia ya Mt. Margareta Maria Alakok, Mtawa
    
            Kule Ufaransa katika karne ya 17, upendo kwa Mungu ulikuwa umepooza sana.
     Watu wengi waliuacha mwenendo wa kikirstu na wengine waliukubali uzushi wa Jansenio aliyehubiri kwamba Mungu hawapendi watu wote sawa, bali anawapenda wengine, na baadhi yao anawaacha kabisa.

        Ili kuwaamshia wakatoliki upendo kwa Mungu, watakatifu watatu hasa walioishi kati ya miaka 1625 na 1690, walliieneza, kwa bidii sana, ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, nao ni Mt. Yohani Eudes (1610-1680).Margareta Maria alizaliwa katika nchi ya Ufaransa mwaka 1647.
        Baada ya kifo cha baba yake, wakamwingiza katika shule ya shirika la Mt. Klara. Alipokuwa na umri wa miaka kumi na mmoja alishikwa na ugonjwa na kwa sababu hiyo hakuweza kutembea kwa muda wa miaka minne. Kisha kupona, alianza kuzipendelea anasa za ulimwengu, kwa kuvaa kimalidadi. Bwana wetu alimtokea akamwambia.     "Ukiniacha mimi na kutaka mchumba mwingine, mimi nitakuacha kwa siku zote".

          Margareta alisikiliza mashauri ya Yesu na alipokuwa na umri wa miaka ishirini na miwili, akaingia katika shirika la masista wa Maonano (Visitation Sisters) huku Paray-le-Monial (Ufaransa).Mwaka 1673, alipokuwa akisali mbele ya Saktramenti Kuu Bwana Yesu alimtokea akamwonyesha moyo wake akisema:
      “Tazama moyo wangu unaowaka mapendo kwa watu.Ningetaka kuwafumbulia watu moyo wangu, na kuwagawia neema zote zilizomo".
       
         Siku nyingine, Mwokozi alimtokea akamwonyesha vidonda vitano mwilini mwake akisema:
         "nimewapenda watu kwa mapendo makubwa. Lakini watu hawana shukrani. Laiti watu wengi wangeyafikia mapendo yangu, ningekuwa tayari kufanya zaidi, na kufanya bado zaidi kwa ajili yao. Lakini watu wanaonionyesha ubaridi na ugumu wao. Ewe mwanangu, unifurahishe kidogo pahali pa wakosefu hao".

     Mwezi Juni mwaka 1675, Bwana wetu alimwonyesha tena moyo wake akisema: “Ndio moyo huu unaopenda sana watu, na watu hawaupendi. Kwa Masomo ya Misa za kila siku.

         Kwa Masomo ya misa na Sala mbalimbali na historia za maisha ya Watakatifu tembelea: MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG.

Monday, 2 July 2018

MASOMO YA MISA JUMATATU YA 13 YA MWAKA. 'B' WAKANISA.

          Masomo ya Misa 02/07/2018

                 Somo la Kwanza
               Amo. 2:6 – 10, 13 – 16
         Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Israeli, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu; nao hutwetea kuipotosha njia ya mwenye upole; na mtu na baba yake humwendea mwanamke mmoja, hata kulitia unajisi jina langu takatifu; nao hulijaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha. Lakini nalimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini naliyaangamiza matunda yake toka juu, na mizizi yake toka chini.
          Pia naliwapandisha ninyi kutoka nchi ya Misri, nikawaongoza muda wa miaka arobaini jangwani, ili mpate kuimiliki nchi ya Mwamori. Tazameni, nitawalemea ninyi, kama gari lilemeavyo lililojaa miganda. Naye apigaye mbio atapotewa na kimbilio; Wala aliye hodari hataongeza nguvu zake; Wala shujaa hatajiokoa nafsi yake; Wala apindaye upinde hatasimama; Wala aliye mwepesi wa miguu hataokoka; Wala apandaye farasi hatajiokoa nafsi yake; Naye mwenye moyo mkuu miongoni mwa mashujaa atakimbia uchi siku ile, asema Bwana.
  Neno la Bwana. Tumshukuru Mungu.

    Wimbo wa katikati
            Zab. 50:16 – 23
      (1). Mtu asiye haki, Mungu amwambia, Una nini wewe kuitangaza sheria yangu, Na kuliweka agano langu kinywani mwako? Maana wewe umechukia maonyo, Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

         (K) Yafahamuni hayo, ninyi mnaomsahau Mungu.
   
       (2).  Ulipomwona mwivi ulikuwa radhi naye, Ukashirikiana na wazinzi. Umekiachia kinywa chako kinene mabaya, Na ulimi wako watunga hila.

           (K) Yafahamuni hayo, ninyi mnaomsahau Mungu.
   
       (3).  Umekaa na kumsengenya ndugu yako, Na mwana wa mama yako umemsingizia. Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza; Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe. Walakini nitakukemea; Nitayapanga hayo mbele ya macho yako.
  
           (K) Yafahamuni hayo, ninyi mnaomsahau Mungu.

          (4). Yafahamu hayo, Ninyi mnaomsahau Mungu. Nisije nikawararueni, Asipatikane mwenye kuwaponya. Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.

             (K) Yafahamuni hayo, ninyi mnaomsahau Mungu.
 
       Shangilio
               Yn. 14:5
          Aleluya, aleluya. Bwana anasema: mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Aleluya.
  
          Somo la Injili
               Mt. 8:18 – 22
          Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng’ambo. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata kokote uendako. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.
    Neno la Bwana. Sifa kwako Ee kristu.

     Copyright ©: 2018.  by  Shajara and published by MAMBO YAHUSUYO IMANI BLOG.
see: imani-katoriki.blogspot.com

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...