Saturday, 7 January 2017

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU, Sherehe ya Tokeo la Bwana (Epifania)


Januari 8, 2017. 

Sherehe ya Tokeo la Bwana (Epifania)

Isa 60: 1-6; 
Zab 72: 1-2, 7-8, 10-13; 
Efe 3: 2-3, 5-6; 
Mt 2: 1-12.


ZAWADI KWA DUNIA NZIMA!

         Katika somo la kwanza, katika ono lake la kinabii, Isaya anaona ujio wa Mungu ulimwenguni. Utakuja muda ambapo watu wote wataletwa pamoja mbele ya Bwana na watabarikiwa sana. Utukufu wa Bwana utashuka ulimwenguni na utukufu wake utauzunguka uumbaji wote.
Tukio hili takatifu litalibadilisha jiji la Yerusalemu na wale wote wanaofanya kazi na kuvumilia watapokea mwanga wa uhai. 
Katika somo la pili, Paulo anaifumbua siri ambayo Mungu anaitoa kwa utukufu wake watu wote pamoja na wapagani, kuwafanya warithi wa ufalme wake. Anasema “sasa imefunguliwa kuwa wapagani wanashiriki urithi ule ule”. Ukombozi wa ulimwengu, Mungu pia anawapenda wasio Wakristo kwani wao pia ni wapokeaji.  
Leo tunasherehekea sherehe ya Tokeo la Bwana. Ni sherehe ya dhihirisho la Bwana wetu kwa watu wa Mataifa. Kulikuwa na mamajusi watatu kutoka mashariki waliokuja kwa Mfalme mpya aliyezaliwa. Mamajusi hawa, watu wa mataifa, ambao hawakuwa katika utajiri wa pamoja wa Waisraeli, walikuwa ni watu waliosoma nyota kwa lengo la kubaini siri na ujumbe wake. Walipokuja katika mahakama ya mfalme, walimuuliza Herode, yuko wapi mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa? Hawakuuliza kama mfalme wa wayahudi amezaliwa? Walikuwa na uhakika kuwa mfalme alikuwa amekwisha zaliwa. Walikuwa tu hawana uhakika wa sehemu yake alipozaliwa, bali juu ya ukweli kwamba amezaliwa walikuwa nao.  
Kama tu vile Yeye alivyo jidhihirisha Yeye Mwenyewe kwa wale mamajusi, kila siku Mungu anajidhihirisha mwenyewe kwetu sisi katika Ekaristi Takatifu. Tunamtukuza Yeye, tunamshukuru na kumfanya yeye afahamike ulimwenguni kote. Basi tujitoe sisi wenyewe kama zawadi na tuunganike naye na  kuhubiri:Mungu amejidhihirisha mwenyewe duniani. Yesu anajitoa mwenyewe zawadi kwa dunia nzima.

Sala: Bwana, niwezeshe niweze kujitoa Mimi mwenyewe kama zawadi kwako. Amina..

MASOMO YA MISA JANUARI 8, 2017SHEREHE YA EPIFANIA


MASOMO YA MISA JANUARI 8, 2017

SHEREHE YA EPIFANIA


SOMO 1
Isa. 60:1-6
       Ondoka, ee Yerusalemu, uangaze; Kwa kuwa nuru yako imekuja. Na utukufu wa Bwana umekuzukia. Maana, tazama, giza litaifunika dunia, Na giza kuu litazifunika kabila za watu; Bali Bwana atakuzukia wewe, Na utukufu wake utaonekana juu yako. Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako. Inua macho yako, utazame pande zote; Wote wanakusanyana; wanakujia wewe; Wana wako watakuja kutoka mbali, Na binti zako watabebwa nyongani. Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa utakuwasilia. Wingi wa ngamia utakufunika, Ngamia vijana wa Midiani na Efa; Wote watakuja kutoka Sheba; Wataleta dhahabu na uvumba; Na kuzitangaza sifa za Bwana.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 72:1-2, 7-8, 10-13 (K) 11
(K) Mataifa yote ya ulimwengu, watakusujudia, ee Bwana.
       (1).   Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako.
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)
       (2).   Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa Amani hata mwezi utakapokoma
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka mto hata miisho ya dunia. (K)
      (3).   Wafalme wa Tarshisi na visiwa walete kodi,
Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.
Naam, wafalme wote na wamsujudie;
Na mataifa yote wamtumikie. (K)
     (4).   Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)


SOMO 2
Efe. 3:2-3, 5-6
Ndugu zangu: Ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo.
Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO
Mt. 2:2
Aleluya, aleluya,
Tuliona nyota yake mashariki, Nasi tumekuja kumsujudia.
Aleluya.


INJILI
Mt. 2:1-12
Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, ansi tumekuja kumsujudia. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao: Kristo azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika Bethlemu ya Uyahudi; kwa maana ndiyvo ilivyoandikwa na nabii, Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda, Kwa kuwa kwako atatoka mtawala atakayewachunga watu wangu Israeli.
Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota, Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie. Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, hata ikaenda ikasimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo

NYIMBO ZA DOMINIKA YA 29 YA MWAKA- C WA KANISA.

Nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka C Karibu kwa ajili ya nyimbo za Jumapili ya 29 Mwaka "C" Mwanzo: Ee Bwana Nimekuita  ...